Kesi ya Mbowe: Mshitakiwa na shahidi wa utetezi “anyukana” na mawakili kizimbani (5)

Kutoka mahakamani kama ilivyoripotiwa na ripota raia, BJ, leo Jumatatu 27.09.2021. Endelea.

Jaji ameshaingia, amekaa na kesi imeshatajwa.

Kesi inasomwa. Ni Kesi namba 16 ya mwaka 2021 Jamuhuri dhidi ya Halfan Bwire, Adam Hassana Kasekwa (Adamoo), Mohammed Abdalah Ling’wenya na Freeman Aikael Mbowe.

Wakili wa Serikali, Wakili Robert Kidando, anatambulisha jopo lake kwa kuanza na yeye mwenyewe:

  1. Robert Kidando
  2. Nassoro Katuga
  3. Ignas Mwanuka
  4. Esther Martin
  5. Tulumanywa Majigo

Wakili Kibatala anawatambulisha mawakili wenzake wa utetezi kwa kuanza na yeye mwenyewe:

  1. Peter Kibatala
  2. Sisty Aloyce
  3. Gaston Garubindi
  4. Idd Msawanga
  5. Alex Massaba
  6. Evaresta Kisanga
  7. Hadija Aron
  8. Michael Mwangasa
  9. Faraji Mangula
  10. Fredrick Kiwhelo
  11. Nashon Nkungu
  12. Jonathan Mndeme
  13. John Mallya

Mshitakiwa wa kwanza anatetewa na Nashon Nkungu

Mshitakiwa wa pili anatetewa na John Mallya

Mshitakiwa wa tatu anatetewa na Fredrick Kiwhelo

Wengine wote wanamtetea mshtakiwa wa nne ambaye ni Freeman Mbowe

JAJI: Siku ya Ijumaa shahidi (mshtakiwa wa pili) alikuwa hajakamilisha utetezi wake. Arejee kwenye kizimba tuweze kuendelea.

(Shahidi anapanda kizimbani).

JAJI: Wakili wa Serikali mpo tayari?

(Wanasema tupo tayari)

JAJI: Upande wa utetezi mmpo tayari?

(Wote wanasema wapo tayari).

JAJI: Shahidi bado upo chini ya kiapo kama tulivyokuapisha siku ya Ijumaa. Unaweza kuchagua kukaa au kusimama. Mawakilibwa Serikali watakuhoji maswali na baadae upande wa utetezi, hususani wakili wako anaweza kuja kukuongoza tena kwa kukuuliza maswali.

SHAHIDI: Nitakaa Mheshimiwa Jaji.

(Shahidi anakaa).

JAJI: Bila shaka Wakili wa Serikali Chavula unaendelea.

WAKILI WA SERIKALI: Naam Mheshimiwa.

JAJI: Tafadhali endelea.

WAKILI WA SERIKALI: Awali siku ya Ijumaa kabla hatujahairisha nilikuuuliza kuhusiana na wale waliokuvamia maeneo ya Rau hawakupata kujitambulisha. Kweli au si kweli?

SHAHIDI: Kweli.

JAJI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Wale watu mlivyotoka pale kwenda Kituo cha Polisi hawakulueleza majina yao akina nani? Kweli au si kweli?

SHAHIDI: Kweli.

WAKILI WA SERIKALI: Walivyokutoa Moshi kukuleta Dar es Salaam hawakukueleza wao majina yao ni akina nani.

SHAHIDI: Kweli.

WAKILI WA SERIKALI: Walipokupeleka Mbweni hawakukueleza majina yao akina nani.

SHAHIDI: Kweli hawakunieleza.

WAKILI WA SERIKALI: Haukupata kuwafahamu majina yao wakati wote.

SHAHIDI: Niliwafahamu kwa wao alipokuwa wanaitana majina yao na nikaja kuthibitisha majina yao hapa Mahakamani walipojitambulisha.

WAKILI WA SERIKALI: Wakati wa kukusafirisha Moshi kuja Dar es Salaam watu wale walikufunga kitambaa usoni

SHAHIDI: Ni sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Ni jacket. Si ndiyo?

SHAHIDI: Ni jacket ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Hukujua ni akina nani unasafiri nao?

SHAHIDI: Kweli.

WAKILI WA SERIKALI: Na hata ulipofika Dar es Salaam ukafikishwa Kituo cha kwanza cha polisi hukujua upo wapi.

SHAHIDI: Kama nilivyoeleza…..

WAKILI WA SERIKALI: We jibu swali langu. Kweli au si kweli?

SHAHIDI: Kweli.

WAKILI WA SERIKALI: Umedai ulipokuwa unasafirishwa ulikalishwa chini kwenye gari. Kweli au si kweli?

SHAHIDI: Ni kweli.

WAKILI WA SERIKALI: Uliweza kujua ni sehemu gani ya gari?

SHAHIDI: Nilikaa upande wa kulia kwa uelewa wangusiyo kwa kuona. Nikafahamu nimekaa nyuma ya gari.

WAKILI WA SERIKALI: Ulikaa nyuma ya gari?

SHAHIDI: Ndani ya gari sehemu ya nyuma.

WAKILI WA SERIKALI: Bila shaka ilikuwa ni haya magari madogo.

SHAHIDI: Siwezi kujua ni gari gani.

WAKILI WA SERIKALI: Unakubaliana na mimi ukiwa umefungwa machoni huwezi kuona?

SHAHIDI: Ndiyo huwezi kuona, ila ukiwa unatendewa unahisi.

WAKILI WA SERIKALI: Ukiwa umefungwa macho huwezi kuona hata kile kifaa wanachokusababishia maumivu.

SHAHIDI: Ni sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Nakurudisha Moshi. Umesema walipokuwa wanakutesa Moshi walikuwa wanakuuliza umekuja Moshi kufanya nini.

SHAHIDI: Ni sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Wewe ukajibu umekuja Moshi kufanya VIP Protection. Ni sahihi?

SHAHIDI: Ni sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Ulisema ulipofika Dar es Salaam kituo cha kwanza cha Polisi walikupa chakula?

SHAHIDI: Ni sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Ni chakula gani?

SHAHIDI: Ugali na mboga za majani.

WAKILI WA SERIKALI: Na wakati wote ulipokuwa pale hukufanyiwa mateso.

SHAHIDI: Sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Na hata ulipokuwa Mbweni hakuna aliyekuja kukupiga?

SHAHIDI: Ni sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Ni lipi Mahakama ichukue kati ya haya mawili. Uliieleza Mahakama kwamba wakati unatoa maelezo hapa Mahakamani kwamba ulitoa maelezo kwa sababu ulikuwa unateswa. Sasa unasema kwamba Kingai na wenzake hawakukupatia mateso isipokuwa walikupa vitisho tu.

SHAHIDI: Rudia swali lako.

WAKILI WA SERIKALI: Wakati wa kesi kubwa umesema kuwa Kingai na wenzake walichukua maelezo yangu baada ya mateso. Leo unasema alikuja Bwana Kingai kunitishia.

SHAHIDI: Umeuliza wakati wa kuchukuliwa maelezo. Mimi wakati wote nilikuwa chini ya mateso.

WAKILI WA SERIKALI: Aahaaaaaa.

MALLYA: Objection! Naomba shahidi akiwa anatoa maelezo yake apewe nafasi ya kumaliza kujibu maswali.

WAKILI WA SERIKALI: Ulipokuwa Dar es Salaam hukuteswa isipokuwa Bwana Kingai alikutishia?

SHAHIDI: Wakili anauliza na kunilisha maneno ambayo mimi mwanzo sikujibu hivyo. Aliniuliza kuhusu kupigwa siyo kuhusu mateso, kwa sababu mimi nilikuwa chini yao na nimefungwa pingu. Bado hayo kwangu ni mateso.

JAJI: Shahidi nafikiri ungejibu sasa hilo unalotaka wala hakuna tatizo kwamba uliteswa au la. Naweza kukusomea.

SHAHIDI: Ningependa unisomee Mheshimiwa Jaji.

JAJI: Kingai hakunipiga tulipokuwa Mbweni, alinipiga na kunitishia.” Sasa tumabie nini kilichokuwa kimetokea

WAKILI WA SERIKALI: Sasa nafikiri umeelewa, kwamba ulitoa maelezo yako baada ya kuteswa na sasa unasema baada ya kuteswa.

SHAHIDI: Miye ananihoji mambo ambayo mimi sikuyasema.

JAJI: Nafikiri wakili sasa unaweza kubadilisha swali. Mallya tusaidie hapo tafsiri yake ni nini.

MALLYA: Kupiga ni kitu kidogo katika jambo kubwa kwenye mateso. Unaweza usipigwe na ukawa upo kwenye mateso.

JAJI: Mawakili wa pande zote mbili nisaidieni hapo.

WAKILI WA SERIKALI: Mahakama ichukue kwamba Dar es Salaam hakupigwa.

KIBATALA: Siyo kwa nia mbaya lakini wakili mwenzangu kakosa mbinu na ulewa

JAJI: Sitaki muingie kwenye malumbano. Nitamhoji shahidi mwenyewe. Je, ungependa tuandike kuwa Dar es Salaam hukupigwa?

SHAHIDI: Ndiyo. Dar es Salaam sikupigwa.

WAKILI WA SERIKALI: Shahidi kwa hiyo tuchukue kuwa maelezo ulichukuliwa baada ya mateso, chini ya Kingai na leo unatuambia ulitishwa?

SHAHIDI: Sijaelewa swali.

JAJI: Maelezo yanayobishaniwa, maelezo yalichukuliwa nje ya muda. Je ulitoa hayo maelezo lakini kwa mateso? Picha ninayopata leo hukutoa maelezo ila ulisaini tu.

SHAHIDI: Sahihi. Ninazungumzia kuwa niliteswa na Kuning’inizwa kama popo au mshikaki

WAKILI WA SERIKALI: Shahidi uliieleza Mahakama Bwana Kingai alikutesa na kutokana na mateso hayo ulilazimika kutoa maelezo. Sasa unasema Bwna Kingai alikuja na karatasi yake akanitaka nisaini na kujaza sehemu ya kuthibitisha. Kipi unachoeleza sahihi?

SHAHIDI: Vyote ichukue.

WAKILI WA SERIKALI: Kwa hiyo Mahakama ichukue vyote?

JAJI: Sasa niandike vipi? Hukutoa maelezo au ulitoa maelezo?

SHAHIDI: Ananiuliza mambo mawili tofauti ambayo hajayatenganisha. Mimi nilitoa maelezo Moshi chini ya mateso. Nilisaini bila mateso.

JAJI: Nilisaini maelezo bila mateso lakini nisaini baada ya vitisho?

SHAHIDI: Ni sahihi Mheshimiwa Jaji.

WAKILI WA SERIKALI: Kabla ya kuletwa Dar es Salaam tarehe saba, kabla ya siku hiyo uliwahi kufika Dar es Salaam?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Makazi yako yapo Dar es Salaam?

SHAHIDI: Hapana.

WAKILI WA SERIKALI: Unafahamu wapi?

SHAHIDI: Kambi ya Jeshi Twalipo na maeneo ya uwanja wa Taifa.

WAKILI WA SERIKALI: Hujawahi kufika Tazara?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Ulishawahi kufika Mbweni?

SHAHIDI: Hapana.

JAJI: Kwa hiyo kabla ya kesi hujawahi kufika Tazara wala Mbweni?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Hakuna wakati unafikishwa Kituo cha Polisi wakakuacha wazi?

SHAHIDI: Sijwahi kutolewa nje ya kituo cha Polisi.

JAJI: Mnaelewana kweli?

JAJI: Kutoka Tazara kwenda Mbweni ulifungwa jacket?

SHAHIDI: Nilifungwa jacket usoni Mheshimiwa. Wakili ulimaanisha hivyo?

WAKILI WA SERIKALI: Ndiyo Mheshimiwa.

JAJI: Sasa nitaomba mnapomtajia Vituo vya Polisi mtaje na majina.

WAKILI WA SERIKALI: Naanza upya. Ulitolewa akitambaa ama jacket lako ulipofikishwa ndani ya Kituo cha Tazara?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Mpaka unaingia Kituo cha Polisi Tazara ulikuwa umefungwa usoni?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Moshi mlikamatwa wangapi?

SHAHIDI: Tulikamatwa wawili.

WAKILI WA SERIKALI: Na nani?

SHAHIDI: Na Mohammed Abdilah Ling’wenya.

WAKILI WA SERIKALI: Wakati wote unasafirishwa hukujua upo wapi?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Kingai na mwenzake Mahita walieleza Mahakama kwamba waliwasafirisha wewe na Ling’wenya kwenye gari moja.

SHAHIDI: Kweli walitoa ushahidi huo.

WAKILI WA SERIKALI: Hakuna mtu aliyewaambia mashahidi wale kuwa si kweli nyie hamkusafirishwa pamoja?

SHAHIDI: Sasaaaaa…

WAKILI WA SERIKALI: Jibu swali langu.

JAJI: Je, ulisikia au hukusikia?

SHAHIDI: Sikusikia.

WAKILI WA SERIKALI: Kama wakati wote unasafirishwa mpaka unafikishwa Kituo cha Polisi Tazara ulikuwa hufahamu Mohammed Abdilah Ling’wenya yuko wapi. Kweli au si kweli?

SHAHIDI: Sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Ulikuwa peke yako kwenye mahabusu?

SHAHIDI: Nilikuwa peke yangu kwenye chumba changu, ila mahabusu wengine walikuwa kwenye vyumba vyao.

JAJI: Kwa hiyo ulikuwa mwenyewe Kwenye chumba cha mahabusu?

SHAHIDI: Ndiyo.

JAJI: Hapakuwa na mahabusu wengine?

SHAHIDI: Walikuwepo kwenye vyumba vyao.

JAJI: Hapa naona tusingeelewana.

MALLYA: Shahidi alitupa picha kuwa kuna mahabusu yenye vyumba vidogo vidogo na yeye alikuwa kwenye kichumba chake ndani ya mahabusu.

JAJI: Naomba kusoma. “Nilifunguliwa jacket nikawa naona sasa. Nikajivuta hadi mlangoni nikaanza kuona mahabusu wengime wakiwa kwenye vyumba vyao.” nafikiri ndicho nilichoandika. Sasa tujielekeze hapo.

WAKILI WA SERIKALI: Umesema ulikuwa peke yako kwenye chumba.

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Kushoto na kulia palikuwa na ukuta?

SHAHIDI: Ni sahihi kabisa.

WAKILI WA SERIKALI: Ulikuwa kwenye tafakari kwanini haya yananitokea, nimekosa nini?

SHAHIDI: Ni kweli.

WAKILI WA SERIKALI: Ulikuwa unaugulia maumivu huku ukitafakari. Kweli au si kweli?

SHAHIDI: Kweli.

WAKILI WA SERIKALI: Nikujeresha Moshi. Unasema walikuning’iniza kama mishikaki kwenye bomba.

SHAHIDI: Kweli.

WAKILI WA SERIKALI: Ulikuwa unaeleaelea ukiwa juu?

SHAHIDI: Kweli.

WAKILI WA SERIKALI: Walikuwa wanakupiga maeneo gani ya mwili wako?

SHAHIDI: Kwenye magoti na kwenye unyayo.

WAKILI WA SERIKALI: Mara ngapi?

SHAHIDI: Mara nyingi.

WAKILI WA SERIKALI: Alikuwa anatumia nguvu kubwa sana?

SHAHIDI: Kweli.

WAKILI WA SERIKALI: Walikuwa wanakupiga kwa kutumia nini?

SHAHIDI: Rungu la chuma.

WAKILI WA SERIKALI: Walikuvunjavunja magoti?

SHAHIDI: Hapana.

WAKILI WA SERIKALI: Eeenhee! Wewe si komandooo bhana!? Hawawezi kukuvunja. Umefuzu sana bhana!

JAJI: Naomba mawakili kama kuna lolote msinong’one tufuate utamaduni wetu. Nafikiri Wakili wa Serikali umeelewa swali la wakili mwenzako.

WAKILI WA SERIKALI: Ni swali tu Mheshimiwa Jaji.

JAJI: Ulikuwa huulizi swali. Ulikuwa unaweka maoni yako.

WAKILI WA SERIKALI: Sawa Mheshimiwa Jaji.

WAKILI WA SERIKALI: Kutokuvunjika kwako ni kwa sababu umefuzu mafunzo ya ukomandoo?

SHAHIDI: Sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Kutokana na ukomandoo wako na kufuzu kwako hukuona haja ya kwenda hospitali?

SHAHIDI: Si sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Umeeleza walikuwa wanakupiga kwa kutumia nini?

SHAHIDI: Nmeshaeleza ni rungu la chuma.

WAKILI WA SERIKALI: Alikupiga mara ngapi?

SHAHIDI: Sikumbuki.

WAKILI WA SERIKALI: Zaidi ya amara 10?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Walikutesa kwa muda gani?

SHAHIDI: Sikumbuki, maana walikuwa wananipiga na kuniacha wakipumzika wanarudi tena.

WAKILI WA SERIKALI: Nyayo zilivunjika?

SHAHIDI: Hapana.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kukupiga kwenye nyayo ulivimba?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Ulipatwa na lengelenge?

SHAHIDI: Lengelenge na kuvilia ni kitu gani?

WAKILI WA SERIKALI: Yote ni hayohayo. Ulipofika Tazara uliweza kutembea?

SHAHIDI: Kwa tabu sana.

WAKILI WA SERIKALI: (Anawafuata mawakili wenzake wa Serikali wananong’ona).

WAKILI WA SERIKALI: Ulieleza Mahakama kuna ugonjwa uliupata ulipokuwa Jeshini. Ni ugonjwa gani?

SHAHIDI: Battle Confusion.

WAKILI WA SERIKALI: Ulisema ulitibiwa Lugalo ukapata nafuu?

SHAHIDI: Kiasi chake.

WAKILI WA SERIKALI: Walikupa dawa za kuwa unameza?

SHAHIDI: Nilikuwa napewa nilipokuwa pale.

WAKILI WA SERIKALI: Uliporuhusiwa ulirudi moja kwa moja kwenye kituo chako cha kazi?

SHAHIDI: Ni sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Ulirudi kwa muda gani.

SHAHIDI: Kwa muda wa miezi miwili.

SHAHIDI: Battle Confusion.

WAKILI WA SERIKALI: Ulisema ulitibiwa Lugalo ukapata nafuu?

SHAHIDI: Kiasi chake.

WAKILI WA SERIKALI: Walikupa dawa za kuwa unameza?

SHAHIDI: Nilikuwa napewa nilipokuwa pale.

WAKILI WA SERIKALI: Uliporuhusiwa ulirudi moja kwa moja kwenye kituo chako cha kazi?

SHAHIDI: Ni sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Ulirudi kwa muda gani.

SHAHIDI: Kwa muda wa miezi miwili.

SHAHIDI: Ameniuliza muda ambao nilikaa kazini baada ya kurejea Kutoka kazini.

WAKILI WA SERIKALI: Taarifa zilizopo Lugalo ulikuwa mtumiaji wa madawa ya kulevya, na siyo Battle Confusion.

SHAHIDI: Hizo taarifa sizijui.

WAKILI WA SERIKALI: Wewe siyo mtumiaji wa madawa ya kulevya?

SHAHIDI: Hapana.

WAKILI WA SERIKALI: Umeeleza Mahakama kwamba wewe hukufukuzwa kwa masuala ya utovu wa nidhamu bali ni ya kiafya.

SHAHIDI: Ni sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Siku ile Kisutu wakati wa PH uliieleza Mahakama uliondolewa jeshini kwa sababu za Kinidhamu. Lipi lilikuwa la ukweli na lipi la uongo?

SHAHIDI: Sijawahi kutoa maelezo popote kuwa nimeondolewa jeshini kwa sababu ya utovu wa nidhamu.

WAKILI WA SERIKALI: Tukiomba Mahakama ikirejea siku ile uliyotoa maelezo upo tayari?

WAKILI WA SERIKALI: Tunaomba Mahakama Itueleze Proceedings za tarehe kumi mwezi wa tisa.

JAJI: Nitasoma mambo ambayo hayakubishaniwa. Kila mshitakiwa alikubali majina na anuani zake zipo sahihi.

JAJI: Washitakiwa wa 1, 2 na 3 wanakubali kuwa walikuwa waajiriwa wa JWTZ mpaka walipoondolewa kwa masuala ya kinidhamu … washitakiwa 1, 2 na 3 walikubali wanafahamianina wa wakiwa wanafanya kazi Ngerengere KJ92.

JAJI: Washtakiwa 1, 2 na 3 walikuwa wanafahamiana kabla ya kesi kuanza.

WAKILI WA SERIKALI: Hukubisha kwamba hukuondolewa Jeshini kwa masuala ya kinidhamu na asasa unasema uliondolewa Jeshini kwa masuala ya kiafya?

SHAHIDI: Siwezi kulijibia.

WAKILI WA SERIKALI: Kwanini huwezi kulijibia?

SHAHIDI: Documents zote sijawahi kuzitolea maelezo. Zilikuja na kuletwa na watu walioandaa.

WAKILI WA SERIKALI: Documents zipi hizo?

SHAHIDI: Zilioletwa kufungulia kesi ya ugaidi.

WAKILI WA SERIKALI: Ulisaini hukusoma?

SHAHIDI: Nilisaini.

WAKILI WA SERIKALI: Na Mahakama ilikusomea?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Unasema ulikuwa kwenye misheni Congo?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Ulikuwa Battalion ya Tatu? Wewe ulikuwa Kikosi cha Mizinga?

SHAHIDI: Hapana.

WAKILI WA SERIKALI: Wewe ulikuwa unafanya nini?

SHAHIDI: Nilikuwa Special Force.

WAKILI WA SERIKALI: Huko Special Force ulikuwa unafanya kazi gani?

SHAHIDI: Kazi zote.

WAKILI WA SERIKALI: Zitaje.

SHAHIDI: Zote kuanzia kupika mpaka kwenda vitani.

WAKILI WA SERIKALI: Huko vitani huwa mnajihusisha na kuteka watu?

SHAHIDI: Siyo kazi yangu kuzungumzia masuala ya vita.

WAKILI WA SERIKALI: Lakini vitani huwa watu wanatekwa.

SHAHIDI: Ukingalia kwenye muvi wanatekwa ila mimi ya vitani siwezi kuyaeleza. Kuna watu wake maalumu wa kuyaeleza.

WAKILI WA SERIKALI: Moja ya kazi ni kulinda lindo. Mnalinda dhidi ya nani?

SHAHIDI: Dhidi ya adui.

WAKILI WA SERIKALI: Unapokuwa umemkamata mtu lindo moja ya mambo ni kumfunga pingu ili asitoroke.

SHAHIDI: Kweli.

WAKILI WA SERIKALI: Kweli kwa sababu mmeyafanya huko vitani.

(Wakili wa Serikali anaongea na tena na mawakili wenzake).

WAKILI WA SERIKALI: Wewe huwa unatesa watu?

SHAHIDI: Sijawahi.

WAKILI WA SERIKALI: Ukiwa umekamata adui ukamfunga pingu utakuwa umemtesa?

SHAHIDI: Utakuwa hujamtesa. Ndiyo maana umemuita adui.

WAKILI WA SERIKALI: Naomba kuwaachia wenzangu.

JAJI: Nawakumbusha tuna dakika 20 kabla hatuja- break.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Mheshimiwa mimi ninayo machache kati ya mengi yaliyoulizwa na mwenzangu.

JAJI: Labda nimuulize shahidi mwenyewe. Una nguvu au tunaweza kuendelea na maswali?

SHAHIDI: Tuendelee Mheshimiwa Jaji.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Wakati umeanza kuulizwa na Wakili wa Serikali umeongea ukweli. Tunaomba uendelee kusema ukweli … wakati unakamatwa, Ling’wenya yeye alikuwa umbali gani?

SHAHIDI: Alikuwa karibu yangu. Sababu nilikuwa pembeni naongea na simu.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Umesema Ling’wenya alishuhudia wakati unawekewa madawa ya kulevya.

SHAHIDI: Siyo yeye tu. Watu wote waliona kwa sababu jambo hilo lilifanyika hadharani mbele za watu.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Kati yako wewe na Ling’wenya nani mtaalamu wa madawa ya kulevya?

SHAHIDI: Hakuna. Suala madawa walisema wao wenyewe kuwa “Tumemkuta na madawa ya kulevya.”

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Kwenye ushahidi wako wako ulisema kuwa kuhusiana na suala la kusaini hati ya kukabidhi vitu vyako.

SHAHIDI: Sikusema.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Ulimuonyesha Jaji kuhusu makovu. Je una makovu mangapi?

SHAHIDI: Mengine yapo kichwani.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Uliiambia Mahakama kuwa makovu haya mengine yatofautishwa na miguuni.

SHAHIDI: Mahakama haikuuliza kuwa hayo mengine yametokana na nini.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Mahakama itatofautishaje sasa?

SHAHIDI: Hiyo ni kazi ya Mahakama siwezi kuifundisha.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Ulipokuwa Mbweni kuna askari alikuambia upo Mbweni baada ya kuwaonea huruma?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Huyo wa pili aliyekuwa anasema huyo askari ni nani?

SHAHIDI: Mohammed Abdilah Ling’wenya.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Kumbe mlikuwa naye na mkaonana Mbweni?

SHAHIDI: Kujua tupo naye nilijua nimesema. Sikuwahi kumuona kwa macho.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Umeiambia Mahakama aliyekupiga rungu Moshi ni nani?

SHAHIDI: Sikuwa namfahamu.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Maelezo aliyokuletea Bwana Kingai ukayasaini na kuyathibitisha ukiyaona utayakumbuka?

SHAHIDI: Siwezi kuyakumbuka kwa sababu sikuyasoma. Labda sehemu za sahihi yangu na nilipoandika.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Wakati unateswa Moshi uliwajibu kuwa umeenda kwa VIP Protection, ukawajibu upo kwenye mazungumzo.

SHAHIDI: Ni kweli.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Wakati Wakili Kibatala anakuuliza wakati wa maelezo ulisema ungeweza kumuita mwajiri wako.

SHAHIDI: Mwajiri mtarajiwa.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Kwa hiyo Mahakama iandike hujawahi na kuajiriwa na mshitakiwa wa nne?

SHAHIDI: Ni sahihi.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Kwa hiyo ni sahihi nikisema katika hayo mazungumzo yenu mliwawahi kufanyia Aishi Hotel?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Wakati mnafanya hayo mazungumzo mlikuwa na mshitakiwa wa tatu?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Wakati upo Tazara unasema uligudua kwa vitu viwili kwa honi ya treni na kuambiwa hiki ni kituo cha kuhifadhia watuhumiwa wa ugaidi.

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Ulishaiambia Mahakama kwamba unatuhumiwa kwa ugaidi?

SHAHIDI: Hapana.

JAJI: Subiri kidogo.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Nina swali moja la mwisho.

WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Wakati unachomwa na bisibisi ushawahi kuiambia Mahakama walikuwa wanataka nini? Kama vile Moshi walikuwa wanakuuliza umefuata nini?

SHAHIDI: Hapana.

JAJI: Sawa tunapumzika kwa muda na tutarejea baada ya dakika 20.

Jaji ananyanyuka.

Mahakama imerejea. Jaji amewahi kabla ya watuhumiwa.

JAJI: Nataka kuanza utamaduni wa kuanza kuzingatia muda. Nikisema naanza saa tatu mtanikuta humu. Nikisema tunaanza saa tatu itakuwa saa tatu kamili. Nikisema saa nne itakuwa saa nne kamili. Itapendeza kama tutazingatia muda.

JAJI: Na huo ndio ustaarabu. Ikitokea mtu ana dharura nijulishwe. Haipendezi kesi ikianza milango inafunguliwa kila saa.

JAJI: Upande wa Jamhuri wapo tayari kuendelea? … Utetezi? … Shahidi?

Wote wapo tayari.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Wakati tukiendelea na hii kesi tangu mwanzoni na Kingai, mawakili wako na ushahidi wako ulihojiwa Mental Status ya akili yako. Ni kweli jambo hili limejitokeza?

SHAHIDI: Ni kweli limejitokeza?

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Kwa usahihi ukaita Battle Confusion?

SHAHIDI: Ni sahihi.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Kama kweli hali hiyo imejitokeza moja ya mambo ambayo litakukumba ni kupoteza kuona mambo kwa usahihi?

SHAHIDI: Sijui.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Hujui kwa sababu hukumbuki wakati ukiwa na tatizo hilo nini kilikuwa kinakutokea?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Umewahi kupoteza uwezo wa watu unaowatambua au maeneo unayoyafahamu?

SHAHIDI: Sijawahi.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Vipi kuhusiana na kutambua muda na tarehe? Umewahi kuwa na tatizo la kuchanganya hivi vitu?

SHAHIDI: Hapana. Sijawahi.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Vipi kwenye kuchukua maamuzi sahihi, kwamba umempiga mtu bila sababu halafu baadaye ukaja kukumbuka?

SHAHIDI: Hapana sijawahi kufanya maamuzi ya namna hiyo.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Kwa sababu ya jambo la Battle Confusion hujaeleza kwanini lilikukuta.

SHAHIDI: Nilieleza Mahakama kuwa tatizo hilo nililipata baada ya kutoka vitani.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Sababu ya Battle Confusion zipo nyingi. Utakubaliana na mimi?

SHAHIDI: Mimi siyo mtaalamu.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Moja ya sababu ya kupata Battle Confusion ni matumizi ya madawa ya kulevya yaliyokithiri. Ni sawa?

SHAHIDI: Sababu zenu hizo siwezi kuwabishia.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Katika kipindi cha hili tatizo ulipangiwa kazi?

SHAHIDI: Nilipangiwa kwenda hospitali.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Ilikuchukua takribani miezi miwili baada ya kurudi jeshini, kabla ya kufukuzwa kazi kwa sababu wewe uliendelea kutumia madawa ya kulevya?

SHAHIDI: Sijawahi kutumia madawa ya kulevya.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Post Dramatic Disorder ni Kitu gani?

SHAHIDI: Sifahamu.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Kama ufahamu kuhusiana na ugonjwa wa Post Dramatic Disorder limefikaje hapa Mahakamani? Umewahi kumwambia nani?

SHAHIDI: Sijawahi kumwambia mtu.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Utataribu baada ya kurudi kazini ulikuwaje?

SHAHIDI: Nilitakiwa kuendelea kuriport hospitali.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Kwa hiyo ugonjwa huu umeathiri utimamu wa akili?

SHAHIDI: Hapana.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Unasema ulienda Moshi kufanya kazi ya VIP Protection. Kile kitabu chenye orodha ya mashahidi na ushahidi wote we ulikipata?

SHAHIDI: Ndiyo. Ninacho.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Kuna chochote mshitakiwa wa nne amesema alikuita wewe na wenzako kwa ajili ya VIP Protection?

SHAHIDI: Sijakiona.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Kwa hiyo hili suala lako la VIP Protection hajalisema, hata alipopewa nafasi ya kusema hakuwahi kulisema popote.

SHAHIDI: Sijui yeye sasa. Miye niliulizwa ndiyo maana nikajibu.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Ulipokuwa unahojiwa na Mawakili wa Serikali ulikuwa unachukua muda sana kujibu, hata wakati mwingine Mheshimiwa Jaji alikuwa akitoa mwongozo. Nikisema una uwezo mdogo au umeathirika kiakili…

SHAHIDI: Kama wewe ni daktari siwezi kukubishia uchunguzi wako, ila miye nilikuwa nashindwa kujibu kwa haraka kwa sababu maswali yanazunguuuuuka. Hayajanyooka.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Nipo sahihi nikisema hali ya akili yako ipo sawasawa?

SHAHIDI: Upo sahihi.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Hujatueleza umuhimu wa kutuleza utimamu wa kwanini umeieleza Mahakama tatizo la akili kwa wakati fulani.

SHAHIDI: Nimeeleza umuhimu kwa kufuatia swali nililoulizwa Mahakamani.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Ina uhusiano gani suala la ugonjwa wako na makosa ya njama za kutenda ugaidi?

SHAHIDI: Kwangu naona vina uhusiano kwa sababu nimeulizwa na Mahakama. Isingekuwa na umuhimu nisingeulizwa.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Je, unajua umuhimu wa kwamba umewahi kupata Battle Confusion?

SHAHIDI: Umuhimu inajua Mahakama yenyewe iliyouliza hilo swali.

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji naomba tukomee hapa. Hakuna swali lingine.

JAJI: Wakili Mallya kama una maswali ya marejeo?

MALLYA: Mheshimiwa Jaji ninayo machache

MALLYA: Swali langu la kwanza kwamba wewe ni komandoo umefundishwa kukaa na njaa na kuhimili mateso. Je, uelewa wako ni nini katika swali hili?

WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Objection. Hilo swali haliruhusiwi katika re-examination. Yeye ange- recall tu katika yale aliyojibu katika examination.

JAJI: Mallya unakubaliana na alichosema Wakili wa Serikali?

MALLYA: Sababu ya muda naomba nirudie swali tu.

JAJI: Hapana. Je, umekubaliana naye?

MALLYA: Sikubaliani naye lakini sababu ya muda narudia swali tu.

JAJI: Sasa hapo tulimalize kwanza kabla hujaenda mbali kuliko kwenda na mambo ambayo mtu hajaridhika nayo.

MALLYA: Sijaja na swali jipya. Napitia maswali yale yale na majibu yale yale.

JAJI: Sawa. Unaweza ukaanza na swali mwanzoni.

MALLYA: Swali langu la kwanza kwamba wewe ni komandoo umefundishwa kukaa na njaa na kuhimili mateso. Je, uelewa wako ni nini katika swali hili?

SHAHIDI: Katika upande wa mafunzo una kanuni zake na taratibu zake na kwa upande wa ukamataji wa watuhumiwa kuna kanuni zake na taratibu zake.

WAKILI WA SERIKALI: Objection!

JAJI: Subiri kwanza shahidi ajibu kwanza tuone kama linahusika na mnachotaka kufanyia objection.

WAKILI WA SERIKALI: Hakuna sehemu tuliyomuuliza kuhusiana na kuvumilia njaa.

JAJI: Mliuliza nini siku hiyo?

Wakili wa Serikali (Chavula): Katika mafunzo yenu mnafundishwa kuvumilia njaa?

JAJI: Kwanini uliuliza hilo swali? Ulilenga ku- establish kitu gani?

WAKILI WA SERIKALI: Nililenga kuwa ni mtu ambaye ni trained na yale ya kukaa na njaa si kitu kigeni kwake.

JAJI: Sawa. Kaeni chini. Nafikiri hakuna kitu kigeni kati ya mlichouliza, kilichoulizwa na kinachojibiwa. Namruhusu Wakili Mallya kuendelea.

MALLYA: Kwa uelewa wako kwanini uliulizwa swali hilo?

SHAHIDI: Nimeelewa kuwa kukaa na njaa ni haki kwangu. Kupitia mateso ni haki yangu na kwamba kukamatwa bila kuzingatia sheria ni haki yangu kwa sababu tu ni vitu nilivyowahi kupitia.

MALLYA: Kuna sehemu umesema ulipigwa na kuna sehemu uliteswa. Mgawanyiko wa hili jambo ukoje?

SHAHIDI: Kupigwa ni sehemu ya mateso. Kutishiwa ni sehemu ya mateso. Ndiyo maana nilisema nilipofika Dar es Salaam nilikuwa bado nipo ndani ya mateso … Kitendo cha kutolewa kwenye chumba na kuambiwa kitakurudia kilichokutokea Moshi ni sehemu ya mateso wakati huo comfortability yangu imeshapotezwa kwa sababu nilikuwa nasimamiwa na nastola.

SHAHIDI: Na vilevile kitendo cha kushinda na njaa ni mateso pia. Kitendo cha kutolewa kituo kimoja cha Polisi na kupelekwa kingime na kubadilishiwa jina unalotambulika na ulimwengu, kwangu iliniathiri na nikaona bado nipo chini ya mateso.

MALLYA: Umeulizwa kumjua au kumwona mahabusu ya Tazara na Mbweni ulipokuwa unasema ulijua yupo ila sikumuona.

SHAHIDI: Nilikuwa nakimaanisha alipokuwa aahabusu nyingine tuliweza kusalimiana hata kwa sauti ya juu. Lakini siyo kuonana kwa face to face.

MALLYA: Nia ya kuonyesha makovu ilikuwa ni nini?

SHAHIDI: Kwa sababu kuonyesha kuwa baada matendo yale yaliacha alama za kuumia, ndiyo maana nikaonyesha makovu.

MALLYA: Umeulizwa pia kuhusiana na kupigwa ukiwa Moshi na kuwaona waliokutesa Moshi kama uliwatambua au hukuwatambua.

SHAHIDI: Kwenye kile chumba nilichokuwa nateswa palikuwa na watu wengi. Wengine nilikuja kuwatambua mbele ya Mahakama na mtu mwingine sikuweza kumfahamu.

MALLYA: Uliulizwa kuhusiana kutobolewa na bisibisi kwenye makalio …

Wakili wa Serikali Objection! Aulize yaliyojitokeza kwenye examination. Hii kwamba elezea hiyo ni maswali ambayo hayaruhusiwi.

JAJI: Wakili Mallya?

MALLYA: Re-examination wajibu wake ni kufanya explanation.

JAJI: Nafikiri Wakili wa Serikali yupo sahihi. Unachouliza unaacha uwanja mpana wa shahidi kueleza jambo jipya badala kuziba mwanya wa kilichoulizwa.

MALLYA: Wale waliokuwa wanakuchoma bisibisi walikuwa wanataka nini?

SHAHIDI: Ilikuwa ni sehemu ya mateso. Walikuwa wanasema nyinyi si mmejifanya kutusaliti? Sasa mtaona.

JAJI: Nafikiri sasa tunafungua boksi kwa kile nilichokuwa naeleza.

MALLYA: Wakili wa Serikali alikuuliza Swali kwamba waliokuwa wanakuchoma bisibisi walitaka kujua nini?

JAJI: Naona mawakili wa serikali wanataka mshauriane hapo. Inaruhusiwa.

MALLYA: Nitarudi baadaye kwenye swali hilo. Je, hapa kwa ufahamu wako kinachoendelea Mahakamani ni jambo gani?

SHAHIDI: Ni shauri dogo katika shauri kubwa.

JAJI: Lile swali lako umeuliza kweli?

MALLYA: Nimeliweka akiba. Nitalirejea.

(Mallya anaenda kushauriana na mawakili wenzake wa utetezi).

MALLYA: Wakati wanakuchoma walikuwa wanataka nini?

SHAHIDI: Muendelezo wa mateso.

MALLYA: Nafikiri nimemaliza.

Shahidi ambaye ni mshtakiwa wa pili anaondoka kizimbani.

JAJI: Wakili Mallya endelea. Uwanja ni wako.

MALLYA: tunae shahidi mwingine.

JAJI: Anaitwa nani?

MALLYA: Mohammed Abdilah Ling’wenya.

JAJI: Jitambulishe.

SHAHIDI: Mohammed Abdilah Ling’wenya. Dini Mwislamu.

Jaji anamtaka aape. Ameapa.

JAJI: Tutapisha Aadhana halafu tutaendelea.

JAJI: Wakili Kibatala ulitaka kuzingumza?

Kibatala: Naomba nimtambulishe Wakili Dickson Matata kwa ajili ya Mshitakiwa wa tatu.

JAJI: Sawa. Nakushukuru.

JAJI: Hapa kuna maelezo. Kuna shida kumuita mshtakiwa wa tatu kuwa shahidi, Serikali?

JAJI: Kiwhelo kuna tatizo kwa mshitakiwa wako kuwa shahidi?

Wakili Kiwhelo: Hapana.

MALLYA: Makazi yako kwa sasa hivi Kimara King’ong’o.

JAJI: Makazi yako kwa sasa hivi?

SHAHIDI: Natokea Gereza la Ukonga.

MALLYA: Kabla ya kukamatwa ulikuwa wapi?

SHAHIDI: Mtwara kampuni DOT kampuni ya kusaga Kokoto.

MALLYA: Kabla ya hapo?

SHAHIDI: Nilikuwa Ngorongoro.

MALLYA: Unamfahamu mshitakiwa wa pili?

SHAHIDI: Ndiyo.

MALLYA: Umemfahamu wapi?

SHAHIDI: Jeshini KJ 92 JWTZ Ngerengere.

MALLYA: Umeanza lini?

SHAHIDI: Mwaka 2008 mpaka 2017.

MALLYA: Kazi gani ulikuwa unafanya?

Shahidi” Komandoo, Special Force.

MALLYA: Unamfahamu vipi mshtakiwa wa pili?

SHAHIDI: Nilikuwa nipo Mtwara nikapigiwa simu na askari mwenzangu ambaye nilikuwa nipo naye jeshini anaitwa Dennis Urio kwamba kuna kazi ya kwenda kumlinda mtu bila kunitajia huyo mtu ni nani. Nikamwambia asubiri nikifika nyumbani aongee na baba, akikubali sawa. Nilipofika nyumbani akapiga simu nikampa akaongea na baba. Baba akauliza si unamfahamu? Nikasema NDIYO. Akaniambia nakuombea dua, nenda.

MALLYA: Siku ya tarehe tano mwezi wa nane 2021 maeneo ya Rau Madukani kulitokea kitu gani?

SHAHIDI: Nilikuwa kwa dada yangu mmoja anaitwa Hasma. Akiwa dukani kwake mimi na Adamoo tukawa tunasubiria chakula.

MALLYA: Kilichokupeleka Rau Moshi ni kitu gani?

SHAHIDI: Tulikuwa tunaenda kukutana na mwajiri wetu ili kuweza kukubaliana naye.

MALLYA: Mshitakiwa wa pili alikuwa anafanya kitu gani?

SHAHIDI: Wakati nipo dukani kwenye upenyo corridor nikasikia kelele sana. Nikataka niende kuona. Nikakuta Adamoo ameshanyanyuliwa na kukabwa. Nikauliza tatizo ni nini? Nikashikwa mkono. Wakaniuliza wewe unamfahamu huyu?

MALLYA: Ulipata kujua ni akina nani?

SHAHIDI: Niliwaona kwa mara ya kwanza. Wakaniuliza unamfahamu huyu? Akatoka mwingine akasema ana pistol, ana pistol, ana pistol.

SHAHIDI: Alinyofoa kutoka mwilini kwa Adamoo upande wa kulia akasema “ana pistol, ana pistol.” Akasema na madawa ya kulevya anayo.

MALLYA: Eleza sasa pistol anatoa wapi?

WAKILI WA SERIKALI: Objection! Anam- feed majibu.

MALLYA: Baada ya kumkuta Adamoo amenyanyuliwa juu kitu gani kiliendelea? … Ukisema alimtolea unataka Mahakama ipate picha gani?

SHAHIDI: Baada ya kuona wanamfanyia Adamoo yale na Adamoo namfahamu na nilikuwa naye muda mrefu, nikauvuta mkono wangu kwa aliyekuwa amenishika. Nikawaambia kuwa Adamoo hakuwa na hivyo vitu. Nikatoa simu na wallet nikaweka kibarazani.

JAJI: Ulitoa simu na nini?

SHAHIDI: Simu na wallet.

MALLYA: Kusema walimuwekea unamaanisha nini?

SHAHIDI: Kwa sababu nilianza safari ya kwenda Moshi na Adamoo kuanzia Chalinze. Nafahamu hakuwa na vitu hivyo.

SHAHIDI: Nikasema huyu mtu kwa kuwa mmemuwekea na mimi ngoja nitoe vitu vyangu.

MALLYA: Wakati huo Adamoo yuko wapi?

SHAHIDI: Wameshusha chini ila wanampiga pale pale chini.

MALLYA: Uliweka vitu vyako wapi?

SHAHIDI: Waliochukua walikuwa ni Polisi.

MALLYA: Kwenye wallet kulikuwa na nini?

SHAHIDI: Palikuwa na pesa.

MALLYA: Kiasi gani?

SHAHIDI: 300,000/-.

MALLYA: Zipo wapi?

SHAHIDI: Sielewi.

MALLYA: Watu waliomvamia Adamoo unaweza kujua walikuwa ni watu wangapi?

SHAHIDI: Walikuwa zaidi ya watano.

MALLYA: Baada ya kupanda gari mmlielekea wapi?

SHAHIDI: Central Moshi.

MALLYA: Kilichofuata nini?

SHAHIDI: Waliotuleta wakatoka baada ya kutuacha. Walitutenganisha. Nakumbuka mmoja alikuwa askari bonge nilimueleza kuwa mimi nilikuwa mwanajeshi. Wakauliza kama nawajua Komba na Msellemu.

JAJI: Komba ni mtu mwingine na Msellemu mtu mwingine.

MALLYA: Nini ulishihudia kinachomhusu Adamoo?

SHAHIDI: Nilishihudia akiwa yeye ni wa kwanza kuinginzwa SELO yake na mimi nikawekwa SELO nyingine.

MALLYA: Walipomtoa SELO ulionaje?

SHAHIDI: SELO ya kwanza ya kwangu na ya pili wakati wanamwingiza SELO yake sikumwona ila wakati wanamtoa alikuja mtu kwenye SELO yangu akaita “Ling’wenya”. Nyuma yake wakampitisha mtu wamemuinamisha.

MALLYA: Ulimtambuaje?

SHAHIDI: Alikuwa na jeans nyeusi na shati la maua maua.

MALLYA: Nini kilifuata?

SHAHIDI: Nilisikia kilio huko alipopelekwa kwa Sababu haikuwa mbali na SELO yangu. Nilisikia kilio akilia na nilimtambua kwa sauti sababu namuitaga sauti ya zege.

MALLYA: Ulitambua sauti ni ya nani?

SHAHIDI: Nilitambua ni sauti ya Adamoo.

MALLYA: Ilikuwa ni sauti ya namna gani?

SHAHIDI: (Sauti) ya mtu anayepigwa. Alikuwa analia … sauti ya mtu anayeteswa.

MALLYA: Ilidumu kwa muda gani?

SHAHIDI: Sina uhakika ila ni kama nusu saa.

MALLYA: Umesikia sauti ya zege analia kwa nusu saa. Nini kilifuata?

SHAHIDI: Baada ya muda mfupi kupita akapitishwa mtu yuleyuke aliyevaa jeans nyeusi na shati la maua maua akiwa hawezi kutembea. Alishikwa huku kushoto na kulia na wakamburuza hadi SELO inayofuata baada ya kwangu.

MALLYA: Nini kilifuata?

SHAHIDI: Nikajua anayefuata ni mimi.

MALLYA: Baada ya kujua anayefuata ni wewe, kilifuata nini?

SHAHIDI: Walinichukua mimi wakanipeleka huko. Nikaenda nikakuta watu wamekaa na wana simu zao wananirekodi. Wakasema taja majina matatu. Nikawatajia. Wakaniuliza “unafanya kazi gani?” Nikawatajia nimetoka Mtwara. Wakanipiga buti wakasema wanajua mimi nimefuata nini Moshi.

MALLYA: Mahita yupi unayemzungumzia?

SHAHIDI: Mara ya mwisho nilimuona hapa mahakamani akitoa ushahidi.

MALLYA: Hapo mlikuwa sehemu gani?

SHAHIDI: Ni ndani ya Central Police palepale. Nilitolewa SELO nikapalekwa kwenye kijumba kidogo. Palikuwa na bomba refu nikiwa nimefungwa mikono na miguu. Mimi kwa ufahamu wangu inaitwa killing zone.

MALLYA: Killing zone ni kitu gani?

SHAHIDI: Unakuwa unaning’inizwa miguu juu kichwa chini.

MALLYA: Kilifuata kitu gani?

SHAHIDI: Nilipigwa sana kwenye unyayo kwa sababu zilikuwa zimekaa juu.

MALLYA: Wakati wanakupiga wanasemaje?

SHAHIDI: Aliyenipiga ni Mahita tu.

MALLYA: Walikuwa wanahitaji kitu gani?

SHAHIDI: Niliwaambia nimekuja kwa kazi ya VIP Protection kwa kumlinda Mwenyekiti wa Chadema. Wakasema “utasema tu”.

MALLYA: Ilichukua muda gani?

SHAHIDI: Kama nusu saa.

MALLYA: Ikawaje?

SHAHIDI: Alikuja mtu aliyevaa kiraia akatoa amri “mwacheni sasa msimpige.”

SHAHIDI: Wakawa wameniweka nimekaa chini nikiwa na pingu na mguuni nimefungwa kamba.

JAJI: Miguuni ulifungwa nini?

SHAHIDI: Miguuni nilifungwa kamba.

MALLYA: Baada ya hapo ulipelekwa wapi?

SHAHIDI: Wakanirudisha SELO. Nikiwa pale nikawa naita Adamoo! Adamoo! Adamoo!

MALLYA: Aliitikia?

SHAHIDI: Aliitika akaniambia vipi Brother!!? Akaniambia huku hoi na yeye akaniambia mimi mwenyewe huku hoi.

JAJI: Ukisema “mimi huku hoi” unamaanisha nini?

SHAHIDI: Yaani nimeumia sana na kuchoka sana.

MALLYA: Mahita alikuwa anakupiga na kitu gani?

SHAHIDI: Sijakishika vizuri lakini kama shaba nzito.

MALLYA: Nini kilifuata?

SHAHIDI: Ilikuwa jioni kigiza kimeingia, nikamwambia tupumzike ndugu yangu. Akajibu “haya”. Mpaka kesho yake wakaja kutuchukua kuelekea Dar.

MALLYA: Mimi na mheshimiwa Jaji tunaweza tusielewe. Ukisema huyu mafuta siyo mengi maana yake nini?

SHAHIDI: Ni kwamba kwa wao walivyonipiga walifikiri sitaweza kutembea. Lakini mimi walipomaliza kunipiga niliweza kutembea na palepale walipomaliza kunipiga nikiwa nimekaa chini niliwaomba waniruhusu nirukeruke kutuliza maumivu. Wakati wanajitoa nje Afande Jumanne akaropoka “Mwenzako amepigwa sana, bahati yako ulipata mtetezi”. Wakati mimi nikiwa tayari ndani ya gari tayari nilimuona Adamoo anatolewa kwa kukokotwa. Wakaniwahi Mahita akampa Goodluck shuka wakanifunga kichwani.

SHAHIDI: Nikawa nimetulia, nikaona mlango wa gari umefunguliwa na mtu akaingia na kuanza safari.

MALLYA: Baada ya kumuona Adamoo wakakuzuia na kukufunika usoni, je, ulimwona akiwa na hali gani?

SHAHIDI: Nilimwona akiwa anakokotwa hawezi hata kutembea.

MALLYA: Baada ya kuinamishwa kichwa na akufungwa shuka usoni kitu gani kilifuata?

SHAHIDI: Nilikuwa kimya wakati huo gari ikawa wakati wote inatembea.

MALLYA: Wakati huo nini kilifuata?

SHAHIDI: Mimi nilikuwa katikatika nimekalishwa kushoto yupo Goodluck na kulia yupo Jumanne. Na hali hiyo niliishuhudia kabla sijapigwa shuka usoni.

MALLYA: Wakati huo nini kiliendelea?

SHAHIDI: Nilikuwa wakati wote kimya hata nikiiinua shingo kujinyoosha wananirudisha tena chini.

MALLYA: Unakadiria ilikuwa ni safari ya namna gani?

SHAHIDI: Ilikuwa ni safari ndefu kama ya mkoa kwa mkoa.

SHAHIDI: Baada ya kufika na gari kusimama nilishushwa kwa kushikwa nyuma kwa kuinamisha na kitambaa changu vilevile mpaka wakafungua geti. Nilipoingia wakanitoa kitambaa.

MALLYA: Wakati huo wote mlisimama kula chakula?

SHAHIDI: Hatukusimama popote kula chakula.

SHAHIDI: Waliponitoa tu kitambaa alijitokeza jamaa mmoja wa Kirangi, mweupe akaniuliza “nini shida?” Kwa mwonekano wake alikuwa na ndevu ndefu na juu alikuwa amevaa combat lakini siyo ya Kitanzania. Nikamwambia mimi nimekamatwa na tumeletwa hapa sijui ni wapi. Akaniambia “Hapa ni Tazara Kituo cha Polisi.”

SHAHIDI: Wakati naongea na yule Mrangi kuna mwingine akajitokeza kijana mweusi. Nikamwambia nimeletwa hapa lakini mimi nilikuwa ni askari. Yule kijana mweusi akasema Vipi MIC, MIC ni neno la kijeshi. Nikamwambia mbona wewe upo hapa? Akaniambia mimi ni askari nilikuwa naswali kwa Azizi Ally kambi yangu ni Twalipo. Alipokuwa amepaki pikipiki nje akiwa anaswali ndani, wakamsubiri atoke wakampini wakamleta Tazara na akasema yupo Tazara kwa miezi nane. Nikamuuliza shida nini? Akasema wanaoletwa hapa ni kesi za kigaidi.

MALLYA: Alikuwa anasema “hapa”. Anamaanisha hapa wapi?

SHAHIDI: Hapa Tazara … Nikamwomba aangalie SELO inayofuata kama kuna mwenzangu kwa sababu wao SELO yao ilikuwa haijafungwa na walikuwa wakifanya mpaka usafi mle ndani. Wao SELO yao walikuwa wanaona kila kitu. Wakaniambia kuna mwenzako mmoja yupo SELO ya mbele. Nikaanza kuita Adamoo! Adamoo! Adamooo! Kuna askari mmoja akasema tuache kelele yeye hajatuleta.

SHAHIDI: Nikawa naendelea kupiga story na yule mwanajeshi niliyemkuta pale. Wenzake wakamshtua asiongee na mimi na mimi wakanipa ishara kwamba watu wenu wanakuja.

MALLYA: Kitu gani kilifuata?

SHAHIDI: Nikawa nachungulia kwenye SELO yangu. Hawakufika kwenye SELO yangu.

MALLYA: Wakati gani tena ulimuona mshitakiwa wa pili?

SHAHIDI: Siku inayofuata nikiwa kwenye SELO siku inayofuata nikasikia kilio. Nikachungulia kule nyuma. Nikaona watu niliokuwa nao Depo JKT, TPDF na 92KJ Komandoo.

JAJI: Tuahirishe hadi saa tisa kamili.

Jaji ameshaingia na shauri limeshatajwa.

Jaji amemkumbusha Lin’gwenya walipoishia.

SHAHIDI: Nilishubudia Chuma Chugulu na Alex akiwa na kijitabu na wenzie wakiwa ‘wana-Depo’ wenzangu kupitia matundu ya dirisha walikuwa wanamtesa mtu, ambapo baade nilimfahamu yule mtu kwa majina anatolewa kwenye magari mabovu alipokuwa anateswa kwa kushikwa na mtu mmoja na mmoja yupo nyuma yake nilimfahamu aliyekuwa anateswa kuwa ni Dennis Urio ambaye ni Luteni wa Jeshi ambaye alinitafutia hii kazi ya VIP Protection kwa Mwenyekiti wa Chadema.

MALLYA: Awali ulisikia kilio baadae ukaona mtu mwenye kitabu na rungu na baadaye Urio anatolewa kule kwenye magari mabovu. Kwa ufahamu wako nani alikuwa anateswa kule?

SHAHIDI: Kwa nilivyoona mimi Luteni Dennis Urio ndiye alikuwa anateswa.

MALLYA: Kwa muda gani ulisikia hiko kilio chake?

SHAHIDI: Siwezi kuwa na uhakika nao ila kama dakika 15 mpaka 20.

MALLYA: Kipi ulitangulia kuona kwanza kati ya Wana- Depo wenzio na baadye askari polisi na Urio?

SHAHIDI: Nilishuhudia Alex ndiye wa kwanza kutoka, baadaye katoka Chuma Chungulu na mapolisi wakiwa na Urio.

MALLYA: Kilifuata nini?

SHAHIDI: Ilipofika usiku nilitolewa nikafungwa kitambaa.

MALLYA: Ulipigwa kitambaa ukiwa wapi?

SHAHIDI: Ndani ya gari.

MALLYA: Kabla ya kufungwa kitambaa uliwatambua waliokuwa ndani ya gari?

SHAHIDI: Nilimtambua Goodluck na Mahita.

MALLYA: Ni kabla ya gari kuondoka ndiyo ulifungwa kitambaa?

SHAHIDI: Ndiyo.

MALLYA: Unaweza kutambua gari ilitumia muda gani?

SHAHIDI: Ni muda mrefu sana. Ila siyo kama ule wa kwenda mkoani.

MALLYA: Kitu gani kiliendelea?

SHAHIDI: Maaskari wakasema mwenzenu Moses Lijenje tumeshamtupa. Ameshatangulia, huku wakinigusa kichwani na kitu nilichokuwa nahisi kuwa ni bastola. “Ukileta ujanja ujanja na wewe tunakutupa.”

MALLYA: Maneno haya ulikuwa unaambiwa wakati gani? Wakati wa safari au baada ya kufika?

SHAHIDI: Wakati wa safari. Tulipofika nilikuwa nimebakia kwenye gari. Nilihisi watu wakifungua milango na kushuka. Ikatoka amri nishushwe. Nikashushwa. Wakaniinamisha chini nikiwa bado na kitambaa usoni pale mapokezi nilipahisi hivyo kwa sababu tulisimama na kuulizwa naitwa? Mmoja akajibu Johnson John. Wakaniinamisha kichwa. Wakanipeleka mpaka SELO. Kule nilipoingia ndiyo wakanitoa kitambaa,

MALLYA: Ulijuaje pale ni SELO?

SHAHIDI: Nilipofikishwa tu ile sehemu nikatolewa kitambaa nikaanza kuona mazingira kama ya Tazara. Kama milango ya chuma na vingine.

MALLYA: Huyu Johnson John waliyemtambulisha ulipata kumjua?

SHAHIDI: Sikupata kumjua. Walinipa jina la bandia.

SHAHIDI: Kesho yake wakati wanakagua mahabusu Johnson John halikuitwa hilo jina. Wakapita mpaka kwenye SELO yangu wakaniuliza we unaitwa nani? Nikawajibu naitwa Johnson John. Alikuwa ni askari wa mwanamke.

MALLYA: Unasema uliambiwa useme jina lako unaitwa Johnson John? Nani alikuambia utaitwa Johnson John?

SHAHIDI: Jumanne. Alinipa na kikaratasi kuwa kuanzia leo mtu yeyote akija utasema wewe ni Johnson John.

MALLYA: Alipopita mtu akakuuliza baada ya kutoitwa jina lako?

SHAHIDI: Nikamwambia naitwa Johnson John. Akawaita askari wengine. Nahisi yule mwanamama alikuwa ni mkubwa wa kituo, na alipotoka akaja askari mwingine akaniambia “sasa tuambie jina lako la ukweli.”

MALLYA: Ukajibu vipi?

SHAHIDI: Nikawajibu kuwa hili nimepewa hapahapa. Wakaniuliza una kesi gani? Nikawajibu nimekamatwa Moshi baada ya kwenda kumlinda Mwenyekiti wa Chadema. Sijajua nimeshikiliwa kwa kesi gani.

MALLYA: Ulifanya jitihada gani kujua pale ulipo ni wapi?

SHAHIDI: Baada ya ile zamu alikuja koplo mweupe nikaanza kuongea naye. Nikamwambia mimi ni mzaliwa wa Mwanza. Akaniambia na yeye alishawahi kuishi Mwanza. Nikamwambia nilishawahi kuwa mwanajeshi wa KJ 92. Akaniambia kuwa kama ulikuwa mwanajeshi wa 92 KJ basi mmeshafika hapa watatu sasa.

MALLYA: Unaweza kuieleza Mahakamani ulijuaje ni Koplo?

SHAHIDI: Kwa uniform zake na jinsi ranks zilivyokaa.

MALLYA: Kuna wakati gani ulimwambia hapa ni wapi?

SHAHIDI: Baada ya kuniambia tumeshafika watatu na hapa ni Mbweni.

MALLYA: Ulipata kujua au kumuona mshitakiwa wa pili? Adamoo.

SHAHIDI: Alinimbia mmoja yupo ila hakai sana mlangoni, anajificha ficha sana kwenye kona katika SELO yake.

JAJI: Umesema mmoja?

SHAHIDI: Kwenye SELO yake hakai mlangoni. Anajibu akiwa apembeni. Ila mmoja nimeongea naye kajitambulisha ni Luteni wa Jeshi anatoka KJ 92. Anaitwa Dennis Urio.

MALLYA: Unaposema anatoka 92 KJ unamaanisha nini?

SHAHIDI: Anatokea Kikosi cha Komandoo.

JAJI: Subiri kidogo. Ulitumia ….?

SHAHIDI: Nilimtumia yule yule askari kuwa yule aliyejificha anaitwa Adamoo. Mwambie Ling’wenya anakuuliza vipi hali?

MALLYA: Ulijuaje aliyejificha ni Adamoo?

SHAHIDI: Ni kwa ufahamu wangu baada ya kuambiwa tupo watatu na na Adamoo na Urio nimewaona Tazara nikajua ndiyo hao hao.

MALLYA: Kitu gani kilifuata baada ya hapo?

SHAHIDI: Aliniambia anaendeela vizuri. Tukawa tumezoeana hata alipokuwa anaingia kazini alikuwa lazima aanze kuita “Sauti ya zegeeeeee….” hata akija kiraia.

MALLYA: Unaweza kukumbuka pale Mbweni ulikaa kwa muda gani?

SHAHIDI: Nilikaa kuanzia tarehe tisa mpaka tarehe 19 nilipofikishwa Mahakamani.

JAJI: tarehe 19 ya mwezi gani?

SHAHIDI: Tisa ya mwezi wa nane mpaka tarehe 19 ya mwezi wa nane mwaka 2020.

MALLYA: Nakurudisha Moshi. Ulipopigwa kwa marungu ukaomba kurukaruka nini maana yake?

SHAHIDI: Niliomba kurukaruka ili nichezeshe visigino. Maumivu yasikae sana.

WAKILI WA SERIKALI: Objection! Wakati shahidi anatoa ushahidi wake asubuhi hakusema kuwa Mahita ndiye aliyempiga.

JAJI: What is your concern katika hilo?

WAKILI WA SERIKALI: Mwanzo halikutajwa jina la Mahita ndiye aliyempiga.

JAJI: Lilisemwa au halikusemwa? Sasa itabidi nirejee nilichokiandika asubuhi.

(Jaji anasoma)

JAJI: Wakati anatoa ushahidi wake mshtakiwa alisema alipigwa na Mahita peke yake. Wengine walikuwa wanauliza kwanini nilikuwa Moshi … Bila shaka Mahita ndiye aliyetajwa kufanya kazi hiyo. Tunaweza kuendelea.

MALLYA: Kile kitendo cha kuomba kurukaruka maana yake ni nini?

SHAHIDI: Yale maumivu ya kupigwa kwenye nyayo kama ningekaa yangezidi. Kwangu niliona bora kurukaruka kuyapunguza. Sikutaka kukaa kabisa.

MALLYA: Wakati unasafirishwa kutoka Kilimanjaro Kuja Dar es Salaam mikono yako ilikuwaje?

SHAHIDI: Ilikuwa imefungwa pingu.

MALLYA: Na uliposhuka pale Tazara mikono yako ilikuwa katika hali gani?

SHAHIDI: Ilikuwa na pingu.

MALLYA: Na ulipokuwa Mbweni mikono yako ilikuwaje?

SHAHIDI: Nilikuwa na pingu.

JAJI: Kwa hiyo ukiwa SELO Tazara na Mbweni mikono yako wakati wote ilikuwa na pingu?

SHAHIDI: Ndiyo Mheshimiwa Jaji.

MALLYA: Wakati wote huo unafungwa pingu unaweza kuielezea Mahakama ulikuwa unajisikiaje?

SHAHIDI: Sikuwa najisikia vizuri. Ukizungatia Goodluck lazima azibane sana zile pingu hata nikimwambia Mahita yeye anasema muache hivyo hivyo.

MALLYA: Wakati wote huo ukiwa Mbweni Adamoo ulimsikia tena?

SHAHIDI: Nilimsikia kwa sababu kila siku asubuhi lazima nimwite “vipi hukooooooo!!” Yeye anajibu “mdogo mdogo.”

MALLYA: Katika Kesi hii ndogo elezea uhusika na ushiriki wake.

SHAHIDI: Pale Rau yeye ndiye alikuwa anatoa amri zote kama kutupiga pingu, kutuchukua, kutuweka kwenye gari. Mahita wakati ananishughulikia katika kijumba nilipopatia mateso yeye ndiye alikuwa akinihoji.

MALLYA: Kwa hiyo ASP Kingai alikuwepo wakati unafanyiwa mateso?

SHAHIDI: Alikuwepo.

MALLYA: Na uwepo wake alikuwa anafanya kitu gani?

JAJI: Tunaweza kuendelea. Unasema ulimuona Kingai Mbweni ulipotolewa nje. Ulitolewa nje na nani?

MALLYA: Ulimuona wakati gani?

SHAHIDI: Wakati Goodluck na Mahita wananitoa nilipishana naye nikapelekwa kwenye kile chumba.

MALLYA: Mheshimiwa Jaji sina swali la ziada.

JAJI: Sijui kama muda uliobakia unatosha kwa maswali au tu-break mpaka kesho.
(Kibatala ananyanyuka na kwenda kwa mawakili wa Serikali kwa mashauriano)

JAJI: Wakili Kibatala?

Kibatala: Busara inatuongoza tupumzike mpaka kesho.

JAJI: Nashukuru sana. Tunaahirisha mpaka kesho saa tatu kamili asubuhi ambapo shahidi wa pili wa utetezi ataendelea kutoa ushahidi wake.

Like
2