Maji ni Shida Kubwa Kanda ya Ziwa – Mbowe

 MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema inashangaza kwamba maji ni moja ya changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wengi wa ukanda wa Ziwa Victoria.

Tathmini kutoka mikutano ya hadhara iliyofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mpaka sasa katika mikoa ya Kagera, Geita na Mwanza, imethibitisha kwamba maji ni janga kubwa katika ukanda wote wa ziwa Victoria.

Chadema imeshafanya mikutano kwenye kata na maeneo mbalimbali ya Bukoba Mjini, Bukoba Vijijini, Misenyi, Kyerwa, Karagwe, Muleba Kaskazini na Muleba Kusini, Ngara na Biharamulo (Mkoa wa Kagera) na Chato, Busanda, Geita Mjini, Geita Vijijini, Nyang’whale na Bukombe (mkoa wa Geita) na Buchosa, Sengerema, Kwimba na Sumve (mkoa wa Mwanza).

Leo, akihutubia maelfu ya wananchi wa Nyarugusu jimbo la Busanda (Geita) na Isemengeja, Misasi na Kolomije (jimbo la Misungwi) na Sumve mjini (jimbo la Sumve), Mbowe aliwashawishi wananchi kuachana na utawala wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kwani umeshindwa kabisa kuwaondolea umaskini na kuwatatulia shida nyingi zinazowakabili ikiwemo ya kukosa maji safi na salama ya bomba.

“Maeneo yote ya ukanda wa ziwa Victoria tuliyopita, zaidi ya asilimia 60 hayana maji safi na salama. Ziwa Victoria linawanufaisha watu wa Misri na nchi nyingine, ninyi hamna. Geita mjini, Geita vijijini, Nyarugusu, kote huko wana utajiri mkubwa wa dhahabu lakini hawana maji. Wanakunywa maji yasiyo salama yanayochanganyika na madini yenye sumu ya zebaki inayotumika kwenye shughuli za madini. Uongozi mbovu wa CCM umegeuza utajiri mkubwa wa raslimali kuwa a curse of resources (laana ya raslimali),” alisema Mbowe.

Akinukuu nadharia ya mwanazuoni Thomas Hobbes inayoitwa “social contract” yaani mkataba wa baina ya watawala na watawaliwa, Mbowe alisema ni wajibu wa serikali kuhakikisha wananchi mnapata huduma bora za maji, afya, elimu, barabara, umeme na maendeleo kwa ujumla, kwani wananchi mnalipa kodi na serikali imepewa dhamana ya kukusanya mapato yote yatokanayo na maliasili zetu, kwa sharti la kuyatumia mapato yote yanayopatikana kuwarejeshea wananchi.

“Wananchi wengine hawajui kama wanalipa kodi. Ni hivi …unaponunua mfuko wa simenti (saruji) kwa mfano, serikali inachukua kodi ya shilingi 9,000 mpaka 10,000. Kwenye soda kuna kodi ya shilingi 270 mpaka 300 na kwenye bati kuna kodi ya shilingi 7,000. Kila bidhaa unayonunua, hata sanda, ina kodi inayokwenda serikalini. Kodi hizi zilipaswa kuwaletea huduma bora ya maji safi na salama, lakini serikali ya CCM imeshindwa kufanya hivyo kwasababu ya wizi na ufisadi,” alisema Mbowe

“Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonesha takribani asilimia 40 ya fedha za bajeti ya nchi inapotea kwenye ufisadi. Geita Mjini wana mgodi pale ambao umeingiza zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni moja kwa mwaka uliopita, lakini Geita nayo haina hata maji,” alisisitiza.

Alisisitiza kuwa njia pekee na ya lazima kwa wananchi kujikwamua kutoka kwenye shida kubwa ya maji na umaskini kwa ujumla, ni kujiunga Chadema kwa wingi ili kujenga Chama imara zaidi cha kuing’oa CCM madarakani.

Katika hatua nyingine, Mbowe, kupitia mikutano yote iliyofanyika leo, aliendeleza utaratibu wake wa kuwapigisha wananchi kura ya wazi kuunga mkono au kupinga mkataba wa bandari na maeneo mengine ya kiuchumi ulioingiwa na serikali ya Tanzania na Dubai.

Katika mikutano yote, wananchi wameunga mkono msimamo wa Chadema unaopinga mkataba huo.

Like