Mauaji ya raia mikononi mwa Polisi wa Magufuli yazidi kuibuliwa

Former Regional Police Commander for Dodoma Gilles Muroto

UTATA mkubwa umegubika kifo cha mkazi wa Jiji la Dodoma, Josephat Hans, ambaye anadaiwa kutoweka – kwa miaka miwili sasa – akiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi ambalo lilimkamata kwa tuhuma za wizi wa kompyuta mpakato (laptop).

Josephat aliyekuwa akifanya kazi ya kuendesha bodaboda, alikamatwa na askari akituhumiwa kwa wizi wa laptop katika Hotel ya Blue Sky jijini Dodoma akishirikiana na mhudumu mmoja wa hoteli hiyo.

Taarifa zinaeleza kuwa Josephat aliteswa kwa kuwa alikataa kutoa rushwa ili aachiwe. Aligoma kwa sababu alisisitiza kuwa hakuwa na kosa.

Uchunguzi uliofanywa na SAUTI KUBWA unaonyesha kuwa si polisi wala ndugu zake Josephat Hans wanaojua alipo, ingawa polisi mkoani Dodoma walisisitiza kuwa mtuhumiwa huyo aliwatoroka akiwa mikononi mwao.

Baadhi ya watuhumiwa wenzake aliokuwa kuwa mahabusu wanadai kuwa aliitwa na kuchukuliwa na hakurudishwa. Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Gilles Moroto, aligoma kuzungumzia sakata hili.

Alikataa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata hili, na alipoona wamezidi kumpigia simu akawablok namba zao. Walipompigia kwa simu nyingine isiyo yao akapatikana, lakini walipojitambulisha akawakatia simu.

Barua kutoka Jeshi la Polisi iliyotumwa kwa Lusina Kiria, mama mzazi wa Josephat, iliyoandikwa na Jeshi la Polisi, inaeleza kuwa kijana wake, alitoroka akiwa mikononi mwa polisi Machi 6, 2019 baada ya “kuwapiga chenga.”

Lakini uchunguzi wa SAUTI KUBWA unatilia shaka maelezo haya ya mtuhumiwa kutoroka akiwa mikononi mwa polisi kwa sababu taratibu za kipolisi zinawalazimisha askari kusindikiza watuhumiwa mahali popote nje ya gereza wakiwa wamewafunga pingu.

Polisi pia hutakiwa kuwa na silaha katika baadhi ya mazingira, hasa mtuhumiwa anaposhikiliwa kwa ujambazi. Pia imethibitika kuwa madaftari ya za polisi hayakuwa na taarifa za kutoroka kwa Josephat.

Licha ya utata huo wa “kutoroka,” shaka zaidi inabuka baada ya taarifa ya polisi na ile ya wizara kutofautiana.

Utata huo ndiyo ulimfanya mama mzazi wa Josephat Hans kuandika barua mfululizo za kutaka kujua alipo mtoto wake, kwani alipofuatilia kwenye kituo cha polisi, hakukuwa na taarifa kwenye kitabu cha taarifa kuonyesha mtoto wake alipo na makosa aliyofanya.

Wao walimweleza kuwa ametoroka, na wanapofuatilia mtandaoni wanaona kama yupo Iringa. Mama yake akawahoji: “Mnafuatilia kwa mtandao upi wakati simu yake mnayo hapa kituoni? Hebu nionyeshe mtandao mnaotumia.” Alijibiwa: “Usitufundishe kazi…”

Barua kutoka wizarani ya Aprili 30, 2019, iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, kwenda kwa mama yake, ilimsihi asubiri uchunguzi ukamilike ili baadaye apate kujua mustakabali wa kijana wake.

Juni 10, 2019 barua ya siri ya wizara kwenda kwa Lusina inaeleza kuwa uchunguzi uliofanywa unabainisha kuwa Josephat alikiri kufanya matukio ya wizi na uvunjaji kwa kushirikiana na wenzake na pia barua hiyo inathibitisha kwamba Josephat alitoroka akiwa mikononi mwa polisi 6 March 2019.

Dada wa mtuhumiwa huyo, Adelina Jerome Hans, alitilia shaka uwezekano wa ndugu yake kutoroka kwa jinsi alivyokuwa amepigwa na anasimama kwa tabu. Alishuhudia hali ya kaka yake akiwa kituo cha polisi alipompelekea chakula; kwamba alionekana kuwa mnyonge na mwenye maumivu makali, alikuwa akitembea kwa taabu huku akiwa anashikilia ukuta.

Wema Mohamed, ambaye alikuwa mmiliki wa pikipiki aliyokuwa akifanyia kazi Josephat, alisema kuwa kwa miaka miwili ambayo alikaa na kijana huyo hakuwahi kusikia au kuhisi taarifa yoyote ya tabia au tuhuma za wizi.

Mmiliki huyo aliiambia timu yetu ya uchunguzi  kwamba alishangazwa na taarifa za Josephat kukamatwa na polisi kwa tuhuma za wizi.

Katika uchunguzi wa SAUTI KUBWA imebainika kuwa siku chache baada ya kukamatwa, Josephat aliondolewa kituo hicho cha polisi na kupelekwa kusikojulikana. Hakurejea na hakuonekana tena.

Mmoja wa askari aliyejitambulisha kwa jina moja la Malope, kutoka kituo hicho cha Polisi ambaye anatajwa kumkamata Josephat, alipoulizwa kuhusu kadhia hii, alikataa kuzungumza na kusaidia jambo lolote kuhusu suala hilo. Alitaka mwandishi amuulize Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma – ambaye hakutoa ushirikiano.

Miaka miwili imepita sasa, bado Josephat Hans hajulikani alipo na hakuna taarifa yoyote kutoka Makao Makuu ya Polisi inayoeleza maendeleo ya tukio hilo.

Mama mzazi wa Josephat Hans ameitaka serikali kufanyia kazi kadhia hii ili mtoto wake apatikane; au polisi watoe taarifa sahihi juu ya alipo kijana huyo.

Katika MAKALA YA TATU ya uchunguzi huu, vigogo wa Jeshi la Polisi Tanzania wanamulikwa kuhusiana na dhuluma na mauaji ya raia.

MAKALA YA KWANZA ilimulika mauaji ya Leopold Lwajabe, Ofisa Mwandamizi wa Wizara ya Fedha aliyekuwa anasimamia pesa za misaada kutoka Umoja wa Ulaya, na kijana Richard Lombo wa Arusha aliyeuawa na polisi katika Kituo cha Polisi Usa River.

Like
3