MIAKA 60 YA UHURU: SAMIA FUFUA RAMANI YA MAENDELEO YA NYERERE

AWAMU ya kwanza ya uongozi wa nchi yetu, chini ya Mwl. Julius Nyerere, ilichora ramani ya maendeleo kwa kuzingatia siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Kupitia sera hiyo, mamia ya viwanda yalijengwa ili kusindika mazao karibu yote ya kilimo na mifugo. Kwa mfano, viwanda vya nguo vya Kilitex, Mwatex, Urafiki, Mutex viwanda vya korosho, kahawa, magunia, viatu, maziwa, nyama, n.k.

Vile vile, vilijengwa vyuo vya utafiti vya kilimo na mifugo, zilianzishwa ranchi za taifa, yalianzishwa mashirika ya umma ya kuzalisha bidhaa mbalimbali ya misitu, kilimo, uvuvi, taasisi za kiufundi kama CAMARTEC, TEMDO n.k.

Vyuo vya kuzalisha wataalamu ngazi ya kati kama; MZUMBE, UHASIBU (Dar-es-salaam na Arusha), DAR TECHINICAL, ARUSHA TECHINICAL, VYUO VYA UTABIBU, MIFUGO n.k

Elimu yetu ilikuwa bora, kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na ya chuo kikuu.

Kufuatia kumalizika kwa vita ya kumng’oa nduli Idi Amin wa Uganda 1979, nchi yetu ilikabiliwa na uhaba wa fedha za kigeni, hali iliyopunguza uwezo wetu wa kuagiza vipuli muhimu na malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu na baadhi ya mashirika ya umma.

Hali hii ilizipa fursa taasisi za fedha za kimataifa (IMF na World Bank) na  nchi za magharibi, zikiongozwa na Marekani, kuiwekea nchi yetu masharti magumu ya kukopa, kwa lengo la kudhoofisha mafanikio yaliyotokana na sera ya Ujamaa na Kujitegemea.

Baadhi ya masharti hayo yalitutaka  kubinafsisha viwanda na mashirika yetu ya umma.

Baadhi ya mashirika na taasisi zilizobinafsishwa mwanzoni ni Tanzania Cigarette Company, Tanzania Breweries na Benki ya CRDB. Ubinafsishaji uliofanyika kwa mashirika haya, kimsingi, ulichukua sura ya serikali kuuza sehemu ya hisa zake.

Kwa bahati mbaya, awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa ililegeza msimamo wa awali na kuanza “kuuza” kiholela mashirika na taasisi za umma kiasi kwamba hata Mwl. Nyerere alikosoa waziwazi ubinafsishaji wa mashirika ambayo yalikuwa yanazalisha faida, kama NBC.

Kwa  bahati mbaya, Mwl. Julius Nyerere aliaga dunia Oktoba 1999, na hivyo nchi ikakosa baba au mzee mwenye kauli ya mwisho, mtetezi wa maslahi ya nchi katika kutekeleza sera ya ubinafsishaji.

Kufuatia utekelezaji wa sera  hizo za taasisi za kimataifa na kwa kukosa umakini, ramani ya maendeleo ya nchi yetu iliparaganyika. Kama wasemavyo Waingereza, “the rest is history.”

TUFANYE NINI?

Serikali ya awamu ya sita ifanye juhudi za makusudi na za haraka kufufua “ramani ya maendeleo” iliyoandaliwa na awamu ya kwanza kwenye maeneo yote.

Kwanza, lazima serikali kuu itafute fedha na kusimamia upimaji wa ardhi yote ya nchi yetu ili kutenga maeneo ya shule, vyuo, michezo, kilimo, ufugaji, uhifadhi n.k.

Pili, ziandaliwe hati kwa ajili ya kilimo na ufugaji ili wawekezaji wanaotaka kuwekeza kwenye kilimo/ufugaji wa biashara wapate maeneo hayo bila ucheleweshaji au kusababisha migogoro.

Tatu, kila wizara ishirikiane na wadau wa sekta husika wakiwemo wastaafu, kubaini ramani ya wizara hiyo na kutoa mapendekezo ya kuboresha ramani hiyo kwa kuzingatia mahitaji ya sasa. Huwezi kuboresha kitu usichokijua.

Nne, kuondokana na ufujaji wa kodi za wananchi. Kipindi cha awamu ya kwanza, magari ya kifahari yalikuwepo lakini Mwl. Julius Nyerere aliegesha Rolls Royce aliyorithi kwa Waziri Mkuu wa kikoloni, akatumia Land Rover 109 akiwa mikoani ijapokuwa barabara hazikuwa za lami.

Leo hii, hata wakopeshaji wetu kutoka Ulaya (EU), Marekani na kwingineko,  wanashangaa jinsi watumishi wengi wa umma wanavyotumia magari ya kifahari kwa kodi ya wananchi.

Tano, ubinafsishaji. Yapo mashirika na taasisi za umma ambazo angalau asilimia 30  ya hisa zake zingeuzwa kwa wananchi ili kuongeza ufanisi na tija ya mashirika hayo. Mashirika kama TANESCO, TBA, National Housing Corporation, AICC n.k.

Sita, haitoshi balozi zetu za nje ya nchi kufanya kazi moja ya kuvutia wawekezaji. Ingefaa mabalozi wetu waandae taarifa rasmi za kuonyesha:-

  1. Bidhaa gani za kilimo, mifugo n.k tunazoweza, kuuza kwenye nchi walipo.
  2. Mambo gani tunafaa kuiga katika maeneo mbalimbali ya maendeleo kama utawala bora, elimu, afya, michezo, ukusanyaji wa kodi, ajira n.k.
  1. Maeneo ambayo vijana wetu wanaweza kwenda kupata elimu, ujuzi na  uzoefu wa kufanya mambo kisasa zaidi.

Saba, kufufua moyo wa ushirika au kufanya kazi pamoja. Watu wetu wametafsiri vibaya sera ya kujiajiri. Kwa mfano, fundi seremala 10 wakijiunga pamoja, watahitaji randa 5, misumeno 5, nyundo 5 n.k.

Lakini iwapo kila mmoja atafanya kazi peke yake, kila mmoja atahitaji vitendea kazi vya kwake ambavyo ni jumla ya randa 10, misumeno 10, nyundo10 n.k.

Hali ni hiyohiyo kwa biashara karibu zote hata za kitaalamu; wamiliki 10 wa secretarial bureau  watahitaji photocopier 10, printers 10 n.k. lakini wangeunda umoja bila shaka wangehitaji mashine tano tano tu.

Huwa najiuliza, wamiliki wa vituo vya petroli 10 hawawezi kumiliki kiwanda kikubwa?

MUTEX

Kwa hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan na timu yake warejeshe hamasa ya wananchi kuzalisha fikra mbadala au mawazo ya kuendeleza jamii na nchi kwa ujumla.

Leo hii, tofauti na ilivyokuwa miaka ya 60, tunao Watanzania wengi wenye elimu, ujuzi, uzoefu na maarifa ya namna ya kuboresha kila nyanja ya maisha ya Mtanzania.

Serikali ifungue haraka wigo wa  kuzalisha, kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi hususan wadau,  wakiwemo watalamu na wastaafu katika sekta zote za maisha ya Mtanzania.

Hebu fikiria utajiri wa rasilimali watu tulionao wa wastaafu kama walimu, maDED,DAS, makatibu wakuu, majaji, wahandisi, madaktari, manesi, maofisa kilimo, maofisa mifugo, maofisa maji, maofisa ardhi, maofisa biashara n.k

Iwapo kila wizara ingepewa jukumu la kuendesha makongamano nchi nzima ya kupokea mawazo/mapendekezo ya wastaafu hawa na wadau kwa ujumla, katika kila sekta, hakika tungeweza kuchora ramani ya maendeleo ambayo ingetuwezesha kufanya “leap forward” ya maendeleo yetu.

Mwl. Nyerere alisistiza wakati wote wa uhai wake kwamba ili tuendelee tunahitaji kufanya mambo makuu mawili.

Kwanza, kuzalisha mawazo yetu wenyewe ya njia bora za kujiletea maendeleo na si kutegemea mawazo ya mataifa yaliyoendelea.

Pili, kuimarisha umoja ndani ya nchi yetu na ndani ya Bara la Afrika katika kuzalisha fikra, kuandaa mipango ya maendeleo na kuitekeleza mipango hiyo.

Badala yake, serikali yetu, hususan katika awamu ya tatu, nne, tano, na sasa ya sita, inaimba wimbo wa sera ya chama tawala ambayo Rais Mkapa (hayati) alishasema kuwa “haitekelezeki.”

Sera ya chama tawala kamwe haiwezi kuwa mbadala wa fikra na mipango  shirikishi.

MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI AFRIKA.

Like