Na Venance Stephen, Dar es Salaam
MGOMBEA Urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Bernard Membe, ameibuka na kutangaza mbele ya waandishi wa habari kwamba ataendelea kuwa mgombea, licha ya viongozi wake wakuu wa chama hicho kutangaza kuwa wanamuunga mkono Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Membe, ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa, alirejea kauli aliyowahi kuitoa wakati fulani kwamba ana imani ya dhati kuwa pamoja na kuwa nje ya uwanja wa kampeni ataibuka mshindi na kuushangaza umma.
“Nataka kufunga bao dakika ya 89 kutoka benchi. Watanzania mkae chonjo. Tumefanya kazi kubwa huku chini, sasa tunakuja juu kupata bao la ushindi dakika ya 89 na dakika za nyongeza,” alisema.
Hata hivyo, kauli yake hii haijulikani inahusisha akina nani wakati chama chake mwenyewe, ambacho ndicho kilichopaswa kufanya kazi hizo anazosema, kimeshangaza kumuunga mkono Lissu. Wakati Membe akisema hayo kwa waandishi wa habari, mwenyekiti wa chama chake, Seif Sharif Hamad, alikuwa jukwaa moja na Lissu katika mkoa wa Kilimanjaro, akimnadi na kumwombea kura.
Membe, mwanadiplomasia ambaye kifamilia yuko karibu na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete, ameibuka baada ya kutoweka muda mrefu ikiwa ni siku mbili tu tangu swahiba wake huyo ajitokeze hadharani akimnadi Rais John Magufuli anayetetea kiti alichokikalia kwa miaka mitano.
Kuibuka kwa Membe mbele ya wanahabari siku chache tu baada ya Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na, kabla yake, Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, kutangaza kumuunga mkono Lissu, kulionekana kuwatatiza wanahabari waliohudhuria mkutano wake huo wa leo Jumatatu Oktoba 19, 2020.
Akionekana dhahiri kuwa mtu aliyekuwa akijaribu kukwepa mkono wa sheria na kanuni za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya ushirikiano wa vyama, Membe alisema hatua ya viongozi wake wawili si jambo linaloweza kumzuia yeye kuendelea na harakati zake, na hapo hapo akasema tayari alikuwa ameshawasiliana na wenzake hao kabla ya mkutano wake na waandishi wa habari.
Tayari hatua hiyo ya Membe kujitokeza imeibua hisia tofauti miongoni mwa wafuatiliaji wa siasa za Tanzania, huku mashabiki wa CCM na wale wa upinzani wakiitafsiri kuwa yenye lengo la kugawa kura za Lissu ambaye kwa mujibu wa Zitto na Maalim Seif ndiye mgombea wanayeamini ana uwezo mkubwa wa kumwangusha Magufuli katika Uchaguzi Mkuu unaofanyika Jumatano ya wiki ijayo.
Ingawa hatua hiyo inaonekana kuwashitua baadhi ya watu, baadhi ya wachambuzi na wadadisi wa mambo wamesema Membe anajaribu kukijengea ACT-Wazalendo mazingira ya kuendelea kustawi mbele ya safari.
Fikra hizi kwa kiwango kikubwa zinachagizwa na ukweli kwamba, japo Membe anaonekana kuwa mgeni katika chama hicho, historia yake ya kufungamana na Zitto katika ACT-Wazalendo ilianza hata kabla chama hicho hakijaanzishwa.
Taarifa zinaonyesha kwamba Membe, wakati akiwa waziri katika serikali ya Kikwete alishiriki kikamilifu kuwasaidia Zitto na waasisi wenzake wa ACT -Wazalendo wakati chama hicho kilipoanzishwa mwaka 2014, mwaka mmoja tu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.
Wadadisi wa mambo wanaeleza kwamba, hatua ya Membe wakati huo ambaye alikuwa akipewa nafasi kubwa kwamba ndiye angeteuliwa na CCM kugombea urais mwaka 2015, ililenga kuidhoofisha Chadema ambayo imekuwa ndiyo chama kikuu cha upinzani. ACT-Wazalendo iliasisiwa na watu waliohama kutoka Chadema.
Ushirika huo wa faragha wa Membe na ACT-Wazalendo ndiyo unaotajwa pia kuwa sababu ya msingi iliyowafanya viongozi wa chama hicho kipya wakati huo kukataa kujiunga katika umoja wa vyama vya upinzani wa wakati huo uliokuwa ukijulikana kwa jina la UKAWA uliomuunga mkono Edward Lowassa, hasimu mkubwa wa Membe kisiasa nyakati hizo, kugombea urais.
Lowassa, ambaye alihama kutoka CCM na kujiunga na Chadema mwaka 2015, alipitishwa na chama hicho kuwa mgombea urais aliyekuwa akipigiwa chapuo na vyama vya CUF, NCCR Mageuzi na NLD.
Inadaiwa pia kwamba ushawishi wa chini kwa chini wa Membe, kupitia kwa watu wa karibu na mwanasiasa mwingine maarufu wa upinzani enzi hizo, Dk Wilbroad Slaa, ulichangia Dk. Slaa kujiondoa Chadema akipinga uteuzi wa Lowassa kuwa mgombea urais, saa chache baada ya yeye kuridhia uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho ambacho alikuwa Katibu Mkuu wake.
Wachambuzi wa siasa wanaendelea kufuatilia hatima ya “ukaidi” huu wa Membe dhidi ya uamuzi wachama chake kumuunga mkono Lissu. Wengine wanadai ni mkakati wa kisiasa usio na madhara kwa Lissu wala kwaMembe mwenyewe.