BAADA ya Rais John Magufuli kuonekana katika picha akidaiwa kuwa katika mazungumzo ya simu na Rais wa China juzi, watu wengi makini wamekuwa wanahoji umakini wa rais na wasaidizi wake, hasa kuwa kuzingatia aina ya ofisi inayoonekana kwenye picha. Katika maoni binafsi haya, mchambuzi huru anayejiita MenukaJr wa FikraHuru anazungumzia aibu na ushamba vinavyoambatana na picha hizo. SAUTI KUBWA inachapisha maoni yake kama yalivyo. Endelea.
Mimi sijui ni nani aliefanya kosa hili lakini nakulaumu Gerson. Ni wewe!!
Wewe ndie msemaji wa Ikulu, jambo lolote linalotokea Ikulu kuja kwa umma ni kazi yako. Umetukosea sana kwa picha zile chafu namna ile kutoka katika Ofisi ya Rais.
Si kila picha au jambo analofanya Rais lazima litolewe, mambo mengine yanabakishwa kwa ajili ya kumbukumbu za Rais mwenyewe. Kwa kosa hilo mimi ningalikufuta kazi wakati huohuo.
Ni lazima tuiheshimu Ikulu, ni lazima tuiheshimu kazi ya Rais. Mazungumzo kati ya Rais na Rais hayawezi kufanywa maonesho au kama ililazimu tungaliandaa mazingira kufanana na ofisi ya Rais. Mimi ningalikufuta kazi Msigwa, hatuwezi kwenda hivi.
Mtu mmoja ameniuliza; Menuka, Rais wenu siku hizi anafanya kazi zake katika ofisi ya secretary wake!? Nimemjibu NDIO. Huwa siwezi kujitetea katika mambo ya namna hii.
Kwa uzembe mnadhani mnasaidia kutuonesha kuwa Rais yuko busy, huu ni ushamba. Watu wa Iringa bado ni walewale. Picha ile ni chafu, haiko organized hata mafaili yamepangwa kilevilevi.
Pichani juu ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda akiwa ofisini mwake
Zile faili kwa watu smart zingeweza kupangwa vizuri zikaonekana katika mpangilio safi, zikavutia agenda yenu ingefanikiwa.
Kwa taarifa yenu, zile picha zinaweza kutafsirika hivi; Mwenye ofisi ni mvivu, hafanyi kazi zake kwa wakati ndio maana faili zimejaa mezani.
Mwingine anaweza kuona ni uchafu, akasema mwenye ofisi hayuko makini, ofisi haina msaidizi mwenye maarifa ya kupanga faili mezani kwa weredi ndio maana ziko shaghalabghala. Mtu mwingine anaweza kusema faili zimeletwa mezani kwa ajili ya picha za matangazo kwa sababu hakuna muda kati ya simu ya Rais wa China na maandalizi ya picha.
Pichani juu ni marais Paul Kagame wa Rwanda na Uhuru Kenyatta wa Kenya, wakibadilishana maoni katika ofisi ya Rais Kagame
Atasema, picha zilipigwa baadae ndio maana zinamapozi kama zile za kwenye mawe yale. Sijui kwanini tumepeleka watu wa Iringa Ikulu, huu nao ni ushamba vilevile. Watu wa Iringa mmetukomesha!
Rais amekataza picha za kazini, amesema hazina maana tufanye kazi kimya kimya. Siku chache baadae picha za maonesho na mapozi zinatoka IKULU yake. Hii nayo ni kashfa kwa ofisi ya Rais.
Hapakua na ulazima huo au tungaliandaa mazingira mazuri. Ofisi ya Rais kuonekana kama stoo ni aibu Duniani. Watu wengine wanaweza kudhani ni ofisi ya tarishi, tunaiingiza nchi katika mijadala mingi ya kijinga bila sababu.
Pichani juu ni Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya akiwa ofisini mwake
Mda mfupi kabla, Rais alituma salam za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida kufuatia vifo vya ndugu zetu viliyosababishwa na ajali kwa njia ya simu. Tulitumiwa taarifa tupu bila picha ya Rais na simu, tukaelewa. Kwanini mnaifanya Ikulu kuwa uwanja wa maonesho!?
Gerson umeturudisha nyuma tena, unatufedhehesha Duniani. Picha hazina shida lakini picha CHAFU namna ile kutoka katika ofisi ya Rais ni KOSA!!