Kishindo cha Mbowe chatikisa Magu

– Asema mitumba ya CCM imeua Pamba ya Wasukuma

SERIKALI ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imeuwa viwanda vingi vya nguo na kusababisha Tanzania kuwa *”Taifa la Wavaa Mitumba”*, huku pamba inayozalishwa nchini, hususan kwenye mikoa ya kanda ya ziwa, ikizidi kuporomoka bei kwa kukosa soko.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, katika mikutano yake aliyoifanya leo kwenye maeneo ya Nyambiti, Mallya, Sishani na Magu Mjini, mkoani Mwanza.

Mbowe pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, wamepiga kambi kubwa kwenye mikoa ya ukanda wa ziwa Victoria, wakiendesha Operesheni kabambe ya kuimarisha chama hicho na kuwasemea wananchi shida zao, inayoitwa Operesheni +255 yenye ujumbe wa “Katiba Mpya: Okoa Bandari Zetu”

Kiongozi huyo amesema, viwanda vingi vilivyoasisiwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, viliuzwa au kubinafsishwa kiholela, lakini kwa ahadi kuwa vingeendeshwa vizuri zaidi.

Matokeo yake, pamba inayozalishwa nchini imepoteza hata soko la ndani lenye zaidi ya watu milioni 60.

Bei ya pamba kwasasa imeporomoka na kufikia Shilingi 1,060 kwa kilo, kutoka bei ya zaidi ya shilingi 2,040 huko nyuma, ikiwa ni mporomoko wa zaidi ya asilimia 50.

Akihutubia maelfu ya wananchi wa Magu, Mbowe amesema:

“Wakati wa Mwalimu, pamba ya Wasukuma ilikuwa na thamani sana kwasababu tulikuwa na viwanda vya nguo. Hapa Mwanza tulikuwa na kiwanda cha Mwatex, Musoma tulikuwa na Mutex, Morogoro tulikuwa na Morogoro polytex, Arusha tulikuwa na Kilitex, Mbeya tulikuwa na Mbeyatex, Dar es Salaam tulikuwa na Urafikitex, Sunguratex

Tulikuwa tunauza nguo mpaka nje ya nchi. Wakashindwa kuendesha viwanda walivyoachiwa na Mwalimu. Wakavibinafsisha kiholela.Vingi vimekufa au kuanguka katika uzalishaji. Wamesababisha Tanzania kuwa Taifa la wavaa mitumba. Pamba ya msukuma imeporomoka bei, imekosa soko na wengine wameacha kabisa kulima pamba kwasababu haiwalipi”

Mwanasiasa huyo aliongeza kuwa mbali na kuuwa viwanda, CCM pia imeuwa benki muhimu za Taifa zilizoanzishwa kwaajili ya kusaidia wakulima na wafanyabiashara.

“Nchi yetu ilikuwa na mabenki. Benki kama CRDB ilianzishwa kama benki ya ushirika ya kusaidia mahitaji kilimo kama ya kununua pembejeo, lakini serikali za kifisadi zilizofuata baada ya Mwalimu zikaibinafsisha. NBC ilikuwa ni benki ya Taifa ya Biashara na NMB ilikuwa sehemu yake. Nazo wakashindwa kuziendesha, wakazibinafsisha. Matokeo yake leo hakuna benki ya uhakika ya kusaidia wakulima,” alisema Mbowe.

Mbali na kuporomoka kwa bei, kilimo cha pamba kinakabiliwa na tatizo la kuwa na tija ndogo ya uzalishaji, ambapo kwa wastani wakulima huvuna kati ya kilo 200 mpaka 300 kwa ekari moja.

Uzoefu wa nchi nyingine kama Brazil unaonesha kuwa wanavuna mpaka kilo 3,000 kwa eneo la ekari moja, tija ambayo ni kubwa kwa zaidi ya mara kumi ya Tanzania.

Tija ndogo katika uzalishaji inasababishwa na huduma duni za ugani na wakulima kukosa pembejeo stahiki za kilimo, husani kukosa mbegu bora na mbolea, huku ruzuku ya mbolea inayodaiwa kutolewa na serikali, ikiwa haifikii walengwa wengi wala kukidhi haja ya malengo yao ya kilimo.

Alihoji: “Kwa hiyo leo, tuna Chama ambacho kimeshindwa kusimamia kilimo; kimeshindwa kusimamia mifugo; kimeshindwa kusimamia uvuvi kimeshindwa kusimamia madini; kimeshindwa kusimamia mbuga zetu za wanyama, wanauza mapori yetu kila mahali, wamehamisha watu kule Loliondo na kuwapa wageni; Chama ambacho kimeshindwa kusimamia mashirika ya umma takribani 450 aliyoyaacha Mwalimu.Na baada ya kushindwa kusimamia kila kitu, sasa wameona haitoshi, wamegawa bandari zetu zote kwa wageni ….what is this (Ni nini hii)?

Alisisitiza kuwa CCM iliyoshindwa kusimamia kila kitu ni hatari ikiachwa iendelee kukaa madarakani, kwani itauza urithi wote wa watoto wa Kitanzania.

“Bandari ni urithi wa watoto wetu. Bandari ni uchumi. Nchi zote zinazotuzunguka kama Congo, Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia na Malawi, hazina bandari, zinategemea bandari yetu kwaajili ya kuingiza mizigo yao kutoka nchi za nje na pia kusafirisha bidhaa zao kwenda nje. Bandari ni roho ya uchumi wa nchi yetu. CCM baada ya kushindwa kuziendesha, wameamua kuwapa Waarabu bandari zote za Tanganyika kwa mkataba wa milele. Ni hatari kuendelea kuongozwa na CCM, tumekuja kuwaandaa kwa mabadiliko,” alisema Mbowe.

Aidha, akiwapigisha kura ya wazi wananchi wa Nyambiti, Sishani, Mallya na Magu Mjini, kuhusu mkataba wa kuendeleza bandari na maeneo mengine ya kiuchumi, ulioingiwa baina ya serikali ya Tanzania na Dubai, uwanja mzima uliunga mkono msimamo wa Chadema wa kupinga mkataba huo na kuipinga CCM inayokubaliana na mkataba huo.

Mbowe aliendelea kuwaomba wananchi kujisajili rasmi kuwa wanachama wa Chadema ili kuipa nguvu zaidi ya kuchukua dola na kujenga Tanzania mpya inayojali haki, uhuru, demokrasia na maendeleo ya kweli ya watu wote.

Like