SERIKALI ya Rais John Magufuli imeanza rasmi kupambana na viongozi wa dini wanaoikosoa, na sasa imeanza “kushughulikia” makanisa kama njia ya kuadhibu maaskofu walioandika nyaraka za kichungaji katika kipindi cha Pasaka mwaka huu 2018 zilizokuwa zinaonya serikali dhidi ya siasa za kikatili zinazotishia amani ya taifa, SAUTI KUBWA linaeleza kwa uhakika.
Makanisa yanayotishwa, na ambayo serikali imesema inaweza hata kuyafuta ni Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), ikiwa ni njia ya kutoa kisasi dhidi ya mabaraza ya maaskofu wa makanisa hayo.
SAUTI KUBWA linajua kuwa tangu mwanzoni mwa wiki hii kumekuwepo na mawasiliano ya maandishi kati ya wizara ya mambo ya ndani na makanisa hayo katika kipindi hiki, na licha ya makanisa hayo kujibu kwa maandishi hoja na tuhuma za serikali, bado viongozi wa makanisa hayo wameitwa kujieleza mbele ya mamlaka za serikali.
Jana ilikuwa zamu ya Rais wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kujieleza mbele ya mamlaka za kanisa. Askofu Frederick Shoo, Mkuu wa KKKT naye ameshaitwa.
Vyanzo vyetu ndani ya serikali visivyopendezwa na hatua hii vinasema: “Hatujawahi kuona kituko kama hiki. Yaani kuna watu hapa wizarani wametumwa kuchomoa dokumenti katika mafaili ya makanisa hayo ili ionekane kuna kumbukumbu hazipo sawa, kusudi maaskofu waonekane hawakuwa na uhalali wa kutoa nyaraka zao. Inasemekana kuna askofu mmoja aliyetengwa na wenzake ndiye anashirikiana na serikali na kuipa mbinu dhidi ya wenzake, kama njia ya kujisafisha. Aise, inatisha.”
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, shabaha ya serikali ni kutisha na kukomesha maaskofu kwa kuonyesha kuwa licha ya maaskofu hao kutoa nyaraka zao za kichungaji na kuikosoa serikali, baadhi yao hawapo madarakani kihalali, kwa mujibu wa usajili wa kiserikali.
Chanzo kimoja ndani ya Kanisa Katoliki kinasmea: “Hivi ni visasi tu, vya Kaizari dhidi ya Mungu. Wafanye watakavyo, hakuna aliyeshindana na Mungu akapona. Sisi tunawaona wakienda makanisani kuwekewa mikono tunadhani wanakwenda kusali, kumbe wanakwenda kumdhihaki Mungu! Yeyote anayeshindana na Mungu hawezi kushinda, anajitafutia maangamizi yake mwenyewe.”
Viongozi wote wakuu wa makanisa yote mawili hawakupatikana kuzungumzia sakata hili, lakini SAUTI KUBWA lina habari kuwa mabaraza ya maaskofu ya makanisa yote mawili yanaandaa vikao vikubwa kwa ajili ya kujadili suala hili.
Vyanzo vyetu serikalini vinasema serikali inataka kujua makanisa hayo yalitumia vigezo gani kutoa nyaraka hizo za kichungaji na kuzungumzia masuala ya kijamii badala ya kiroho tu.
Vyanzo hivyo vilivyo karibu na msajili wa makanisa, ambavyo vimechungulia mafaili hayo na kuona majibizano ya barua zao, vinasema kwa kifupi:
“Kanisa Katoliki limeeleza kuwa vigezo vilivyotumika ni uhuru wa maoni, uzalendo, na mwaliko wa serikali wa mara kwa mara kwa viongozi wa dini kuisadia katika kuhamasisha wananchi kuwa raia wema. Mamlaka ya kutoa waraka au ujumbe huo yanatokana na mamlaka liliyopewa kanisa Katoliki” ‘Enendeni ulimwenguni kote mkaihubiri injili,’ kama ambavyo maudhui ya ujumbe yalivyogusia.”
KKKT nao walijibu: “Mamlaka ya kusema tulichoandika yamo ndani ya waraka wenyewe, hayatoki duniani wala kwa mwanadamu yeyote. Kanisa linasajiliwa lakini imani haina msajili.”
Majibu hayo yalipofika wizarani yalipelekwa Ikulu ili wakubwa wayaone na kutoa maoni, huku wizara ikisubiri “amri” kutoka juu.
SAUTI KUBWA imeambatanisha hapa moja ya barua kutoka serikalini kwenda kwa kanisa mojawapo.