Mpwa wa Magufuli adai anaponda raha kwa Samia kuliko enzi za utawala wa mjomba wake

FURAHA Dominic, mpwa wa hayati John Pombe Magufuli (aliyekuwa rais wa awamu ya tano wa Tanzania) amesema kwa sasa anaishi kwa raha zaidi kuliko kipindi cha uongozi wa mjomba wake.  

Pia amesema hawezi kuwa miongoni mwa watu wanaojiita “Timu Magufuli” – kwa kuwa waliomo kwenye kundi hilo wanajulikana na ndiyo wanaendeleza mambo ya kiongozi huo wa Tanzania aliyefariki mapema mwaka jana, 2021.  

 Akizungumza jana, Furaha ambaye aliongoza kwa kura za maoni wakati wa mchakato wa kupata mgombea ubunge Jimbo la Kawe, Dar es Salaam, kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na baadaye akaenguliwa na vikao vya juu vya chama hicho, ameuambia umma kuwa amani na furaha yake sasa ni kubwa kwa kuwa “hakuna wa kumtupia mawe kwa kumhusisha na familia ya Rais Magufuli.”  

Furaha anasema wakati wa uongozi wa Rais Magufuli, haikuwa rahisi kujilinda dhidi ya uonevu, kwani kila aliyemchokoza “alimuacha tu” ili kuepusha maneno kwamba anaringia uongozi wa mjomba wake, endapo angeamua kujibu mapigo.  

“Sasa hivi siogopi tena kuonekana nabebwa na mjomba, mtu akinichokoza, naweza kujilinda na kuchukua hatua nazoona zinafaa,” amesema Furaha.  

Mbali na furaha yake kwa sasa, mpwa huyo wa Rais Magufuli amekanusha hisia kwamba ni miongoni mwa watu wanaounda “Timu Magufuli” na kuwataja baadhi yao kuwa ni Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, Mkuu wa Majesh ya Ulinzi na Usalama, Venance Mabeyo na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro.  

“Hawa ndiyo Timu Magufuli, mimi simo na wala watu wasiniweke humo, hawa ni viongozi ambao alikuwa nao Rais Magufuli na sasa wamebaki wakiendeleza waliyoanza kuyafanya wakati wa awamu iliyopita,” ameongeza mwanasiasa huyo.  

Akizungumzia kadhia ya kufukuzwa kazi baada ya kifo cha Rais Magufuli, Furaha ambaye ni mwajiriwa wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali alikiri kupokea barua ya kuondoshwa kazini kwa kile alichokieleza – “kupewa kosa la kutoonekana kazini kwa siku tano,” lakini kwa sasa amerejeshwa baada ya kugundulika upungufu katika kutolewa kwa adhabu hiyo. Alipokea barua ya kufukuzwa kazi mwishoni mwa Machi, 2021 na sasa amerejeshwa.  

Amemtaka mbunge wa sasa wa Jimbo la Kawe, Askofu Josephat Gwajima, “kukaa mkao wa utayari kuondoka” kwa kuwa anafanya mazoezi ya kuchukua jimbo.  

Like