MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anasema alibaini wakala wa ndege za serikali (TGFA) ililipa Shs. 3.92bn gharama ya huduma za matengenezo makubwa ya ndege ambayo hata hivyo ndege hiyo ilikuwa haifanyi kazi, imetelekezwa tangu 2015. Yaani ‘wafilisti wenu’ walitenga fedha za umma kwenye matengenezo hewa (feki)
Wakala wa ndege za serikali Tanzania (TGFA) mwaka 2019 ilipelekwa ofisi ya Rais (utumishi na utawala bora) kutoka wizara ya ujenzi na uchukuzi, taarifa ya CAG 2019/2020 inaeleza TGFA ililipa Shs 3.92bn kutengeneza ndege ambayo haifanyi kazi, imeegeshwa tangu mwaka 2015.
Manunuzi ya ndege yapo kwa ‘wakala’ iliyohamishiwa Ikulu. hayakaguliwi. Kinakachokaguliwa ni uendeshaji wa ndege uliopo ATCL. CAG ameporwa uwezo wa kutueleza ‘tender’ na bei ya ununuzi, hawezi kukagua wakala wa ndege za serikali, atatueleza hasara ya ATCL tu ambayo ni Shs. 36bn/-
Hesabu zilizokaguliwa za ATCL na zinabainisha kuwa ATCL ilipata hasara ya kiasi cha TZS 60.2 bilioni kwa mwaka wa fedha 2019/2020 na hivyo kufanya hasara jumuifu ya ATCL tangu mwaka 2015/2016 (Accumulated losses) kufikia kiasi cha Sh152.9 bilioni. Hili shirika linaendeshwa kama wamiliki wa daladala.
Kwa mwaka wa fedha 2019/2020 uliomalizika Juni 30, 2020 uchambuzi wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ulibaini kwamba Air Tanzania Company Limited (ATCL) ilikuwa na mtaji wa TZS 246.66 bilioni.
Ukijumlisha hasara jumuifu (accumulated losses) ya ATCL hadi 2021/2022 jumla ni TZS 224.3 bilioni. Wakati huo mtaji wa ATCL ni TZS 246.66 bilioni. Deni la ATCL ni TZS 152.16 bilioni. Deni hilo linahusisha TZS 70.94 bilioni (47% ya deni lote). Deni ambalo wanadaiwa na Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA)
Kuna deni la TZS 87.25 bilioni (ambalo ni 59% ya deni lote) ambalo ni deni la kampuni ya Wallis Trading Inc. kampuni hiyo ya Wallis Trading Inc ilikodisha ndege zake kwa Air Tanzania Company Limited (ATCL). Walis Trading Inc walifungua Case No: CL-2017-000227
Kesi ilifunguliwa Royal Courts of Justice Strand, London, WC2A 2LL. 21/02/2020. The High Court of Justice, Business and Property Courts of England and Wales, Commercial Court (OBD). Mbele ya Mr. Justice Butcher. Mawakili wa Tanzania na ATCL ni Prof, Adeladrus Kilangi, Gabriel Malata na Musa Mbura.
Uamuzi ulikuwa hivi; “For those reasons, Wallis’s claim pursuant to the settlement agreement succeeds. Wallis is entitled to the sum of US$30,114,230.73 there under, together with interest as to the amount of which I will hear the parties. Had I not found that the settlement agreement replaced their obligations under the lease and guarantee, I would have found that the Defendants were liable under those agreements.”
Deni la Air Tanzania Company Limited (ATCL) limeongezeka pia kutokana na kuingia mkataba wa gharama za ukodishaji wa ndege TZS 15.46 bilioni kati yake na Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) kutokuwa na kipengele cha vihatarishi visivyotabirika.
Air Tanzania Company Limited (ATCL) walikodi ndege kutoka Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) ambazo hazikufanya kazi wakati wa COVID-19 kati ya Machi 15 na Juni 30, 2020. Kama kipengele hicho kingelikuwepo katika mkataba, Air Tanzania Company Limited (ATCL) wasingelitozwa gharama hizo.
Air Tanzania Company Limited (ATCL) iliingia gharama mara mbili ya TZS 16.97 bilioni kama gharama za matengenezo ya ndege kutokana na dosari za kimkataba kati ya Air Tanzania Company Limited (ATCL) na Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA).
Mwaka wa fedha 2019/2020 ilipanga kupata mapato ya TZS 661.64 bilioni. Hata hivyo, walifanikiwa kupata mapato ya TZS 157.60 bilioni. Hawakufika hata nusu ya malengo waliyojiwekea wenyewe. Hakuna ufanisi. Hili shirika la umma linaendeshwa kama wodi ya vichaa.
Hasara za ATCL; 2014/2015 hasara TZS 94.3 bilioni. 2015/2016 hasara TZS 109.2 bilioni. 2016/2017 hasara TZS 113.8 bilioni. 2017/2018 hasara TZS 26.6 bilioni. 2018/2019 hasara TZS 48 bilioni. 2019/2020 hasara TZS 60.24 bilioni. 2020/2021 hasara TZS 36.2 bilioni. 2021/2022 hasara TZS 35.2 bilioni.