BAADA ya makatibu wakuu wa CCM wastaafu Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana kutoa tamko kali jana dhidi ya “wakala” wa Rais John Magufuli anayetumika kusakama watu kwa kutumia vyombo vya habari, SAUTI KUBWA imepata orodha ya vigogo wa CCM wapatao 17, ambao vyanzo vya kuaminika vinadai kuwa shutuma za “wakala” huyo dhidi yao ni mkakati wa dola kuwajengea mazingira ya “kuondolewa.”
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wanaotuhumiwa na kuhusishwa na mkakati huu ni rais na viongozi waandamizi wa usalama wa taifa, ambao wanadaiwa kumtanguliza na kumlinda Cyprian Musiba, anayejiita mwanaharakati huru na mtetezi maalumu wa rais, kwa shabaha maalumu na ovu.
Mbali na Mzee Makamba na Kinana, wengine 15 ambao “wanalengwa” na mkakati huu ni Bernard Membe, Januari Makamba, Nape Nnauye, Mwigulu Nchemba, Emmanuel Nchimbi, Stephen Wassira, Mark Mwandosya, Hussein Bashe, Peter Serukamba, Prof. Mussa Assad, Edward Hosea, Ridhiwani Kikwete, Balozi Seif Iddi, Abdallah Bulembo, na Dk. Juma Abdallah Saadala.
Vyanzo vyetu vimesema mbali na viongozi hawa wa chama na serikali kwa upande wa CCM, wapo pia viongozi wa vyama vya upinzani na wabunge wao wanaotafutwa kuangamizwa kwa kuwa hawakubaliani na mfumo na mbinu za utawala wa Rais John Magufuli ambao umekuwa utawala wa manyanyaso na mateso dhidi ya raia.
Kwa nyakati mbalimbali jana na juzi, watoa taarifa hao ambao ni makada na viongozi waandamizi wa CCM wanasema chama chao “kimetekwa na genge linaloelekea kuharibu amani na usalama wa taifa,” na wanaunga mkono kimya kimya jitihada za akina Makamba kukemea uhalifu unaojengwa na mamluki wanaotumiwa kuvuruga nchi.
Juzi Makamba na Kinana walisambaza tamko lao la pamoja kwa vyombo vya habari, ambalo linahoji mamlaka zinazomtuma na kumlinda mamluki Musiba ambaye amekuwa anatumia jina la rais kutoa matamko yanayoweza kuhatarisha usalama wa nchi, na kudhalilisha watu kadhaa kwa kile ambacho wazee hao wamekiita “shabaha maalumu.”
“Tumetafakari kwa kina kabla ya kutoa taarifa hii kwa umma kuhusiana na uzushi alioutoa Cyprian Musiba dhidi yetu katika nyakati mbili tofauti. Watanzania wanajua kuwa haya anayoyasema mtu huyu kuhusu watu mbalimbali siyo ya kwake. Yeye anatumwa kutekeleza maagizo na kutumika kama kipaza sauti tu. Huyu ni mamluki anayetumika kuivuruga CCM na nchi yetu. Katika mazingira hayo hatuwezi kukaa kimya,” ilisema taarifa kwa umma iliyosainiwa na Makamba na Kinana juzi tarehe 14 Julai 2019.
Taarifa ya siri iliyoifikia SAUTI KUBWA inasema: “Nguvu ya Musiba inatoka kwa JPM (Rais Magufuli) na TISS (usalama wa taifa). Kule TISS inasimamiwa na Nyaulingo (naibu mkurugenzi wa mkuu wa TISS) na Modestus Kipilimba (Mkurugenzi Mkuu wa TISS). Gazeti la Tanzanite ni la Usalama wa Taifa. Uchapishaji wa gazeti hilo unafanyika Mbweni kwenye chuo cha usalama wa taifa – Malindi Printing Press – mali ya serikali. Musiba analipwa kila mwezi shilingi milioni tatu. Anapewa matangazo na analipwa, amepewa gari, na analindwa na walinzi wawili. Taarifa zote anazoandika anapewa na idara ya usalama na JPM mwenyewe. Lengo la yote haya ni kutaka kuwachafua, kuwadhalilisha, na kuwazushia kashfa mbalimbali viongozi wastaafu wa chama na serikali ili itakapofika mwakani watu hao wasiwepo, ama wawe magerezani au wawe wamepotezwa.”
Habari zinasema pia kuwa kwa maagizo kutoka juu, Musiba amechomekwa kinyemelea kwenye idara ya usalama na katika kitengo kinaitwa “Subversion” au “Uzandiki.” Wasomi wa masuala haya ndani ya kitengo wamekuwa wanalalamika chini chini inakuwaje mtu asiye na elimu kabisa na asiyekuwa mtumishi wa idara anachomekwa na kupewa majukumu nyeti huku wao wakiwekwa pembeni.
Taarifa hii inakamilisha na kufafanua tamko la Makamba na Kinana ambalo halikutaja kwa jina au cheo mtu anayemtuma Musiba kusakama watu. Msisitizo wao upo katika maneno yafuatayo:
“Tuliamini kabisa kwamba pale anapojitokeza mtu hadharani na kuwadhalilisha viongozi waandamizi wastaafu, na huku mtu huyo akijinasibisha na serikali pamoja na rais mwenyewe ambaye ni mwenyekiti wa CCM, basi hatua zitachukuliwa na taarifa kutolewa kwa umma. Kwa bahati mbaya, viongozi wetu hawakuchukua hatua yoyote kuhusu jambo hili. Na zaidi, mtu huyo ameendelea kuwadhalilisha na kuwavunjia heshima viongozi wastaafu na watu wengine katika jamii.
“Mtu huyu amefikia hata hatua ya kuthubutu kuwatuhumu viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa wanamhujumu rais. Amefanya hivyo bila kujali athari za kauli zake kwa Muungano wetu. …Ameachwa akitamba, jambo linaloashiria kwamba anakingiwa kifua. Hata anapotumia lugha za vitisho na kuhatarisha usalama wa raia hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yake.
“…Kwa ushahidi wa kimazingira, mtu huyu anatumwa na kutumiwa na watu wenye uwezo wa kumlinda na kumkingia kifua bila kuhojiwa na taasisi yoyote wala mtu yeyote. Zipo ishara kwamba watu hawa wanaomkingia kifua wana mamlaka, baraka na kinga ambazo wamepewa ili kutekeleza majukumu maalumu, kwa watu maalumu na kwa malengo maovu.”
Tamko la wazee hawa limezua gumzo kitaifa na kimataifa juu ya siasa za, na hatima ya, CCM na Magufuli katika uongozi ambao umejitanabaisha na ubabe, vitisho na mauaji ya raia hasa wakosoaji wake.
Tamko hilo ni hatua mpya katika harakati za Watanzania kupambana na udikteta ambao umeikabili Tanzania na umekuwa unaota mizizi kila wakati ndani ya miaka mitatu mfululizo tangu 2016. Wazee hawa wameandika waraka maalumu kwa Baraza la Wazee wa CCM, “kuwasihi watumie busara zao katika kushughulikia jambo hili…”
Mmoja wa vyanzo vyetu vya habari ameliambia SAUTI KUBWA: “Makamba na Kinana sasa wameyasema ya moyoni. Tusubiri Baraza la Wazee kama kweli wana ubavu wa kumkemea Musiba, JPM na TISS. Walimalize hili halafu wapelekewe waraka mwingine unaohusu kupotea, kutekwa, na kuuawa kwa watu nchini kunakofanywa na idara ya usalama wa taifa.”