MGOGORO wa kifamilia umezuka baada ya kifo cha aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan, Dk. Pius Ng’wandu, kuhusu mahali yatakapofanyika mazishi yake.
Dk. Ng’wandu aliyewahi kuwa waziri katika serikali zilizopita akihudumu wizara mbalimbali, alifariki asubuhi kuamkia leo, Desemba 19, 2020 mjini Bariadi, Simiyu baada ya kuugua ghafla. Alifariki muda mfupi alipofikiswa Hospitali ya Mkoa wa Simiyu, Somanda, iliyopo mjini Bariadi.
Taarifa zilizotufikia SAUTI KUBWA zinaeleza kuwa kumezuka mgogoro kati ya watoto wa marehemu na mjane wake, Mary, aliyefunga ndoa naye mwezi Oktoba, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Mke wa kwanza wa Dk. Ng’wandu, Lucy, alifariki Aprili 25, miaka sita iliyopita baada ya kuugua kwa shinikizo la damu. Alizikwa Makabe, Dar es Salaam. Aliacha watoto watano; wasichana watatu na wanaume wawili.
Taarifa zinaeleza kuwa watoto wa marehemu, Dk. Ng’wandu wanataka baba yao azikwe pembeni ya kaburi la mkewe wa kwanza, Lucy, huku mjane wake, akipendekeza azikwe Sumve, eneo ambalo kuna ukoo wa marehemu, na kwamba Ng’wandu alichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya eneo hilo alipokuwa mbunge kwa miaka 15.
SAUTI KUBWA imeelezwa kwamba mke mpya amewaeleza ndugu wa marehemu kwamba mumewe, pamoja na kuwa hakuandika azikwe wapi, lakini aliwahi kueleza kwamba atakapofariki, azikwe jirani na hapo.
Taarifa zilizotufikia jioni leo, zinaeleza kuwa watoto wawili wa marehemu, Dolres na Alex, tayari wako safarini kwenda Bariadi ili kushawishi famili ili kufanikisha “mapendekezo” ya baba yao kuzikwa pembeni mwa kaburi la mkewe wa kwanza, Makabe, Dar es Salaam.
“Mtoto mmoja amefika hapa Bariadi, mwingine kaka yao amefika Mwanza jioni hii na safari ya kuja hapa imeanza, kazi kubwa ni kujadili mahali pa kumpumzisha mzee wetu,” ameeleza ndugu wa Dk. Ng’wandu aliyeko Bariadi, hakupenda kutajwa jina.
Mvutano huo wa maziko ya Dk. Ng’wandu, umeelezwa na wakili John Masele kwamba kisheria, mke wa marehemu anatambuliwa na kupewa nguvu zaidi na sheria juu ya uamuzi wa chochote cha marehemu.
“Ikiwa marehemu hakuandika wosia, na yuko na mkewe, sheria inambeba zaidi mkewe halali, sasa kwa hili la Dk. Ng’wandu kama kweli kuna mgogoro, mkewe anaweza kuamua azikwe wapi, lakini majadiliano na watoto yanaweza kuleta muafaka na kuepusha mvutano,” amesema wakili huyo aliyebobea masuala ya familia.
Kuna taarifa kuwa katika miezi michache iliyopita, watoto hao walivutana na baba yao wakipinga wazo mpango wake wa kuoa mke mwingine. Alipowashirikisha wazo hilo, walimkatalia katakata kw amadai kuwa umri wake ni mkubwa mno kuwa na mke mpya.
Dk. Ng’wandu alizaliwa mwaka 1944 huko Sumve. Mjane, ambaye ndiye alikuwa mke wake mpya aliyemuoa Oktoba mwaka huu, ana miaka 33.
Baada ya watoto hao kumgomea kuhusu mpango wake huo, Dk. Ng’wandu aliamua kufunga ndoa isiyo na mbwembwe akisindikizwa na watu waapatao sita. Picha na ndoa hiyo zilisambazwa mitandaoni na kuibua gumzo katika jamii.
SAUTI KUBWA imeambiwa kuwa hata watoto hao wa Dk. Ng’wandu walipata taarifa za ndoa hiyo baada ya picha hizo kusambazwa mitandaoni.
Taarifa zinasema kuwa kila walipompigia simu kumuulizia habari hizo, akiwa safarini mikoani na mkewe mpya, baba yao aliwambia: “Msiwe na wasiwasi, niko salama. Nitawajulisha nitakaporudi Dar es Salaam.”
Tangu Oktoba, Dk. Ng’wandu na mkewe mpya wamekuwa ziarani Arusha, Tanga na Morogoro. Walikuwa wakielekea Sumve ambako Dk. Ng’wandu amewahi kuwa mbunge kwa miaka kadhaa, shabaha ikiwa ni kumtambulisha mkewe kwa wana ukoo.
Dk. Ng’wandu amewahi kuongoza wizara za elimu ya juu, maji, ardhi, nyumba na kwamba baada ya kustaafu utumishi wa umma, alisoma sheria Chuo Kuu Huria cha Tanzania na baadaye kuidhinishwa kuwa wakili waliomaliza kwa ufaulu, Shule Kuu ya Sheria.