MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema chama hicho kikiingia madarakani kitaboresha maisha na maslahi ya watumishi wa umma, wakiwemo wa Jeshi la Polisi, kwani wana kipato duni na maisha magumu.
Akihutubia wananchi wa Kayenze Mwanza, Mbowe amesema katika ziara yake ya mikutano ya hadhara kwenye mikoa ya kanda ya ziwa, amebaini kuwa watumishi wa umma hususan wa Jeshi la Polisi wana changamoto nyingi ikiwemo kukosa nyumba bora, hali inayoathiri weledi na ufanisi wao.
“Tangu uhuru nchi hii imeongozwa na CCM lakini imeshindwa kuondoa umaskini mwingi unaotesa wananchi. Nikiwa Geita nilitaarifiwa kwamba kuna tatizo kubwa sana la watumishi wa umma kukosa nyumba bora, wakiwemo Polisi, na uhaba wa vitendea kazi ikiwemo magari ya kufanyia doria,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Kama Mwenyekiti wa Chama hiki, ninatambua wajibu wa vyombo vya usalama katika kulinda usalama wa raia na mali zao. Kwa hiyo, Chadema, itathamini mchango wao kwa taifa hili kwa kuhakikisha tunaboresha maslahi yao, maisha yao na kuwatengenezea mazingira mazuri yatakayoongeza ufanisi wa kazi yao,” alisema Mbowe.
Hata hivyo, alizungumzia uchaguzi ujao wa serikali
za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Mbowe alivisihi vyombo vya usalama nchini kote kuacha kabisa kujihusisha na njama na shughuli za kuvunja sheria na kanuni za uchaguzi, ikiwemo kuzichezea kura, kwa lengo la kukibeba chama chochote kile.
“Bila msaada wa Jeshi la Polisi, CCM hawa ni walaini kuliko maini. Polisi watuache tushindane na CCM kwa uhuru na haki. Wasiipendelee CCM wala wasiipendelee Chadema. Nawataka wasijiingize kabisa katika dhambi ya kuisaidia CCM kuiba kura,” alisema.
Aidha, Mbowe alitangaza msamaha kwa askari polisi wote waliotumika vibaya kuiba kura na kuvuruga uchaguzi uliopita. Msamaha huo pia uliwahusu walimu aliodai kuwa baadhi yao walitumika vibaya kuibeba CCM wakati wakisimamia uchaguzi uliopita.
“Natangaza msamaha kwa askari polisi wote na kwa walimu wote waliotumika vibaya kuisaidia CCM kuiba kura katika uchaguzi uliopita. Tuwasemehe ili kwa pamoja tuweze kuanza upya na kujenga Taifa linalojali haki, uhuru, demokrasia na maendeleo ya kweli ya watu.
“Madhara ya wizi wa kura yanaumiza pia polisi wenyewe pamoja na familia zao na vizazi vyao. Kwasababu ya viongozi wabovu wanaopatikana kwa wizi wa kura leo tuna serikali isiyojali maisha na maslahi bora ya watumishi wa umma, licha ya mchango mkubwa wanaoutoa katika nchi hii.
“Ninawahakikishia kwamba Chadema ikiongoza nchi hii, moja ya vitu vya mwanzo kabisa tutakavyofanya ni kuboresha maisha na maslahi ya watumishi wote wa umma, wakiwemo Polisi na waalimu.”
Vile vile, aliwaomba polisi kuungana na wananchi katika kupinga mkataba tata wa kuendeleza bandari na maeneo mahsusi ya kiuchumi ulioingiwa na serikali ya Tanzania na Dubai, kwani hauna maslahi kwa Taifa.