MAGOLI matatu ya Lionel Messi yamewezesha Barcelona kubeba kombe la Ligi Kuu ya Hispania kwa mara ya tatu ndani ya miaka minne mfululizo.
Ikicheza ugenini, Barcelona ilifunga magoli manne dhidi ya mawili ya Deportivo La Coruna. Messi alifunga matatu, na Coutinho, ambaye alijiunga na vinara hao wa La Liga akitokea Liverpool ya Uingereza katika dirisha dogo la uhamisho wa wachezaji Januari 2018, alifunga goli moja.
Hili ni kombe la 25 kwa Barcelona, ambayo pia kwa ushindi huu imebeba makombe mawili katika msimu huu wa 2017/2018. Wiki iliyopita ilitwaa pia Kombe la Mfalme baada ya kuicharaza Sevilla.
Ushindi huu pia ulikuwa na umuhimu wa pekee kwa Andres Iniesta, nahodha wa Barcelona ambaye kwake ilikuwa mechi yake ya mwisho kwa klabu hiyo.
Aliingia uwanjani katika dakika za mwisho za kipindi cha pili.
Hata kabla ya mechi ya leo, Iniesta aliwaambia waandishi wa habari: “Shabaha yangu ni kuongeza kombe jingine la ligi.” Amefaulu.
Kwa Iniesta, huu ni ubingwa wa tisa wa La Liga akiwa na Barca kwa miaka 13.
Barcelona imekuwa timu pekee katika La Liga ambayo imepata ubingwa bila kushindwa mechi yoyote katika msimu mmoja.
Mbali na Barcelona kufunga magoli 4 dhidi ya 2 ya Deportivo, walitawala mchezo kwa asilimia 63 za umiliki wa mpira.
Kwa kipigo hiki, Deportivo wameshuka daraja kutoka La Liga hadi La Liga 2 (daraja la pili).
Katika miaka 10 Barca wamebeba makombe saba ya La Liga, huku washindani wao wakuu, Real Madrid wakiambulia mawili tu. Wamebeba kombe la msimu huu wakiwa bado na mechi nne mbele.
Timu bora kabisa Hispania
Takwimu zinaonyesha kuwa Barca ndiyo timu iliyotwaa makombe mengi kuliko zote katika Hispania. Katika makombe ya ndani, Barca inayo 72. Klabu inayofuata kwa mbali ni Real Madrid yenye makombe 64.
Katika hayo, Barca imebeba kombe la La Liga mara 25, Copa de Rey mara 30, Supercopa mara 12, Copa Eva Duarte mara tatu (3), na Copa de la Liga mara mbili (2).
Madrid, katika makombe yake 64, imetwaa kombe la La Liga mara 33, Copa de Rey mara 19, Supercopa mara 10, Copa Eva Duarte mara moja (1), na Copa de la Liga mara moja (1).
Hata katika jumla ya makombe yote, kitaifa na kimataifa, Barcelona imetwaa 92, Madrid 89.