Mbowe atema cheche Ukerewe

FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ameichambua hali mbaya ya umaskini unaowasibu takribani watu takribani 400,000 wa visiwa 38 vya wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, huku akiwataka wananchi wa visiwa hivyo kuachana kabisa na utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akihutubia maelfu ya wananchi wa Irugwa, Ukara, Kakukuru, Muriti na Nansio jana, Mbowe alisema Ukerewe inakabiliwa na umaskini wa kila aina licha ya kuwa katikati ya ziwa Victoria lenye utajiri mwingi wa raslimali za maendeleo.

Kwanza, alizungumzia jinsi serikali ya CCM na shirika la umeme (TANESCO) kwa ilivyoshindwa kupeleka umeme Ukerewe na kuviacha visiwa hivyo vikitumia umeme ghali unaosambazwa na kampuni binafsi ya umeme.

“Naishukuru sana kampuni hii vinginevyo msingekuwa na umeme kabisa. Hata hivyo, umeme mnaotumia ni ghali sana. Nimeelezwa kuwa mnauziwa unit moja kwa shilingi 2,000 wakati umeme wa TANESCO unit moja ni takribani shilingi 357.

:Kuishi visiwani haipaswi kuwa adhabu hata mteswe kiasi hicho. Tujiandae upya kuiondoa CCM madarakani,” alisema Mbowe.

Pili, alisema wilaya ya Ukerewe inayovua samaki na inayotegemea samaki kwa uchumi wake ilipaswa kuwa na angalau kiwanda kimoja cha samaki, lakini ni jambo la kusikitisha kuwa miaka 62 ya uhuru serikali za CCM hazijaona umuhimu wa kufanya hivyo.

Mbali na kukosa kiwanda, sekta ya uvuvi inakabiliwa na changamoto ya tozo nyingi ambapo kwa ujumla kilo moja ya samaki inatozwa si chini ya shilingi 500 kama tozo, sawa na shilingi 500,000 kwa tani moja kwa mwezi.

Kwa wastani mvuvi anaweza kupata tani 3 za samaki na kwa hiyo analazimika kulipa 1,500,000 ya tozo kwa mwezi, sawa na 18,000,000 ya tozo kwa mwaka. Hiyo ni mbali ya kulipia leseni na kodi ya mapato ya serikali.

“Kodi na tozo nyingi zinauwa mitaji ya uvuvi na kuwafilisi kabisa wavuvi. Kuendelea kuongozwa na watu waliochoka kufikiri kwaajili ya kusaidia wananchi ni hatari sana,” alifafanua Mbowe.

Tatu, alizungumzia baa la njaa Ukerewe. Tarizo ni uzalishaji duni wa mazao ya chakula Ukerewe, unaodaiwa kusababishwa na kufifia kwa afya ya udongo, kukosekana kwa mbolea, mbegu bora na kukosekana miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji. Matokeo yake mazao kama mahindi, viazi na mihogo yaliyokuwa yakitegemewa kwa chakula sasa hayatoi mavuno yanapolimwa Ukerewe na wananchi wanaingia gharama kubwa kununua chakula nje ya visiwa hivyo.

“Mna ziwa lakini serikali ya CCM imeshindwa kuchukua hatua za kidiplomasia na za kiuwekezaji za kuwezesha ziwa hili kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji. Hamna skimu yoyote ya umwagiliaji, mnateseka kwa njaa kwasababu mnaongozwa na watu wanaofikiria kuyatumia madaraka kujineemesha wao na familia zao tu,” alisisitiza Mbowe.

Nne, alizungumzia shida kubwa ya maji safi na salama katikati ya ziwa Victoria ambalo ni ziwa la pili duniani kwa kuwa na maji halisi.

“Zaidi ya 60% ya watu wa Ukerewe hamna maji safi na salama ya kunywa. Hatupaswi kulalamika. Tunapaswa kuchukua hatua za kuondokana na CCM,” alieleza Mwanasiasa huyo.

Tano, akizungumzia elimu, aliishutumu serikali ya CCM kwa kutoa elimu duni isiyowezesha vijana wa nchi hii kushindana kwenye soko la ajira ambapo alieleza kuwa elimu inayotolewa nchini haiwajengei watoto wa kitanzania ujuzi au stadi za kazi za kuwawezesha kushindana vema kwenye soko la ajira.

Takribani visiwa 30 kati ya 38 vya wilaya hiyo havina huduma ya elimu kabisa huku kwa maeneo yenye shule kukiwa na uhaba mkubwa wa walimu, hali inayosababisha wazazi kuingia gharama kubwa ya kutakiwa kutoa michango ya kugharamia walimu wa kujitolea. Mbali na hilo kuna michango pia ya chakula, madawati na mitihani hali inayofanya ile dhana ya elimu ya bure isionekane tena.

Tano alizungumzia afya hususan changamoto kubwa ya kukosa madawa.

Aidha, Ukerewe ina uhaba mkubwa wa zahanati na vituo vya afya, kwani ina zahanati kwenye vijiji 28 tu kati ya vijiji 76, na vituo vya afya vya hadhi ya kata 4 kati ya kata 25 zinazounda jimbo hilo.

Kwa ujumla, Mbowe alilisitiza kuwa umaskini wa watu wa Ukerewe ndiyo umaskini wa nchi nzima na kwamba namna pekee ya kuikomboa wilaya hiyo ni kuiondoa CCM madarakani.

Mwenyekiti huyo wa Chadema anaendelea na mikutano ya hadhara ya kuimarisha Chama hicho kwenye mikoa ya kanda ziwa

Like