IDADI ya Watanzania wanaokula mlo mmoja kwa siku inazidi kuongezeka baada ya kuwepo kwa ugumu wa maisha unaotokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ukosefu wa ajira, mabadiliko ya hali ya hewa, kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu – ikiwamo chakula.
SAUTI KUBWA inaweza kuthibitisha pasipo shaka kwamba maisha ya Watanzania wengi yameendelea kuwa magumu kufuatia majibu ya dodoso 1,100 ambazo zilisambazwa kwa baadhi ya wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Mwanza na Mtwara. Kila mkoa ulipewa dodoso 220 ambapo watu wa idadi hiyo waliohojiwa.
Asilimia 37 ya waliohojiwa, sawa na watu 407 walidai familia zao zimeacha kula mara tatu kwa siku kutokana na kuwepo ugumu wa kupata fedha za kukidhi mahitaji ya familia na hasa chakula, kulipa pango, matibabu na usafiri wa kwenda kusaka “vibarua” na kurejea nyumbani.
Dodoso hizo ambazo hazikulazimisha wahojiwa kutaja majina, zinaonyesha wenye familia, waliokuwa na umri kati ya miaka 36 hadi 51 (wengi wakiwa ni wanaume), walisema kuwa familia zao zinaanza kuzoea kula mara moja tu kwa siku, tofauti na mazoea ya wananchi wengi kula milo mitatu kwa siku. Waliohojiwa waliandika kwa maandishi na wengine walichagua kuzungumza na maelezo yao kuchukuliwa.
“Mimi nalazimika kula mara moja tu, mchana saa 9 na usiku nakunywa maji au chai na kulala, hata sasa tumbo langu limezoea,” amesema mkazi mmoja wa Mabatini, Mwanza.
Akieleza sababu anazodhani zimesababisha maisha kuwa magumu, mwananchi huyo alisema ni kupanda kwa bei ya mafuta kulikosababishwa na vita vya Russia na Ukraine.
Mwananchi mwingine kutoka Mtwara ameeleza kwamba familia yake ya watu watano inalazimika kula mara mbili; kifungua kinywa na chakula cha mchana. Anasema alizoea kula mara tatu kwa siku, lakini kwa ugumu wa maisha, hawezi kwa sasa.
Anasema, kati ya watu watano wa familia yake ni wawili tu ndiyo wanaokula mara tatu kwa sasa.
“Wanaokula mara tatu ni watoto wangu wadogo wenye umri wa miaka mitano na mitatu, wengine ni mwendo wa kula mara mbili, maana maisha yamekuwa magumu na hakuna pesa kabisa za kuendesha maisha tuliyozoea,” anaongeza.
Akieleza sababu za ugumu wa maisha, mwananchi huyo anasema – “ni viongozi wetu tu kushindwa kutumia uwezo wao na labda utashi wa kutumia nafasi zao kufanya maisha yawe mepesi.” Hakufafanua zaidi.
Mwananchi huyo anaamini kwamba ikiwa serikali itaamua kupunguza baadhi ya kodi kwa bidhaa muhimu kama mafuta, kuna uwezekano mkubwa wa bei za bidhaa, hasa chakula kushuka na kuleta unafuu kwa wananchi.
Mussa Liberatus, mtaalamu wa uchumi anayeishi na kufanya kazi zake Dodoma, anaeleza kwamba pamoja na kwamba familia kukosa milo mitatu iliyoozoeleka – siyo kipimo pekee cha maisha magumu, lakini ni kiashiria muhimu kwamba wananchi wengi wako katika mtanziko wa maisha magumu.
“Maendeleo ya kweli hayapimwi kwa kuwa na majumba makubwa wala barabara nzuri wala kuwa majengo mazuri ya taasisi za serikali na idadi kubwa ya ndege, kama watu wako hawali, basi ni useless (hakuna faida), kipimo kikubwa cha maendeleo ya kweli ni watu kula chakula cha kutosha na kwa wakati muafaka,” anasema msomi huyo.
Anaishauri serikali kuwa na mkakati wa kupunguza mlolongo wa kodi kwenye bidhaa muhimu kama mafuta ya kuendesha mitambo; ya kula; kuongeza wigo wa ajira; kulipa makandarasi kwa wakati na kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima katika kuendesha nchi.
Mbali na kuandaa dodoso, SAUTI KUBWA imefanya utafiti na kugundua mwaka huu, idadi ya vijana wanaouliza namna ya kuuza baadhi ya viungo vyao – hasa figo, katika mitandao ya kijamii (Google search, Twitter na Facebook) imeongezeka. Katika kipindi cha Septemba 2021 hadi Machi, 2022 Watanzania walioulizia njia na bei ya kuuza figo walikuwa 211.
Pia takwimu za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) zinaonyesha kupokea maombi ya wananchi 36 wakiuliza uwezekano wa kuuza figo zao na wote hawa walieleza sababu ya kuwa na uamuzi huo wa kuuza baadhi ya viungo vyao ni “ugumu wa maisha.”
Mwaka jana, kupitia majibu ya utafiti wa Taasisi ya Afrobarometer iliyoko nchi zote za Afrika, ilieleza kwamba Tanzania kwa mwaka 2020 – 2021 ilikuwa na familia 32 kati ya 100 ambazo ama hazikuwa na chakula cha kutosha au kula mara moja tu kwa siku. Utafiti huo hufanywa kwa nchi zote za Afrika na katika kipindi hicho ilibainika kuwa nchi iliyokuwa na hali mbaya Zaidi ya chakula Afrika ilikuwa Malawi ikiwa na familia 79 kati ya 100 zilizokuwa na hali mbaya ya chakula. Mauritius iliongoza kwa kuwa na familia 10 kati ya 100 mbazo zilikuwa zinakula mara moja tu kwa siku.
Tayari Rais Samia Suluhu Hassan amezungumzia ugumu wa maisha kwa wananchi na kueleza kwamba maisha huenda yakazidi kuwa magumu kwa kuwa “mabadiliko ya kupanda kwa bei ya mafuta yamesababishwa na vita ya Ukraine na Urusi, hivyo Tanzania hatutanusurika, bidhaa zote zitapanda bei, nauli zitapanda bei kila kitu kitapanda, thamani ya kila kitu itapanda juu.
Rais Samia – Machi 8, mwaka huu akiwa Zanzibar alisema amesikia kuwepo kwa minong’ono kuwa maisha yanakuwa magumu, lakini siyo kosa la serikali wala viongozi, isipokuwa madhila ambayo yako nje ya uwezo wao.