Malisa GJ, a.k.a Mwalimu wa zamu, amefanya uchambuzi mfupi juu ya mambo 10 tunayopaswa kujua kuhusu ya hiki kinachoitwa “uchumi wa kati” ambao Tanzania imetangaziwa kuingia. Hebu tufuatane naye katika hoja hizi:
Nitaeleza kuhusu dhana ya uchumi wa kati, kwa lugha rahisi sana ambayo hata mtu ambaye hana ufahamu wa uchumi ataweza kunielewa. Nitatumia mfumo wa maswali na majibu ili kurahisisha usomaji.
Swali la Kwanza: Uchumi wa kati ni nini?
Jibu: Uchumi wa kati ni nadharia mojawapo inayotumiwa na benki ya dunia katika kupima maendeleo ya uchumi wa nchi mbalimbali duniani. Benki ya dunia inazo nadharia 4 za kupima uchumi.
Ya kwanza ni Uchumi wa chini/Fukara (Low income economy). Hizi ni nchi ambazo wastani wa pato lake kwa mtu mmoja mmoja ni chini ya $1,035 (kama TZS 2.3M) kwa mwaka.
Pili ni uchumi wa kati uliodhoofika (Lower-middle income economy). Hizi ni nchi ambazo wastani wa pato la mtu mmoja mmoja ni kuanzia $1,036 hadi $4,045 kwa mwaka. Kama TZS 2.3M hadi 9.2M.
Tatu ni uchumi wa kati ulioimarika (Upper-middle income economy). Hizi ni nchi ambazo wastani wa pato la mtu mmoja mmoja ni kuanzia $4,046 hadi $12,535 kwa mwaka. Yani kuanzia TZS 9.2M hadi 30M kwa mwaka.
Nne ni uchumi wa juu (High income economy). Hizi ni nchi ambazo wastani wa pato la mtu mmoja mmoja kwa mwaka ni kuanzia $12,536 (Yani TZS 30M) na kuendelea.
Swali la Pili: Je, Benki ya dunia inatumia kigezo gani kupima uchumi wa nchi?
Jibu: Inachukua pato ghafi la nchi (GNI) gawanya kwa idadi ya watu wote katika nchi. Yani unachukua kipato cha watu kama Bakhresa, Rostam Aziz, Mo Dewji, Diamond Platnumz, Bashite unachanganya na kipato cha mama ntilie wa Yombo Buza, fundi vibatari wa Irangi Kondoa, fundi makanika wa Ngudu Kwimba, halafu unagawanya kwa watanzania wote hadi aliyezaliwa leo. Kinachopatikana ndio kinaitwa wastani wa Pato la mtu mmoja mmoja (Per capita income).
Lakini hizi ni hesabu za nadharia tu sio uhalisia wa pato la mtu. Ndio maana nchi kama Marekani ambayo wastani wa pato la mtu ni TZS 30M bado kuna masikini wasioweza hata kupata mlo wa siku moja (homeless people). Kwahiyo ni hesabu za nadharia zaidi lakini hatuwezi kuzipuuza. Zina maana kubwa kiuchumi. Nitaeleza badae.
Swali la Tatu: Je, GNI ni nini?
Jibu: GNI ni kifupi cha maneno Gross National Income. Zamani iliitwa Gross National Product (GNP). Hili ni pato ghafi la taifa kwa mwaka. Yani pato la raia wa nchi fulani bila kujalisha lilipozalishwa. Kwa mfano unachukua pato la watanzania wa ndani unajumlisha na pato la watanzania waliowekeza au wanaofanya kazi nje ya nchi. Kinachopatikana ndio kinaitwa GNI.
GNI ni kipimo kizuri cha pato la nchi kuliko GDP (Gross Domestic Product). GDP inaangalia pato ghafi la nchi lililozalishwa ndani ya mipaka ya nchi husika bila kujalisha limezalishwa na nani.
Kama Wachina wamewekeza viwanda hapa, pato lao litahesabiwa kwenye GDP yetu kwa sababu viwanda vyao vipo kwetu, hata kama pesa hizo watazisafirisha baadae kwenda kwao China. Kwahiyo GDP huwa inatoa matumaini hewa. Ndio maana wasomi walidiscorage matumizi ya GDP na badala yake wakashauri tutumie GNI ambayo ina uhalisia zaidi.
Swali la Nne: Je, Tanzania tumefikia hatua gani katika uchumi wa kati?
Jibu: Kama nilivyosema uchumi wa kati uliodhoofu (Lower middle-income economies) unaanzia $1,036 hadi $4,045. Sisi wastani wa pato letu ni $1,080 kwa hiyo tumeingia kundi hili.
Hata hivyo bado sisi ni “vibonde” katika kundi hili. Kuna nchi tupo nazo kwenye kundi moja lakini zipo mbali sana kutuzidi. Kwa mfano wastani wa pato la mtu mmoja mmoja nchini Algeria ni $3,970 (kama 9M) lakini tupo nayo kundi moja wakati wastani wa pato letu ni TZS 2.3M kwa mwaka.
Kahiyo hatupaswi kushangilia sana hadi tukajisahau. Kuna kazi kubwa sana ya kufanya ili kupiga hatua na kwenda angalau kundi la uchumi wa kati ulioimarika (Upper-middle income economy). Ili tufike hapo tunahitaji wastani wa pato la mtu mmoja mmoja lifikie walau TZS 9.2M kwa mwaka.
Sasa jiulize, kama tumetumia miaka 60 (tangu uhuru mpaka sasa) kufikisha 2.3M je tutatumia miaka mingapi kufikia 9.2M ili tuvuke kwenda kwenye uchumi wa kati ulioimarika? Tusipokua makini tunaweza kubaki kwenye kundi hili kwa muda mrefu sana au tukaporomoka na kurudi kwenye kundi la nchi fukara. Tunahitaji kuwa na mikakati mikubwa kama taifa.
Kwahiyo hatujafika nusu ya safari kama wengi wanavyodhani. Maana kuna ambao wakisikia uchumi wa kati wanadhani tupo nusu ya safari kuelekea uchumi wa juu. Hatujafika nusu ya safari. Wala hatujafika nusu ya nusu ya safari. Tupo mwanzo wa nusu ya kwanza ya safari.
Swali la Tano: Je, tumefika uchumi wa kati kwa juhudi za serikali ya awamu ya 5?
Jibu: Kila awamu imechangia lakini serikali ya awamu ya 5 imechangia kidogo zaidi kuliko awamu zilizotangulia. Yani serikali ya awamu ya 5 imefanya kumalizia tu kazi iliyofanywa na waliotangulia. Kwa lugha ya mtaani tunasema kumsukuma mlevi.
Kama kuna pongezi kidogo basi ziende awamu ya 4. Wakati Kikwete anaingia madarakani mwaka 2005 wastani wa pato la mtu mmoja mmoja lilikua $597. Mwaka 2010 akafikisha $740 (ongezeko la $143 kwa miaka mitano). Mwaka 2015 wakati anakabidhi madaraka lilikua $980 (ongezeko la $240 kwa miaka mitano).
Serikali ya JPM imepokea kijiti wastani wa pato la mtu mmoja mmoja likiwa $980 mwaka 2015. Na amefanikiwa kufikisha $1,080 mwaka huu, (sawa na ongezeko la $100 kwa miaka mitano). Hivi hapa anayepaswa kupongezwa zaidi ni nani? Aliyeongeza $240 kwa miaka mitano au aliyeongeza $100 kwa miaka mitano?
Swali la Sita: Je, tulipaswa kuwa hapa?
Jibu: Hapana. Tulipaswa kuwa mbali zaidi. Nchi nyingi tulizolingana nazo kiuchumi wakati tunapata uhuru kwa sasa zipo kwenye uchumi wa kati ulioimarika (Upper-middle income economy). Nchi kama Thailand, Indonesia na Malaysia, wakati tunapata uhuru zilikua maskini kuliko sisi. Lakini kwa sasa zimetuacha mbali sana.
Wastani wa pato la mtu mmoja mmoja kwao ni zaidi ya TZS 10M kwa mwaka. Sisi ndio kwanza tumefika TZS 2.3M halafu tunashangilia nchi nzima kama vile tumepona tetekuwanga. Ukweli ni kwamba tulitakiwa kuona aibu kwa sababu miaka 60 baada ya Uhuru ndio tunafika hatua ambayo wenzetu waliifikia miaka mingi iliyopita.
Ajabu ni kwamba waliotuchelewesha miaka yote hiyo ndio haohao wanaotaka tuwashangilie kwa kutufikisha uchumi wa kati. Tulipaswa kuingia uchumi wa kati wa chini (Lower-middle income economy) miaka ya 1970’s na miaka ya 1990’s tuwe kwenye uchumi wa kati ulioimarika (Upper-middle income economy), na awamu hii tuwe tunapambana kuelekea uchumi wa juu (High Income economy). Lakini jamaa wametuchelewesha kwa miaka 60 na bado wanataka tuwashangilie. Uzwazwa!
Swali la Saba: Faida za kuingia Uchumi wa kati ni zipi?
Jibu: Faida kubwa ni kuongezeka kwa wigo wa uwekezaji kutoka nje. Wawekezaji wengi wakubwa huogopa kuwekeza mitaji yao kwa nchi fukara (Lower Income economy) kwa sababu zina changamoto nyingi sana zinazosababishwa na mifumo kulegalega.
Lakini nchi ikiingia uchumi wa kati ni kiashiria kwamba mifumo imeanza kuimarika, angalau kuna uhakika wa soko, literancy rate ni kubwa, miundombinu imeimarika (hata kama si sana lakini ina afadhali) na huduma za jamii zipo. Kwahiyo wawekezaji huvutwa sana kuja kuwekeza mitaji yao.
Faida nyingine ni kwamba uwezo wa nchi kukopa katika masoko ya Fedha na mitaji unapanuka kuliko ilivyokua awali. Kwahiyo tunaweza kukopa zaidi na kufanya mambo makubwa zaidi. Ni sawa na “mangi” awe anakukopesha sukari kilo mbili kwa sababu anajua mshahara wako ni laki moja. Siku akijua mshahara wako umeongezeka hadi laki 3 atakuambia sasa unaweza kukopa hadi kilo 5 bila wasiwasi.
Swali la Nane: Hasara za kuingia uchumi wa kati ni zipi?
Jibu: Hasara mojawapo ni kupungua kwa misaada kutoka nje. Tulikua tunapewa misaada mingi kwa sababu tulikua nchi fukara, isiyojiweza. Lakini kwa sasa kiwango cha misaada kitapungua. Kwahiyo tutegemee idadi kubwa ya magari ya DFP/DFPA kupungua mtaani.
Ni sawa na kusema kwa sasa tumeanza kutembea kwahiyo hatuhitaji “baby walker” tena. Ile “baby walker” yetu tutanyang’anywa watapelekewa nchi kama Malawi, Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia, Madagascar, Bangladesh na mafukara wengine kama hao.
Hasara nyingine ni kwamba riba ya mikopo itakua kubwa zaidi. Kwa mfano kama kipato chako ni kidogo ukaenda kukopa laki moja benki, riba yako haiwezi kuwa sawa na aliyekopa milioni 10. Wa 10M atapewa asilimia kubwa zaidi ya riba kuliko wewe. Kwahiyo tutarajie kukamuliwa kodi zaidi ili kufidia ongezeko la riba kwa mikopo tutakayochukua kuanzia sasa.
Swali la Tisa: Je tumefika tulipokusudia?
Jibu: Hapana. Kuna watu wanadai tumefika uchumi wa kati kabla ya muda tuliojipangia. Kwamba ilikua tufike 2025 lakini tumefika mapema zaidi. Mtu yeyote anyesema hivi ni MBUMBUMBU. Awe Mbunge, Waziri, Askofu, Sheikh, au baba yako mzazi mwambie “wewe ni Mbumbumbu” kwa herufi kubwa huku ukimtizama machoni bila tashwishwi.
Mwaka 2010 tulitengeneza Dira ya maendeleo ya taifa (Tanzania Development Vision 2025) na tukaweka lengo la kufika Uchumi wa kati wa wastani wa Pato la mtu mmoja mmoja kuwa $3,000 ifikapo mwaka 2025. Kwahiyo hoja sio kuingia uchumi wa kati, hoja ni uchumi wa kati ambao pato la mtu litakuwa $3,000 sawa TZS 7M kwa mwaka.
Ukweli ni kwamba hatujafikia lengo hilo. Tumevuka mstari na kuingia uchumi wa kati lakini lengo letu la kufikia pato la $3,000 mwaka 2025 bado lipo palepale. Kwahiyo mtu anayesema tumefikia lengo kabla ya wakati ni mbumbumbu tu. Hajui anachozungumza.
Ni vizuri ieleweke kuwa sipuuzi hatua tuliyofikia. Ni hatua muhimu sana. Lakini tusibweteke au kupotosha kuwa tumefikia lengo kabla ya muda. Bado tuna kazi kuwa sana. Ili kufikia lengo la $3,000 mwaka 2025 tunahitaji ongezeko la $2,000 katika pato la mtu mmoja mmoja. Je tutaweza? Kama kwa miaka mitano ya JPM tumepata ongezeko la $100 tu, je hadi 2025 tutaweza kupata ongezeko la $2,000 ili kufikia lengo letu la $3,000?
Swali la Kumi: Je, tunaweza kurudi tena kwenye kundi la nchi fukara (Low income economy)?
Jibu: Ndio tunaweza kurudi kama hatutachukua hatua madhubuti za kiuchumi. Kwa kuwa tutapunguziwa misaada sekta nyingi zitaathirika (multiplier effect). Pia kwa kuwa tumepewa wigo wa kukopa zaidi tunaweza kukopa bila mipango na kwa riba kubwa, hivyo kujikuta tumerudi kwenye kundi la nchi fukara.
Pia kama idadi ya watu itaongezeka (tukafyatua watoto kama JPM anavyoshauri) kuna uwezekano wa kurudi kwenye kundi la nchi fukara. Kama nilivyoeleza awali kwamba wastani wa pato la mtu mmoja mmoja (Per capita income) unachukua pato ghafi la nchi (GNI) unagawanya kwa idadi ya watu. Kwa hiyo idadi ya watu ikiongezeka wastani unakuwa mdogo, na idadi ikipungua wastani unakuwa mkubwa. Kwahiyo kuna haja ya kucontrol “birth rate” yetu kwa sasa kuliko ilivyokua awali.
Zipo nchi ambazo zimeporomoka kutoka nafasi walizokuwepo mwaka jana. Algeria imeporomoka kutoka Upper-middle income hadi Lower-middle income. Sudan imeporomoka kutoka Lower-middle income hadi Lower Income economy yani imerudi kwenye kundi la nchi fukara. Kwahiyo tunapaswa kuwa makini zaidi kwa sasa kuliko tulivyokua awali.