Mgombea urais kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameahidi kuwa akishinda nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu, Serikali atakayoiongoza itafuta sheria zote zinazominya uhuru wa habari na haki za kiraia zinazotumiwa na Serikali iliyopo madarakani kukandamiza watu.
Mgombea huyo ametoa ahadi hiyo Septemba 26, 2020 wakati wa mkutano kati yake na Wahariri na Waandishi wa habari waandamizi uliofanyika jijini Mwanza, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.
Uhuru wa maoni na utawala wa sheria
Mgombea huyo ambaye mikutano yake ya kampeni inahudhuriwa na umati wa wananchi ametaja miongoni mwa sheria zitakazopitiwa upya, kubadilishwa nap engine kufutwa ni ile inayounda Idara ya Habari Maelezo na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo kiuhalisia ina chembechembe za ukoloni kwa sababu zinaminya uhuru wa maoni, mawazo, kujieleza, kutafuta na kupata habari.
“Chini ya Serikali itakayoongozwa na Chadema uhuru wa maoni, kujieleza, kutafuta na kupata habari utatekelezwa bila kuwekewa vizingiti kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,” anasema Lissu ambaye ni mwanasheria na wakili mahiri nchini Tanzania
Anaongeza; “Taratibu zitakuwa kama ilivyo nchini Ghana ambako siyo tu mtu haitaji usajili kuanzisha chombo cha habari, bali pia hakuna udhibiti wa vyombo vvya habari.”
Wakati akiahidi kulivunja Idara ya Habari Maelezo, mgombea huyo pia ameahidi kuinyang’anya TCRA nguvu ya kupiga faini na kufungia vyombo vya kielektroniki, badala yake itakuwa kuvisajili kwa ajili ya kumbukumbu za kiofisi.
Kuhusu utawala wa sheria, mgombea huyo amesema Serikali itakomesha maamuzi na vitendo vya kibabe vya viongozi wa ngazi zote akitolea mfano agizo la Rais John Magufuli la kuwabomolea nyumba wakazi wa eneo la Kimara, jijini Dar es Salaam licha ya kuwepo zuio la Mahakama.
“Kwa ajili ya kuweka misingi ya kuwazuia wengine watakaoongoza Taifa hili kuonea watu, Serikali chini ya Chadema itawalipa fidia wananchi wote waliovunjiwa nyumba na mali zao zingine kuharibiwa bila kulipwa fidia,” anasema
Kundi lingine litakalofidiwa ni lile la watu waliokamatwa, kuswekwa rumande, kufunguliwa kesi, kufilisiwa au kufungwa kwa uonevu.
“Ni bahati mbaya hiyo bili itakuwa kubwa, lakini tutatafuta fedha hizo. La msingi kwanza tukubaliane kuwa wana haki ya kulipwa kwa mujibu wa sheria,” anasema Lissu
Apangua propaganda ya ubeberu
Akijibu swali kuhusu tuhuma kuwa wanaopigania na kutetea uhuru wa maoni na haki kwa makundi yote ya kijamii wanatumiwa na mabeberu, mgombea huyo amesema hoja hiyo hutumiwa na waliofilisika kisiasa kwa sababu kiuhalisia uhuru wa maoni, demokrasia na maendeleo ya watu ni masuala ya msingi na asili ya binadamu.
Ameahidi kuwa Serikali atakayoongoza itajenga na kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Mataifa mengine bila kusahau taasisi na mashirika ya kimataifa ambao ni wadau muhimu wa maendeleo.
“Tanzania haiwezi kuendelea bila kutengeneza mahusiano na nchi zote marafiki, wahisani, taasisi na mashirika ya kimataifa, asasi za kiraia na wadau wengine wa maendeleo ili kuvutia mitaji na teknolojia kutoka nje,” anasema na kuongeza
“Hatuwezi kuendelea bila kushirikiana na wengine. Hutuwezi kullima na kula korosho zetu wenyewe, Dhahabu, almasi na madini mengine na hata mbuga na hifadhi zetu zinategemea soko na wageni kutoka nje kwenye hizo nchi zinazoitwa za mabeberu.”
Pamoja na kuboresha mahusiano kimataifa, Lissu pia ameahidi kuweka mazingira mazuri yatakayovutia uwekeza na biashara ndani na nje ya nchi na hatimaye kuongeza kipato cha wananchi na Serikali na hatimaye uwezo wa kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Kukuza uchumi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kunahitaji muunganiko na ushirikiano wa kidunia. Hatuwezi kujitenganisha na dunia,” anasisitiza Lissu
Amesema hata Serikali ya CCM inayoeneza propaganda ya ubeberu nayo inategemea na kushirikiana mataifa na taasisi za nje kutekeleza miradi kadhaa ya maendeleo ikiwemo sekta ya ujenzi wa barabara.
Ametumia mkutano huo kuahidi kuondoa ubaguzi uliopo hivi sasa katika mikopo ya elimu ya juu ambapo wanafunzi waliosoma shule binafsi za msingi na sekondari wananyimwa au kupewa asilimia ndogo ya mkopo ikiamini kuwa wazazi au walezi wao wana uwezo kiuchumi, jambo ambalo si sahihi.
“Tutaondoa ubaguzi huo na kushusha kiwango cha riba ya mikopo ya elimu ya juu kutoka asilimia 15 za sasa hadi kiwango cha awali kabida cha asilimia tatu ambayo itaanza kulipwa baada ya aliyekopa kupata ajira au kipato halali ndani au nje ya nchi,” anasema
CCM wahaha kuhujumu msafara wake
“Mgombea wa CCM hakupata mapokezi mazuri alipokwenda mkoani Kagera, sasa walipoona mapokezi yetu wakaamua kuwaanda vijana kuvuruga msafara wetu kwa kuturushia mawe wakiwa kwenye jengo la CCM,” anafichua Llissu
Hata hivyo, mgombea huyo anawapongeza askari polisi waliokuwa wakiongoza msafara wake kwa kulidhibiti kundi hilo.
Anasema hali kama hiyo pia ilijitokeza mkoani Geita ambako kundi la vijana walipanga mawe kuzuia msafara wake kupita kwenye barabara inayopita jirani na ofisi za CCM.
“Kwa mara nyingine polisi waliwadhibiti na kwa Geita walitawanywa kwa mabomu ya machozi. Hata hivyo, nimesikitika kupata taarifa kuwa, RPC na OCD wa Geita nao wamehamishwa kosa lao likiwa ni kuwapiga mabaomu wana CCM,” anasema kwa masikitiko
Anasema hata mkoani Songwe pia amepata taarifa za mkuu wa upelelezi wa mkoa huo kuhamishwa baada ya kukataa amri haramu ya kuwakamata viongozi wa wagombea wa Chadema wakati wa ziara yake.
Pamoja na viongozi hao wa polisi kukumbwa na madhila hayo, Lissu amewapongeza askari wa jeshi hilo kwa kufanya kazi kwa weledi tangu kampeni za uchaguzi mkuu zilipoanza Agosti 26, mwaka huu.