ANDIKO hili ni maelezo mafupi ya mtu anayedai kudhulumiwa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera. Ni sauti ya mnyonge. Fuatilia:
Naitwa Robert Razalo wa Bukoba, Kagera. Mwaka 2022 nilinunua Toyota Probox, T 931 DNX toka kwa ndugu Kenerd Kerbela wa Mwanza. Nilihamisha umiliki kutoka kwa Kerned kuja kwangu (Nimeambatanisha kadi ya gari).
Mwaka jana nikaamua kuiuza. Mnunuzi akawa anaitumia huku akiendelea na taratibu za kuhamisha umiliki, ili kadi isome jina lake. Tarehe 27/10/2024 nilipigiwa simu na RCO Kagera akinitaka nifike ofisini kwake. Nilipoenda akaniambia gari niliyouza ilikua ya wizi hivyo niseme niliipataje. Nikamweleza niliinunua kwa Kenerd Kerbela wa Mwanza. Akataka nimpe namba zake. Nikampatia.
Gari ikawekwa kituoni nami nikaachiwa kwa dhamana. Nilipompigia Kerned akasema yeye ndiye mmliki wa kwanza kwani alinunua ikiwa mpya.
Nikatarajia kesi itafunguliwa mahakamani ili tutoe ushahidi. Lakini kesi haikufunguliwa. Nikaomba Polisi watuoneshe mlalamikaji anayedai kuibiwa gari lakini hatukuoneshwa. Nilipofuatilia sana nikaambiwa mtu aliyedai kuibiwa gari alifika akasema gari sio lenyewe. Basi nikaomba wanirudishie gari yangu lakini wakasema upelelezi bado unaendelea.
Yule niliyemuuzia, akafungua kesi ya madai. Mahakama ikataka nimlipe gari nyingine au nimrudishie pesa. Sikua na uwezo wa kumpa gari nyingine wala kumrudishia pesa.
Akarudi Mahakamani kukazia hukumu na kuomba kukamata mali zangu. Mahakama ikampa kibali. Wiki mbili baadae, akaja na dalali wa mahakama hawakukuta mtu nyumbani. Wakavunja geti na kwenye parking wakakuta gari ya jirani yangu. Huwa anapaki kwangu akisafiri. Wakaibeba kwa “crane” na kuondoka nayo. Kisha wakachora nyumba kwa maandishi makubwa kwamba inauzwa.
Kinachoniumiza ni kwamba napitia yote haya wakati RCO alishasema gari ilikamatwa kimakosa, na aliyedai kuibiwa gari alishafika kituoni akasema gari si hiyo. Lakini bado wamekataa kuiachilia. Matokeo gari ya jirani yangu imechukuliwa na nyumba ya familia inataka kupigwa mnada. Naumia sana.
Kwanini RCO anagang’ania gari ambalo halina kosa? Nawaza nitamlipa nini jirani yangu? Nawaza nyumba ikipigwa mnada familia yangu itaishi wapi? Napitia yote haya bila kosa. Polisi wamekiri gari wanayoitafuta sio hiyo, sasa kwanini bado wanaishikilia? Naomba unisaidie kupaza sauti maana nahisi kukata tamaa. Namba zangu ni 0687500735.