Kama ilivyoripotiwa na ripota raia, BJ, leo Ijumaa 24.09.2021.
Jaji ameshakaa na kesi inatajwa. Ni namba 16 ya 2021.
Naomba utulivu ili tuanze.
Jaji: Wakili wa Serikali?
Wakili wa Serikali anajitambulisha na kuwatambulisha wenzake.
- Robert Kidando
- Nassoro Katuga
- Ignas Mwanuka
- Esther Martin
- Tulumanywa Majigo
- Abdalah Chavula
Wakili wa Serikali amemaliza. Anakuja Peter Kibatala wa upande wa utetezi. Anajitambulisha na kuwatambulisha wenzake.
- Peter Kibatala
- Jonathan Mndeme
- Fredrick Kiwhelo
- Dickson Matata
- John Malya
- Sisty Aloyce
- Alex Masaba
- Idd Msawanga
- Gaston Garubindi
- Evaresta Kisanga
- Hadija Aron
- Faraj Mangula
- Maria Mushi
- George Masoud
- Michael Lugina
- Nashon Nkungu
Ni hao tu Mheshimiwa Jaji. Wengine wakifika tutaijulisha Mahakama.
JAJI: Nimeona mawakili wa utetezi wapo upande huu. Je, mpo sawasawa?
WAKILI WA SERIKALI: Sisi tupo sawasawa.
KIBATALA: Tupo sawasawa.
JAJI: Wakili Kidando.
Wakili wa Serikali: Shauri limekuja kwa ajili ya kusikilizwa na mpaka sasa tumeshaleta mashahidi watatu kati ya saba. Tunaomba ahirisho mpaka Jumatatu. tunaomba kupata muda wa kupitia ushahidi uliowasilishwa … Tunaomba kuondoa mashahidi wengine waliobakia kwa dhumuni la kesi ndogo tubakie na haohao watatu tu … ni hayo tu Mheshimiwa Jaji.
JAJI: Kuna lolote kwa upande wa utetezi?
KIBATALA: Hakuna Mheshimiwa Jaji.
JAJI: Shauri hili dogo kwa upande wa Jamuhuri limefungwa. Nitamsikiliza Wakili John Malya.
MALLYA: Mshatakiwa wa pili atajitetea mwenyewe na mashahidi wengine watatu pamoja na yeye watakuwa jumla wanne.
JAJI: Kuna kingine?
MALLYA: Mheshimiwa ni hayo tu.
JAJI: Mpo tayari kuanza utetezi hata sasa au mngehitaji muda wa kujiandaa?
MALLYA: Tupo tayari hata sasa.
JAJI: Shahidi wa kwanza wa shauri dogo la utetezi aje kizimbani.
Shahidi anaelekea kizimbani huku askari wa Magereza akiwa nyuma yake.
JAJI: Tutajie majina yyako kwa ukamilifu wake unaitwa nani.
SHAHIDI: Adam Kasekwa.
JAJI: Kuna Jina limekuwa likitumika la Adamoo unalitambua?
SHAHIDI: Nalitambua.
JAJI: Dini yako Mkristo? Apa.
Shahidi anaapa mbele ya mahakama.
JAJI: Unaweza kutoa ushahidi wako ukiwa umesiamama au umekaa. Wakili John Malya unaweza kuendelea.
MALLYA: Shahidi umetoka kuapa. Unaweza kututambulisha ulipoluja Mahakamani umetokea wapi?
SHAHIDI: Nimetokea Gereza la Segerea.
MALLYA: Siku za nyuma ulikuwa wapi?
SHAHIDI: Nilikuwa askari wa JWTZ kikosi namba 72 Sangasanga Morogoro.
MALYA: Ni Kikosi cha namna gani?
SHAHIDI: Zamani kiliitwa Kikosi cha Makomandoo. Siku hizi kinaitwa Special Force.
MALLYA: Umehudumu kwa miaka mingapi?
SHAHIDI: Miaka sita kuanzia 2012 hadi 2018.
MALLYA: Kipi kilikufanya uache kazi?
SHAHIDI: Sikuacha bali niliachishwa na wakuu wangu.
JAJI: Sijui mnasikia? Maana naona kelele za mvua zinaingilia. Kila mtu anayo haki ya kusikia hii kesi.
(Huko nje mvua inanyesha sana).
JAJI: (alipoona watu hawajaitika anauliza tena) Jamani mnasikia?
Watu wanasema “tunasikia”.
JAJI: Kama mkiona hamsikii tunaweza kubreak kidogo. Hasa mawakili na washitakiwa muwe free.
SHAHIDI: Mwaka 2016 hadi 2017 ulikuwa kwenye Misheni ya Congo na kurejea salama nchini nchini kwangu na kuendelea na kazi … wakuu wangu wakagundua kuwa nina tatizo la Battle Confusion.
MALLYA: Unaweza kumweleza Jaji Battle Confusion inakuwaje?
SHAHIDI: Siwezi kujijua sana lakini ni hali ya askari anaposikia milio ya mizinga na risasi kwa wingi anakuwa hawezi kufanya vile anavyotakiwa na wakubwa wake.
MALLYA: Kwenye afya inaathiri mfumo gani?
SHAHIDI: Mfumo wa akili.
MALLYA: Sasa umeshafukuzwa kazi baada ya Battle Confusion. Je, ulikuwa unafanya shughuli gani?
SHAHIDI: Nilikuwa nafanya biashara ya kununua maharage huko Morogoro sehemu inaitwa Nongwe na kuuza Soko la Lubeho na kote Morogoro.
MALLYA: Unamfahamu mshitakiwa namba nne?
SHAHIDI: Simfahamu sana ila nilitakiwa nikafanye kazi kwake ya VIP Protection.
MALLYA: Hiyo kazi ya VIP Protection ni kazi unayoweza kuifanya?
SHAHIDI: Ndiyo.
WAKILI WA SERIKALI: Objection!
MALLYA: Naondoa hilo swali … ulikuwa ukifanya nini?
SHAHIDI: Nilikuwa kwenye hatua ya mazungumzo ya kazi.
MALLYA: Yalikuwa yanahusisha nini?
SHAHIDI: Ni kuhusiana na majukumu ya kazi na malipo yetu.
MALLYA: Unakumbuka ilikuwa ni lini?
SHAHIDI: Mwishoni wa mwezi wa saba mwaka 2020.
MALLYA: Makubaliano ya kufanya kazi na mshitakiwa wa nne mlikuwa mnafanya wapi?
SHAHIDI: Kwa mara ya kwanza tulifanyia Moshi.
MALLYA: Nakupeleka tarehe tano mwezi wa nane mwaka 2020. Kilitokea nini?
SHAHIDI: Siku hiyo nikiwa na mshitakiwa mwenzangu namba tatu Mohammed Ling’wenya sehemu inaitwa Madukani tukavamiwa na watu kama watano hivi.
SHAHIDI: Walinivamia mimi kwanza wakaanza kunipiga. Mshitakiwa mwenzangu akaja kuniokoa. Alipofika akawauliza “mbona mnapiga huyu mtu?” Wakamuuliza wewe unamfahamu huyu? Akajibu ndiyo namfahamu. Wakachukua madawa na silaha. Nikawasikia wakisema “ana madawa.” Wakati wakiendelea kunishambulia, mshitakiwa mwenzangu akawawahi akitoa vitu mfukoni. Nikasikia kwa maneno akisema huyu mmeshamuwekea madawa? Anamaanisha mimi. Mmemuweka madawa na silaha. Mimi natoa vitu vyangu kabisa msije mkaniweka na mimi. Wakati huo mimi wakiendelea kunishambulia.
MALLYA: Unaweza kuwakumbuka watu hao ukiwa hapa Mahakamani?
SHAHIDI: Hapa Mahakamani nimeshawaona watu wawili.
JAJI: Subiri kidogo. (Anaendelea kuandika).
MALLYA: Ambaye ni nani umewaona hapa Mahakamani?
SHAHIDI: Ramadhani Kingai na Mahita ambao nimekuja kuwafahamu majina yao hapa Mahakamani … Muda mwingi wa matukio walikuwepo.
MALLYA: Hawa watu wawili ambao umewataja walikuwa na majukumu gani?
SHAHIDI: Nilikuwa nawatambua kwa sura na matendo yote wakati wakinipiga na uniwekea madawa na silaha.
JAJI: Ukisema kuwekewa madawa na silaha nini kilichotokea?
SHAHIDI: Wakati wananipiga na wamenibana, akaingiza mkono wake kwenye suruali yangu akasema “ana madawa ya kulevya”. Na mwingine akaingiza kitu nyuma ya mkanda akatoa kitu akasema “ana silaha”.
MALLYA: Hili eneo ambalo tukio limetokea lilikuwa ni eneo la wazi?
SHAHIDI: Pana madukaya kubadilisha M-Pesa na Tigo-Pesa na grosari pembeni.
MALLYA: Wewe ulikuwa sehemu gani?
SHAHIDI: Nilikuwa katikati upande wa kulia wa maduka na upande wa kushoto grocery.
MALLYA: Ulikuwa umeenda kufanya nini?
SHAHIDI: Kuagiza chakula. Nilikuwa naandaliwa nyama ya kuchoma lakini ilikuwa hata kulipa bado.
MALLYA: Nini kilifuata?
SHAHIDI: Baada ya mwenzangu kusema natoa vitu vyangu msije kuniwekea kama mlivyomwekea huyu, wakatukamata wakatufunga kwa pingu na kutuingiza kgari yao.
MALLYA: Baada ya kuingizwa kwenye gari waliwapeleka wapi?
SHAHIDI: Muda wote tulikuwa tunapigwa. Hatukujua tunaelekea wapi. Baadae wakatufikisha Kituo cha Polisi.
MALLYA: Kituo gani?
SHAHIDI: Nilikuaa sikijui. Lakini baada ya kuongea hapa mahakamani ndiyo nimekuja kugundua ni Central Moshi.
MALLYA: Baada ya kupelekwa Central Moshi ni kitu gani kilifuata?
SHAHIDI: Walinitoa pale ndani Kituoni, kuna chumba cha pembeni palikuwa na jopo la watu wengi, wakanivua nguo zote. Nikawa ninaning’iza kwenye kichuma fulani kithili ya mshikaki au popo.
MALLYA: Wakakuning’iza kama popo? Kitu gani kilifuata baadaye?
SHAHIDI: Walianza kunipiga na kunitesa, na muda wote wananiuliza swali “Huku Moshi umekuja kufuata nini?” Nikajibu kuwa huku Moshi nimekuja kufanya VIP Protection kwa Mheshimiwa Mbowe. Hilo jibu hawalitaki wala haliingii akilini.
MALLYA: Baada ya kuteswa na kupigwa, nini kilifuata?
SHAHIDI: Nikiwa siwezi kusimama wakanitoa pingu, wakanivalisha suruali na shati. Wakaanza kunikokota.
JAJI: Ulikuwa umezungumzia kuvaa?
SHAHIDI: Ndiyo. Walinivalisha suruali.
MALLYA: Jambo gani lilifuata baada ya hapo?
SHAHIDI: Ndani ya mle mahabusu kuna kichumba kidogo cha mlango wa nondo wakawatoa watu mle wakanifungia mimi.
MALLYA: Ulijua hatima ya yule mtuhumiwa mwingine?
SHAHIDI: Sikujua hatima yake.
MALLYA: Nini kilifuata.
SHAHIDI: Niliendelea kukaa mlemle ndani.
MALLYA: Kuna ushahidi umetolewa kuwa mlizunguka maeneo mablimbali ya Moshi na Hai.
SHAHIDI: Hapana. Sikutolewa kwenda popote.
MALLYA: Nini kiliendelea?
Shahidi: Ndani ya kile chumba kuna askari alikuja kumwaga maji.
MALLYA: Nini kiliendelea?
SHAHIDI: Kesho yake nilikuja kugundua ni kesho tayari baada ya kuona jua.
SHAHIDI: Wakanitoa. Wakinilazimisha nitembee lakini nikajikuta siwezi kutembea.
(Simu ya mtu mmoja inasumbua na jaji anawataka watu waweke simu zao silence zisiingilie kazi yake na ushahidi wa shahidi. Anasema watu wawe waangalifu wasijekumlazimisha akasema mambo ambayo hakutaka kusema).
JAJI: Endelea. Baada ya kutolewa…?
SHAHIDI: Wakaja watu wakawa wananikokota na kunipandisha kwenye gari.
MALLYA: Unaweza kuwakumbuka hao waliokuwa wanakukokota ni akina nani?
SHAHIDI: Namtambua mtu mmoja anaitwa Goodluck.
MALLYA: Baada ya kukukokota na kukufunga jacket usoni walikupeleka wapi?
SHAHIDI: Sikujua naenda wapi. Nilitambua tu nipo kwenye gari na ikaanza kutembea.
MALLYA: Kitu gani kiliendelea baada ya hapo?
SHAHIDI: Nikiwa ndani ya gari kabla haijatoka kwa muda wa nusu saa, mateso yaliendelea kwa kunichoma choma na bisibisi … wakawa wananiambia “leo ndiyo mwisho wa maisha yako”. Waliniuliza hapa tulipo unamjua nani? Nikajibu kuwa simjui mtu. Wakasema basi na wewe hakuna anayejua upo na akina nani.
MALLYA: Endelea.
SHAHIDI: Nilikuwa nimelazwa kwenye floor ya gari, siyo kwenye siti.
MALLYA: Ikawaje?
SHAHIDI: Baada ya safari ya muda mrefu sana, tukafika sehemu wakanishusha kwa kunikokota vievile na tulipofika kwenye kachumba wakanitoa jacket wakaniuliza “Unajua uko wapi hapa?” Nikawaambia hapana sifahamu … wakafunga mlango nikiwa mlemle ndani nikiwa na pingu lakini jacket wamenivua.
MALLYA: Unamkumbuka aliyekuwa anakuuliza hayo?
SHAHIDI: Namkumbuka ni Goodluck.
MALLYA: Jambo gani lingine lilitokea kwenye kile chumba?
SHAHIDI: Nikiwa na pingu nikajikokota kusogea mlangoni. Bahati Nzuri nikaona watu wengine wamefungiwa Kwenye chumba kingine kidogo mlemle. Nikawauliza ni wapi hapa? Wakajibu “hapa ni Tazara”.
MALLYA: Hao watu waliokuambia hapa upo Tazara ulipata kuwafahamu au ulikuwa huwafahamu?
SHAHIDI: Hapana. Nilikuwa siwafahamu.
MALLYA: Nini kilifuata?
SHAHIDI: Nilikaa pale tarehe saba, nane na tisa. Na ilipofika tarehe tisa usiku wakaja kunichukua usiku.
MALLYA: Umesema umekamatwa Moshi tarehe tano. Je, kati ya tarehe tano mpaka tarehe saba nini kilitokea?
SHAHIDI: Tarehe tano mpaka saba nilikamatwa Moshi na kuteswa kisha nikasafirishwa kuja Tazara. Siku ya tarehe tidsa wakaja kunitoa usiku. Siku hiyo angalau nilikuwa na uwezo wa akutembea. Lakini wakaniambia huku tunakoenda yanaenda kukuta yaleyale ya Moshi. Sasa ujiandae.
MALLYA: Tarehe tisa baada ya kukuambia ujiandae nini kilifuata?
SHAHIDI: Wakinitoa wakanipandisha kwemye gari. Safi ikaanza. Haikuchukua muda kama Moshi. Siku hiyo sikuwekwa chini kama walivyonisafirisha kutoka Moshi. Wakaniingiza kwenye chumba wakanifungua.
JAJI: Subiri Kidogo. Unasema mlipofika wakakushusha?
SHAHIDI: Walifikisha mpaka kwenye chumba. Chumba kilipofunguliwa wakanitoa jacket usoni. Wakaniamuru niingie ndani.
JAJI: Ndiyo!
MALLYA: Rudi nyuma kidogo Shahidi. Baada ya kuambiwa kuwa upo Tazara, ulifanya jambo lolote kuthibitisha upo Tazara?
SHAHIDI: Ilipofika jioni nilikuwa nikasikia mlio wa honi ya treni. Nikagundua nipo maeneo yanayofanana na Tazara.
MALLYA: Sasa tayari upo sehemu nyingine umevuliwa koti machoni. Nini kilifuata?
SHAHIDI: Niligundua kuwa umeshaingia usiku. Kesho yake usiku tena akaja Kingai na Goodluck wakanitoa mle ndani.
MALLYA: Taratibu shahidi ili Jaji aandike.
SHAHIDI: Wakanipeleka kwenye chumba kilichokuwa na meza. Goodluck akawa mlangoni na Kingai akakaa mbele yangu. Tukawa tunatazamana.
JAJI: Ndiyo! Endelea.
MALYA: Pingu unazozungumzia ni zipi?
SHAHIDI: Pingu za chuma.
MALLYA: Kuna wakati wowote walikutoa pingu tangu utoke Moshi?
SHAHIDI: Kingai akaniambia “mateso yanapopungua ujue kuna kuna mambo mazuri yamekaribia”. Tunataka uwe mstaarabu. Hapa kuna nyaraka tunakuja nazo tunataka usaini. Akamwamuru Goodluck anifungue mkono mmoja. Wakanifungua mkono wa kulia wakaendelea kufunga wa kushoto. Mkono wa kulia ukawa free.
MALLYA: Mkono wa kushoto una pingu. Wa kulia na kalamu. Nini kilifuata?
SHAHIDI: Akawa ananionyesha sehemu za kuandika kama “nathibitisha” na kusaini.
MALLYA: Ulipata kujua kimeandikwa kitu gani katika kile Kingai alichokupatia kutibitisha na kusaini?
SHAHIDI: Hapana.
MALLYA: Shahidi pale Moshi umetuambia walikupiga. Wakakulaza kwenye floor sehemu yenye joto kwenye gari. Je una uthibisho wowote unaoweza kuonyesha hapa Mahakamani?
SHAHIDI: Naweza kutihibitish kwa kuonyesha sehemu nilizoumizwa, makovu yanayoeleka kupona na kwenye mguu nimeumia mpaka leo siwezi kutembea vizuri.
JAJI: Kabla hajatuonyesha atueleze yapo sehemu gani. Isije ikawa sehemu ambayo yanaweza kutweza utu wake.
MALLYA: Shahidi, tueleze maeneo ambayo umeumia ni ni maeneo gani yia mwili?
SHAHIDI: Mguu wangu wa kushoto na mkono wangu wa kushoto.
JAJI: Sina tatizo na maeneo hayo. Wakili unaweza kuendelea.
MALLYA: Unaweza kusimama kuionyesha Mahakama.
JAJI: Unaweza kusimama na mimi nitasogea ili niweze kuona.
JAJI anaonyeshwa.
Baada ya Jaji kumtazama kile alichoonyeshwa, anasema: “Sawasawa” halafu anarudi kukaa kwenye kiti chake. Shahidi naye anarudi sehemu yake kuendelea kutoa ushahidi wake.
MALLYA: Kuna wakati ulitaka kumueleza Jaji kwamba kuna vingine ulitaka kumweleza. Ni hivyo?
SHAHIDI: Takribani mwaka mmoja na mwezi sasa tangu niteswe na kuumizwa, sikuwahi kupelekwa hospitali kwa matibabu na mpaka sasa nahisi maumivu makali.
MALLYA: Je, ulipata akutambua kuwa upo kituo gani cha Polisi?
SHAHIDI: Nilikuja kujua nipo Kituo cha Polisi Mbweni.
MALLYA: Ulijuaje kuwa upo Mbweni?
SHAHIDI: Kuna askari polisi alikuwa zamu. Alisema hamtakiwi kujua mpo wapi. Lakini mpo Kituo cha Polisi Mbweni.
MALLYA: Kuhusu kugundua utofauti wa majina yako Mbweni ulijuaje?
SHAHIDI: Siku ya kwanza nafika Mbweni nilifika pale mlangoni nikakabidhiwa kikaratasi kuwa kuanzia siku hiyo naitwa Vicent Juma, na wakikuuliza umekamatiwa wapi niseme nimekamatiwa Tabora. Na useme kesi ya unyang’anyi … ukiseme majina yako tutajua.
MALLYA: Baada ya kujua upo Mbweni nini kiliendelea?
SHAHIDI: Niliendelea kukaa Mbweni muda wote mpaka siku nafikishwa Mahakamani. Na muda wote sikufunguliwa pingu.
MALLYA: Unakumbuka ilikuwa siku gani na Mahakama gani?
SHAHIDI: Ilikuwa tarehe 19 mwezi nane mwaka 2020. Nilipofika Mahakamani ndipo nilikutana na mshitakiwa mwenzangu ambaye tulikamatwa pamoja Moshi na mshitakiwa namba moja.
JAJI: Kama naelewa tangu mtoke Moshi hamkuwahi kuonana.
SHAHIDI: Ndiyo. Hatukuwahi kuonana kwa macho.
MALLYA: Je, mliwahi kuwasiliana?
SHAHIDI: Tukiwa Tazara tukikuwa tunawasiliana kwa sauti akitokea chumba kingine lakini tulikuwa hatuonani.
MALLYA: Tarehe tano Rau Madukani pale Moshi ulisema wamekuwekea vitu. Je, wewe binafsi ulikuwa na nini mfukoni?
SHAHIDI: Nilikuwa na pesa 260,000 taslimu, simu ya Itel na line ya Halotel.
MALLYA: Hivyo vitu vipo wapi?
MALLYA: Nani alichukua?
SHAHIDI: Alichukua mfukoni Goodluck akampatia Kingai.
JAJI: Shahidi bado unayo maji mkononi. Kama utahitaji utasema maana kuulizwa maswali kunatumia sana akili na kuchosha mwili.
SHAHIDI: Asante Mheshimiwa Jaji.
MALLYA: Ukiondoa Kingai na Goodluck kuna mtu mwingine unamkumbuka alikuja Mbweni?
SHAHIDI: Nilimuona Mahita.
MALLYA: Alikuja kufanyeje?
SHAHIDI: Nilimwona wakati wanakuja kuniona. Lakini hakuingia katika kile chumba.
JAJI: Chumba kipi?
SHAHIDI: Chumba kile ambacho kilikuwa na meza mbili na Kingai.
JAJI: Nimekuelewa.
MALLYA: Umesikia wakitoa ushahidi hapa kwamba walikuwa wanawapa matunzo mazuri na walikuwa wanatunza utu wenu.
SHAHIDI: Si kweli.
MALLYA: Walisema kuwa waliharibikiwa na gari Himo, Je, unasemaje kuhusu hilo?
SHAHIDI: Kwangu ni ngumu kuhusu kuelezea kwa sababu tulikuwa tunasimama sehemu nyingi. Lakini nilikuwa nimefungwa usoni nisione kitu.
MALLYA: Je, unakumbuka tangu tarehe tano mpaka Kingai anakuletea maelezo yako usaini zilikuwa zimepita siku ngapi?
SHAHIDI: Siku sita.
MALYA: Kwa sasa sina la zaidi Mheshimiwa Jaji.
JAJI: Wakili Malya unafikiri shahidi wako anaweza kuendelea?
MALLYA: It depends Mheshimiwa Jaji.
JAJI: Nimekupa wewe kuamua. Nilikuwa naweza kuendelea bila kukuuliza.
MALLYA: Anaweza kuendelea Mheshimiwa.
Sasa anaingia Wakili Nashoni.
NASHONI: Je, ni kweli baada ya kupata Battle Confusion hukupatiwa matibabu?
SHAHIDI: Hapana. Nilipatiwa kwa maana nilipelekwa Hospitali ya Lugalo.
NASHON: Kwenye maelezo watu hawa walikuambia sisi hautufahamu na wewe hutufahamu ni sahihi?
SHAHIDI: Ni sahihi?
NASHONI: Ulipata hisia gani kuwa na watu wa namna hiyo?
SHAHIDI: Nilipatwa na wasiwasi nikaona roho yangu ipo mkononi.
WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji, hisia ni kitu gani?
JAJI: Hilo linamuhusu mwenyewe. Kuhusu hisia zake haliwezi kuathiri jambo lolote.
JAJI: Rudia hisia ulisikiaje hisia zako?
SHAHIDI: Niliogopa kwamba naweza kuteswa sana.
NASHON: Umeeleza kuwa ulikuwa unachomwa bisibisi. Je, ni maeneo gani sasa?
SHAHIDI: Maeneo ya mbavu na matakoni.
NASHONI: Ni muda gani tangu ulipokamatwa Moshi kuja Dar es salaam, Tazara?
SHAHIDI: Baada ya siku moja.
NASHON: Uliambiwa kuwa mnaanza safari ya kuja Dar es Salaam au popote?
SHAHIDI: Hapana. Sikuambiwa.
NASHONI: Unaweza kujua kwanini hamkuanza safari ya kuja Dar es Salaam baada tu ya kukamatwa?
SHAHIDI: Hapana.
NASHONI: Unakumbuka kuwa mlifika Arusha baada ya kukamatwa?
SHAHIDI: Sikumbuki na wala halikuwapo jambo hilo.
NASHONI: Unasema ulikuwa na pesa 260,000/-. Unakumbuka kuandikiwa risiti ya pesa hizo?
SHAHIDI: Hapana.
NASHON: Mheshimiwa Jaji maswali yangu ni hayo tu.
JAJI: Wakili Fred na Matata mtauliza maswali wote wawili au mmoja kwa niaba ya mshitakiwa wa tatu?
WAKILI FRED: Kwa niaba ya mshitakiwa wa tatu hatutakuwa na maswali yoyote.
JAJI: Kibatala kwa niaba ya mshitakiwa wa nne.
KIBATALA: Nataka utuambie kwa vitendo ulikabwaje pale Rau Madukani.
SHAHIDI: Nilikuwa naongea na simu nikiwa nimevaa jacket. Huku nikiongea na simu akatokea mtu kwa nyuma akashika mkono wenye simu. Wakati najitetea akatokea kwa mbele mwingine akanishika mkanda hapa kiunoni.
KIBATALA: Unaweza kutonyesha?
SHAHIDI: Bahati nzuri suruali niliyovaa siku ile nakamatwa ndiyo niliyovaa leo. Haina hata luksi.
KIBATALA: Naweza kuona?
SHAHIDI: Ndiyo. Unaweza kusogea kuona.
Kibatala anasogea.
KIBATALA: Sawa. Lakini pia na Mahakama inataka kuona … Wakati wanakukamata hapo ikawaje?
SHAHIDI: Akatokea mtu mbele akanipiga ngumi.
KIBATALA: Unamkumbuka?
SHAHIDI: Ndiyo. Alikuwa dereva wa gari tuliyopanda.
KIBATALA: Kingai alikuwepo eneo la tukio?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Alikuwa anafanya nini?
SHAHIDI: Yeye ndiyo alichukua pesa zangu baada ya kusachiwa.
KIBATALA: Afande anayeitwa Mahita alikuwepo wakati unakamwata?
SHAHIDI: Aliukwepo na yeye ndiye alikuwa wa kwanza kunikaba wakati naongea na simu.
KIBATALA: Uliwezaje kuona tukio hilo la kukabwa?
SHAHIDI: Niliona kwa sababu ilikuwa mchana na nilikuwa na akili timamu.
KIBATALA: Wakati wanafika kukukamata waliijitambulisha kwa mujibu wa PGO na sheria?
SHAHIDI: Hapana. Hawakufanya hilo.
KIBATALA: Na ni kweli kwamba wakati wanakukamata hawakuwa wameshika notebook?
WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa objection. Anachokifanya Wakili Msomi siyo kinacholekezwa kwa mujibu wa Trial within a Trial pamoja na kwamba haijasema ukomo wa maswali. Matters ambazo ni mpya zitaipotezea muda Mahakama.
JAJI: Wakili Kibatala!?
KIBATALA: Kwa heshima na taadhima wakili Msomi mwenzangu hana hoja. Shahidi analindwa na Jaji kama ningemuuliza swali ambalo lingemdhalilisha ningezuiwa. Sijui anamaanisha nini.
JAJI: Sawa. Tuendeleee. Shahidi huyu kwa sasa ni wa utetezi na siyo wa mashitaka. Labda iwe kwa maswali yanayo dhalilisha.
JAJI: Tuendeleeeee.
KIBATALA: Uliwahi kuona mtu ameshika notebook wakati wa zoezi la kukukaba na kukukamata linaendelea?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Wakati unakamatwa ilikuwa ni eneo la wazi. Bila shaka watu wengi walishuhudia wakati wa kukatwa kwako.
SHAHIDI: Ndiyo. Walikuwa wengi.
KIBATALA: Je, uliona wakati wowote Kingai anaita watu washuhudie kukamatwa kwako?
SHAHIDI: Hapana.
KIBATALA: Uliona hapa Mahakamani kitabu chochote ambacho hapa Mahakamani kimeletwa kinaeleza ni aina gani ya silaha ulikamatwa nayo Moshi?
SHAHIDI: Hapana.
JAJI: Wakili, naomba tu break. Ni takribani masaa mawili sasa … Tutaendelea saa saba kamili mchana. Natoa break ya nusu saa kisha tutarejea kuendelea.
Jaji amenyanyuka na kuondoka chumba cha mahakama.
Jaji amesharejea mahakamani. Hii ni saa 7:14
Jaji anapelekewa mafaili ya kesi.
JAJI: Wakili wa Serikali kuna mabadiliko yoyote?
WAKILI WA SERIKALI: Hapana.
JAJI: Upande wa utetetezi kuna mabadiliko yoyote?
KIBATALA: Hapana Mheshimiwa.
JAJI: Nakuita sasa shahidi. Na ninakukumbusha upo chini ya kiapo.
KIBATALA: Kwa kumbukumbu zako kuna shahidi yeyote aliwahi kuwasilisha hapa mahakamani kwamba bastola imeingia kama sehemu ya ushahidi?
SHAHIDI: Hapana. Sijaona.
KIBATALA: Umesikia mashahidi wa Serikali wamesema walipokuchukua Moshi kwamba waliwachukua kwenda kumtafuta Moses Lijenje kwa sababu ya upelelezi?
SHAHIDI: Hapana. Sijaona.
KIBATALA: Kuna nyaraka yoyote imetolewa kwa ushahidi wa upande wa mshitaka kwamba kuna nyaraka inaonyesha gari iliharibika na kutengenezwa?
SHAHIDI: Hapana.
KIBATALA: Ulishawahi kuona shahidi kutoka Moshi Central Polisi Station Moshi kuwa uliingia na kutoka mara kadhaa ukiwa apale kituoni?
SHAHIDI: Hapana.
KIBATALA: Ulimsikia Jumanne ndiyo alikupekua Moshi. Je uliwahi kumwona Jumanne hapa Mahakamani kama shahidi muhimu?
SHAHIDI: Hapana.
KIBATALA: Ulimsikia shahidi kutoka Central Police Station Dar es Salaam kuwa alikabidhiwa watuhumiwa ukiwemo wewe kutoka kwa Jummanne. Je, huyo Jumanne umemuona hapa Mahakamani?
SHAHIDI: Hapana. Sijamwona.
KIBATALA: Umemwona shahidi ambaye ni dereva ambaye gari lake liliharibika Himo na kwamba ndiye aliyewaendesha sehemu mbalimbali?
SHAHIDI: Hapana.
KIBATALA: Umemuona RPC ambaye baada ya gari kuharibika ndiye alitoa gari yake kuwaleta Dar es Salaam kuja kuthibitisha hilo?
SHAHIDI: Hapana. Sijamuona.
KIBATALA: Ulishawahi kumwona hapa Mahakamani dereva wa RPC ambaye aliwachukua na gari yake kutoka Himo kuwaleta Dar es Salaam?
SHAHIDI: Sijamwona.
KIBATALA: Je, hapa Mahakamani ulishawahi kuona kidhibitisho chochote kinachoonyesha gari ya RPC imeruhusiwa kutoka Moshi kuja Dar es Salaam?
SHAHIDI: Hapana. Sijaona.
KIBATALA: Kwanza, kwa uelewa wako wewe, ulitekwa au ulikamatwa?
SHAHIDI: Nilitekwa.
KIBATALA: Je, ulishawahi kusikia hapana Mahakamani Kingai au wenzake wanazungumzia kuhusu pesa zako?
SHAHIDI: Hapana.
KIBATALA: Je, umesikia mashahidi wa serikali wanasema waliwakamata mkiwa mnakula?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Utakubaliana na mimi kama mlienda kula bila shaka ulikiwa na pesa. Je, umesikia hapa Mahakamani wamezungumzia kuhusu pesa ulizokuwa unataka kununulia chakula?
SHAHIDI: Hapana.
KIBATALA: Je, wakati unatoka Rau Madukani kwenda Central Police Station Moshi ulifungwa kitambaa usoni?
SHAHIDI: Hapana.
KIBATAKA: Kwa hiyo ulifungwa kitambaa machoni wakati wa kutoka Moshi kwenda Dar es Salaam na wakati kutoka Tazara kwenda Mbweni?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Ulisema ulipokuwa kituoni Tazara ulipafahamu kwa kusikia honi ya treni?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Nini kingine kilikufanya utambue kuwa upo Tazara?
SHAHIDI: Kwa sababu niliuliza mahabausu wenzangu.
KIBATALA: Unawakumbuka hao mahabusu?
SHAHIDI: Ndiyo. Namkumbuka mmoja alikuwa anavaa kanzu, mrefu kama Msomali na mwingine alikuwa mwanajeshi kutoka Kambi ya Twalipo na wote walikuwa na mashitaka ya ugaidi pia.
KIBATALA: Je, kwa kesi hii hii?
SHAHIDI: Hapana.
KIBATALA: Umesikia shahidi wa Serikali amesema rumande aliwaletea uji ilikuwa shimoni. Je, rumande ya Tazara ipo shimoni?
SHAHIDI: Hapana. Haipo Shimoni.
KIBATALA: Je, mlipoluwa Tazara walikuja maafisa wawili wa JWTZ. Je unawafahamu?
SHAHIDI: Siwafahamu kwa majina ila nawakumbuka kwa sura kwa sababu nilifanya nao kazi kikosi cha 92KJ.
KIBATALA: Je, unafahamu walikuwa wanahusika na nini pamoja na akina Kingai?
SHAHIDI: Sifahamu.
KIBATALA: Wakati unakwenda Mbweni ulijua kuwa unaenda kwenye mateso?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Ni kweli au si kweli kuwa askari aliyekuambia hapa upo Mbweni ingawa hukutakiwa kujua upo wapi alionyesha utu na kwamba unaonewa?
SHAHIDI: Ni kweli. Ni sahihi kabisa.
KIBATALA: Ni sahihi wakati unahojiwa Afande Kingai alikulazimisha usaini maelezo kule Mbweni. Mweleze Mheshimiwa Jaji kuwa Goodluck alipokuwa mlangoni alikuwa ameshika bastola.
SHAHIDI: Sahihi kabisa.
WAKILI WA SERIKALI: Objection! Sheria ya Ushahidi Kifungu146 (1) & (2) ni kwamba cross examination inafanywa na upande wa pili. Kwa madhumuni kama haya tunakubaliana. Ila madhumuni yake ni kwamba anayefanya mahojiano awe kwa ushahidi ambao umesemwa. Lakini hapa cross examination inatumika kuingiza ushahidi mpya tena kwa leading questions ambapo shahidi kazi yake hapa anasema hapa ni kweli. Sijui hapa mheshimiwa tunaipeleka Mahakama wapi. Imekuwa ni practice sana.
JAJI: Kufupisha muda, unaelewa nini kuhusiana na adverse party?
WAKILI WA SERIKALI: Najua Mahakama ndiyo ina haki ya ku- control cross examination ila tukiruhusu hili sisi tutakosa nafasi ya kuhoji. Tulitegemea wenzetu wangeuliza kwa kielelezo ambacho wamekigusa wao.
JAJI: Kuna kingine?
WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji, ni kweli cross examination haina mipaka, lakini sheria imenainisha ni masuala yapi yataulizwa kwenye cross examination. Sheria ya Ushahidi kifungu namba 151 (6) a, b, c.
JAJI: Kwa tafsiri yako je?
WAKILI WA PILI WA SERIKALI: Maana yake ni kwamba anaweza shahidi akaulizwa masuala lakini masuala hayo lazima yajikite katika mambo ya fuatayo … kutikisa ushahidi, yaelekezwe katika kuvumbua ni nani, na nafasi yake katika maisha ni ipi, yaende katika kutikisa uadilifu wake, na uadilifu wake kwa tabia zake kwa mujibu wa kifungu cha 155 cha Sheria ya Ushahidi. Maswali ya ulimwona Goodluck alishika bastola hatufanyi kujua yeye ni nani. Tukiruhusu tutakuwa tunakiuka Sheria. Mahakama ielekeze katika kuhoji shahidi.
JAJI: Umesoma 155 na ngapi?
WAKILI WA PILI WA SERIKALI: 155 yenyewe tu ila ina a, b na c.
WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji, kabla hujaamua tunaomba turejee kifungu cha Sheria ya Ushahidi namba 146 kwamba mahakama yako ndiyo inayoamua kipi kiingie katika ushahidi. Kwamba anachokiuliza Kibatala hakitakiwi kuingia kwenye ushahidi. Swali alililouliza Kibatala kwamba “Hapa upo Mbweni lakini hutakiwi kujua kama hapa upo wapi” na kauliza swali linalofuata kuwa “Je alikuonea huruma”? Je, suala hilo linaweza kuthibitishwa? Na kifungu kidogo cha tatu inapothibitishwa na Mahakama ndipo ushahidi huo unaweza kupokelewa.
JAJI: Ndiyo.
WAKILI WA TATU WA SERIKALI: Kwa maswali aliyokuwa anam- lead shahidi kuwa je, ushahidi uliletwa au haukuletwa, je, ukiwa haukuletwa wataweza kuleta?
JAJI: Kibatala unaweza kujibu?
KIBATALA: Wenzangu wamechanganya dhumuni la ushahidi. Wamechanganya kujua nafasi yao katika kesi hii. Wamechanganya kujua mimi na Malya ni akina nani. Sisi sote ni adverse Party. Tupo upande mmoja na ndiyo maana tulitengana. Kwa hiyo sisi interests zetu ni adverse party. Niende kwa kifungu cha 155. Shahidi anapohojiwa maswali ya dodoso anaweza kuongezewa likiwemo ukiongezeea maswali yoyote. Kifungu cha 152 maswali ya kumwongoza shahidi yanaruhusiwa wakati wa kufanya dodoso. Hakuna mipaka.
KIBATALA: Kwa sababu ya _leading- huenda kuna mitego. Unapouliza maswali yao dodoso unaruhusiwa kuuliza maswali yanayomtega. Kwa hiyo kifungu 155 wenzetu wamekisoma visivyo. Hapa tuna- discuss mchakato wa kielelezo na si kielelezo. Shahidi yupo free. Na hawa siyo mawakili wa mshitakiwa kwamba mshitakiwa amelalamika nimemtesa na maswali. Na mwisho Mallya mwenye mteja wake hajalalamika kuwa namtesa shahidi wake. Halafu kuhusu Goodluck aliongea Mallya wakati wa kuhoji ushahudi wake hawakuhoji. Sasa ikipita imeshapita. Kuhusu Relevance nimemuuliza kitu kilichoingia kwenye ushahidi wa kwanza. Kuhusu kumwita huyo Goodluck mimi naweza kumuita kwa kupitia mshatakiwa wa nne … Wao walitakiwa kumzuia Mallya kuhusu kumuongelea Goodluck kama ilishapita imepita … Kwa ujumla mheshimiwa Jaji yaliyopo ni binafsi ya mawakili wenzetu si maoni ya sheria. Hatuwezi kufunika haki kwa sababu upande fulani unakereketwa. Katazo au ruhusa lazima lipimwe katika vigezo hivyo.
JAJI: Kama nilivyosema wiki iliyopita.
JAJI: Jambo hili linahusu ushahidi gani upokelewe au ushahidi gani usipokelewe. Kwa hiyo najipa tena dakika chache kabla sijaamua. Kwa hiyo nita- break na kuamua.
Jaji ananyanyuka na kuondoka chumba cha mahakama.
Jaji ameingia na ameshapelekewa mafaili.
JAJI: Nimechukua muda mrefu kutafakari hoja zilizoibuliwa na mawakili wasomi. Mawazo yangu ni kuwa kifungu 252,165 na Kifungu 161 cha Sheria ya Ushahidi kinatoa nafasi ya shahidi kuulizwa maswali yoyote isipokuwa yale yanayoteza utu wa mtu.
JAJI: Yapo maamuzi ya mashauri mbalimbali na mengi ya hayo mashauri yana- contradict, ku-shake au kupunguza thamani ya ushahidi uliokwisha kutolewa. Kwa maoni yangu, mtu anapokuwa ana- contradict au kupunguza thamani ya ushahidi wake … kwa maoni si vyema maneno hayo yaanze na neno ‘kweli’ kwa sababu ukiuliza ‘kweli au si kweli’ unamnyima shahidi nafasi ya kuuliza. Unaweza kuondoa kaeneo ‘si kweli’ hivi na hivi lakini sizuii kuuliza swali lolote. Wakili Kibatala unaweza kuendelea.
KIBATALA: Naomba shahidi arudi kizimbani.
(Shahidi amepanda kizimbani).
KIBATALA: Nakuuliza kuhusu sfisa wa polisi Goodluck. Alikuwa ameshika nini mkononi?
SHAHIDI: Alikuwa na pistol mkononi.
KIBATALA: Pistol umeijuaje?
SHAHIDI: Ninaifahamu kwa sababu nimeziona sana.
KIBATALA: Kwani Goodluck kwa kusimama na bastola mlangoni kulikuwa na shida gani?
SHAHIDI: Sikuona shida yoyote, lakini walishani- alert kabla kuwa wakiona siwapi ushirikiano basi hali ya amani itakuwa imeharibika.
KIBATALA: ACP Kingai anasema alikufuata Central Police Station akakupandisha floor ya kwanza na kwenda kukuchukua maelezo.
SHAHIDI: Si kweli.
KIBATALA: Kama ungepewa nafasi wakati wa kutoa maelezo ungemuita au usingemuita mwajiri wako?
SHAHIDI: Ningemuita.
KIBATALA: Kama Freeman Mbowe asingekuwa na nafasi ya kuja, je mwingine wa kumwita kuja kukusaidia kwenye matatizo ni nani?
SHAHIDI: Ningemuita mke wangu.
KIBATALA: Mke wako yuko wapi?
SHAHIDI: Chalinze.
KIBATALA: Nakurudisha Moshi. Kwamba mahabusu ilimwagiwa maji. Tatizo lako lipo wapi? Je, kama wanasafisha?
SHAHIDI: Nilijua mateso yanaendelea kwa sababu sikuweza kulala.
KIBATALA: Ukawa unafanyeje?
SHAHIDI: Nilikuwa nimekaa usiku kucha.
KIBATALA: Ulipewa chakula lini na wapi?
SHAHIDI: Tazara.
KIBATALA: Moshi hukupewa chakula?
SHAHIDI: Sikupewa chakula Moshi.
KIBATALA: Ulipewa chakula Tazara muda gani?
SHAHIDI: Chakula cha mchana cha mahabusu wote, ugali na mboga za majani.
KIBATALA: Mwambie Mheshimiwa Jaji kama wakati wote ulipokuwa Moshi ulipewa chakula.
SHAHIDI: Hapana. Sikupewa chakula.
KIBATALA: Wanasema mlipokuwa Himo baada ya gari kuharibika mkala chakula na kuja Dar es Salaam. Je, kwa kumbukumbu zako mlikula chakula Himo?
SHAHIDI: Hapana.
KIBATALA: Je, unakumbuka kama ulibadilisha na kupanda gari nyingine?
SHAHIDI: Sikumbuki. Nakumbuka baada ya kutoka Moshi nilikuja kushuka baada ya kufika Dar es Salaam.
KIBATALA: Unasema Moshi ulipigwa na kuteswa kama mshikaki au ppo kwenye chuma. Ulipigwa kipigo gani?
SHAHIDI: Nilikuwa napigwa kwenye unyayo na kwenye magoti. Nikiwa miguu juu kichwa chini.
KIBATALA: Zoezi lilichukua muda gani?
SHAHIDI: Ilichukua dakika 45.
KIBATALA: Husianisha kati ya kipigo chako na kwenye nyayo na hilo chuma, na kushindwa kutembea mpaka kurudishwa mahabusu. Ikabidi wakuburuze?
SHAHIDI: Kuna uhusiano. Nilipopigwa miguu ilivimba nikawa nashindwa kukanyaga chini. Nikikanyaga chini miguu inakuwa inauma kama nimepigwa shoti.
KIBATALA: Kupigwa kuna uhusiano gani na kupoteza fahamu kwenda kwenye ubongo?
SHAHIDI: Kupigwa kwenye unanyo ni torture. Unayasikia maumivu kutoka kwenye miguu mpaka kichwani.
KIBATALA: Hapa kuna maelezo ambayo ni kielelezo. Nataka kujua kweli ulisaini maelezo yako.
SHAHIDI: Nilishasema mwanzo kuwa nilialetiwa (alert) tangu mwanz kuwa endapo nitakwenda kinyume nitakuwa nayatafuta mengine. Kwa kuwa nilishakuwa nimeteswa sana ikabidi kukubaliana nao.
KIBATALA: Unasema suruali uliyovaa leo ndiyo suruali uliyovaa Agosti tano ambayo haina hooks. Je, dhumuni lako lilikuwa kuja kuonyesha Mahakama?
SHAHIDI: Hapana. Kwa sababu leo sikuwa nimejiandaa kuja kutoa ushahidi. Wala sikutegemea kuwa leo nitatoa ushahidi.
KIBATALA: Kwani kwa unavyojua upande wa Mashitaka watakuwa na mashahidi wangapi?
SHAHIDI: Mashahidi saba.
KIBATALA: Leo ulitegemea nini?
SHAHIDI: Waendelee kutoa ushahidi.
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji ni hayo tu.
JAJI: Upande wa Mashitaka?
WAKILI WA SERIKALI: Unaitwa nani? Adam Hassa Kasekwa?
SHAHIDI: Naitwa Adam Hassan Kasekwa na pia kama nilivyomwambia Jaji.
WAKILI WA SERIKALI: Ulikuwa unafanya kazi gani?
SHAHIDI: Ni mwanajeshi. Komandoo.
WAKILI WA SERIKALI: Wewe ni Komandoo mahiri sana?
SHAHIDI: Komandoo. Mahiri gani?
WAKILI WA SERIKALI: Umahiri wa ujuzi.
SHAHIDI: Ndiyo.
WAKILI WA SERIKALI: Umesema ulikuwa VIP Protection?
SHAHIDI: Ndiyo.
WAKILI WA SERIKALI: Ulikuwa unaajiriwa kwenda vitani?
SHAHIDI: Hapana. Niliajiriwa kwenda kumlinda Mbowe.
WAKILI MALLYA: Objection! Mheshimiwa Jaji naomba distance kati ya wakili na mteja wangu kwa sababu za kiafya. Akae mbali kidogo. Wakili amevua barakoa makusudi.
JAJI: Kwa sababu za kiafya kaa mbali.
WAKILI WA SERIKALI: Kwa kuwa wewe ni komandoo uliyefuzu, miongoni mwa mafunzo uliyofuzu ni kuvumilia hali ya mateso?
SHAHIDI: Ndiyo. Na ndiyo maana unaniona hapa.
WAKILI WA SERIKALI: Makomandoo ni watu sio legelege. Ni watu wenye kuhimili shida na mazingira watakayokuumbana nayo.
SHAHIDI: Ndiyo.
WAKILI WA SERIKALI: Kwa kuwa makomandoo ni watu wanaohimili shida, ni nadra kumkuta komandoo analalamika.
SHAHIDI: Si Kweli
JAJI: Wakili hebu rudia swali. Unaposema hali ngumu, hali ngumu ni hali ngumu ya maisha, fedha au mateso?
WAKILI WA SERIKALI: Kwa kuwa mni watu wanaohimili shida ni nadra kumkuta komandoo analalamika.
SHAHIDI: Nimekwambia ndiyo. Kwa sababu makomandoo na wao ni wanadamu.
WAKILI WA SERIKALI: Kwa hiyo unataka kuiambia Mahakama kwamba makomandoo si wastahimilivu?
SHAHIDI: Ndiyo.
WAKILI WA SERIKALI: Katika mafunzo ya ukomandoo ulifuzu kukaa na njaa kwa muda mrefu?
SHAHIDI: Ndiyo.
WAKILI WA SERIKALI: Hatutegemei kusikia unalalamika kukaa njaa kwa muda wa siku mbili.
SHAHIDI: Si kweli.
WAKILI WA SERIKALI: Nikweli kwamba…..
MALLYA: Objection! Kama nimekuelewa ruling yako ya maswali kuanza ni kweli ilikuwa inatuhusu wote.
WAKILI WA SERIKALI: Unakumbukumbu nzuri sana?
SHAHIDI: Ndiyo. Kabisa?
WAKILI WA SERIKALI: Ulikuwa unakumbuka mlolongo wa kesi vizuri sana?
SHAHIDI: Ndiyo. Sahihi kabisa.
WAKILI WA SERIKALI: Yaliyojiri Kule Moshi na kule Mbweni ulimueleza wakili wako kabla kesi haijaanza.
SHAHIDI: Si kweli.
JAJI: Subiri kidogo. Shahidi ukiona kichwa kinapata moto unaweza kuomba maji. Naona unayo. Uongezewe maji mengine?
SHAHIDI: Ndiyo. Niongezewe Mheshimiwa.
WAKILI WA SERIKALI: Kwamba mpaka kesi inaanza ulikuwa hujamwambia wakili wako kuhusu yaliyotokea Moshi mpaka tarehe tisa Mbweni?
SHAHIDI: Sijamwambia.
WAKILI WA SERIKALI: Ulimweleza wakati gani?
SHAHIDI: Wakati kesi inatolewa Kisutu.
WAKILI WA SERIKALI: Kuanzia siku Ramadhani Kingai anatoa ushahidi mpaka leo hii unatoa ushahidi wako wakili wako alikuwa anafahamu mambo yaliyokusibu?
SHAHIDI: Sahihi kabisa.
WAKILI WA SERIKALI: Ulishawahi kutuhumiwa makosa ya utovu wa nidhamu ukiwa jeshini?
SHAHIDI: Hapana.
WAKILI WA SERIKALI: Ulipokuwa jeshini wakati wa Misheni DRC unazitambua kamati za kinidhamu zilizopo jeshini?
SHAHIDI: Ndiyo.
WAKILI WA SERIKALI: Unapotuhumiwa Kwa jambo lolote unatakiwa kupewa haki ya kusikilizwa?
SHAHIDI: Ni haki. Ndiyo.
WAKILI WA SERIKALI: Lengo kule Jeshini wakikutuhumu wakakupeleka kwenye kamati, kwanini wewe lazima uwepo?
SHAHIDI: Unapoitwa kwenye jambo kama hilo, wanataka kujua kutoka upande wako.
WAKILI WA SERIKALI: Usipoitwa utakuwa umenyimwa haki?
SHAHIDI: Ndiyo.
WAKILI WA SERIKALI: Kwa hiyo haifai kumtuhumu mtu wakati haupo?
SHAHIDI: Ndiyo.
WAKILI WA SERIKALI: Hata wewe huwezi kukubali tunazungumza maneno dhidi yako, Kasekwa kafanya 1, 2, 3, 4, 5 wakati wewe haupo.
SHAHIDI: Hilo mimi siwezi kulijibia. Inategemea hao wenyewe.
WAKILI WA SERIKALI: Wewe kazi yako ni kujibu. Lazima ujibu.
JAJI: Msijibizane wenyewe kwa wenyewe huko. Ni vyema wakili kuangalia kama nimemaliza kuandika.
WAKILI WA SERIKALI: Mimi nataka kujua jambo dogo tu. Kitendo kikifanyika dhidi yako halafu watu wakakaa wenyewe bila wewe kuwepo, je, ni haki?
SHAHIDI: Ni sahihi.
WAKILI WA SERIKALI: Kama hali ipo hivyo kama usilopenda kufanyiwa wewe usimfanyie mwenzako. Kingai wakati anatoa ushahidi wake wakati wanakukamata wewe siku ya tarehe tano Rau Madukani, kwamba walipokukamata walikupekua na wakakuta na kete 58 za mya kulevya aina ya Heroine na wakakukuta pistol.
SHAHIDI: Ndiyo alivyoeleza. Unayarudia yote?
WAKILI WA SERIKALI: Usilete kujua sana.
WAKILI MALLYA: Objection! Meneno hayo “kujua sana” yana lengo la kumtoa shahidi wangu nje ya lengo.
JAJI: Maneno hayo ya “kujua sana” nafikiri yasirudiwe tena hapa.
WAKILI WA SERIKALI: Wakati wa ushahidi wa Kingai alieleza kwamba alikuandikisha maelezo na akaita mashahidi wawili wanawake wakati wa upekuzi.
SHAHIDI: Ndiyo. Alieleza.
WAKILI WA SERIKALI: Kingai hakueleza suala lolote la kuhusu kukupiga.
SHAHIDI: Ni sahihi.
WAKILI WA SERIKALI: Wakili wako hakumweleza Kingai kuwa wewe Kingai ulimuwekea madawa ya kulevya na pistol.
MALLYA: Objection! Wakili anauliza mambo ambayo mimi na mteja tulikuwa tunaongea.
JAJI: Upande wa mashitaka unaweza kujibu.
WAKILI WA SERIKALI: Nilichomuuliza kuhusu kutoka Moshi mpaka hapa siyo jambo la siri. Nimeuliza kwamba Kingai hakuhojiwa unayoyaleta leo.
JAJI: Sijaona tatizo katika namna ambayo wakili wa Serikali amemuuliza shahidi.
WAKILI WA SERIKALI: Shahidi narejea tena maneno yangu.
Adhana msikitini inialia. Mahakama imesimama kidogo.
JAJI: Tunaweza kuendelea.
WAKILI WA SERIKALI: Kingai wakati anatoa ushahidi wake hapa hakuulizwa suala lolote kuhusiana kukutilia wewe madawa ya kulevya na kukuwekea wewe pistol na siku ile walikupiga eneo lile la Rau Madukani.
SHAHIDI: Sivyo.
WAKILI WA SERIKALI: Kwa hiyo hali ilikuwaje?
SHAHIDI: Aliulizwa na Wakili Kibatala.
WAKILI WA SERIKALI: Kingai anasema wakati wana kukamata uliwapa ushirikiano. Wakafanya walichofanya. Si ndivyo walivyosema?
SHAHIDI: Sijaelewa.
MALLYA: Maneno ya “kweli au si kweli” ulishayatolea mwongozo.
JAJI: Nadhani nimeweka bayana yasitumike mwanzoni. Inakuwa kama maigizo, ila mwishoni yanaweza kutumika.
WAKILI WA SERIKALI: Leo hii ndiyo mara ya kwanza Mahakama hii inaelezwa kuwa wakati unakamatwa palikuwa na hali ya vurumai, madawa yakawekwa kiunoni kwako, pistol ikawekwa kiunoni kwako na wewe pia ulipigwa.
SHAHIDI: Si kweli. Niliskia hapa. Ingawa mimi siyo mwanasheria hayo yaliulizwa.
WAKILI WA SERIKALI: Maneno haya ni sawa na kusema kukamatwa na kupigwa ni kinyume na sheria na vile vile na kitendo cha kupigwa ni kinyume cha sheria.
SHAHIDI: Sijakuelewa.
SHAHIDI: Umepigwa na kukamatwa umekamatwa na ukapigwa?
JAJI: Adamoo uko sawa?
SHAHIDI: Nipo timamu Mheshimiwa Jaji.
JAJI: Mallya?
MALLYA: Shahidi yupo sawasawa.
WAKILI WA SERIKALI: Namwambia mtu kitendo cha kukamata na kumpiga mtu ni kinyume na sheria, na huyo bwana akasema ni kweli sheria haziruhusu kumpiga mtu wakati unamkamata. Swali linakuja, kitendo cha kumwambia kukamatwa na kupigwa ni kinyume na sheria ni vitendo tofauti.
SHAHIDI: Vinaoana.
JAJI: Wakili usiweke story ndefu sana. Uliza maswali direct. Usizunguke sana. Mtaulizana maswali mpaka asubuhi na bado sitaelewa. Go straight.
WAKILI WA SERIKALI: Kitendo cha kukiuka utaratibu na kusema ni kitendo.
SHAHIDI: Hakuna tofauti hapo.
WAKILI WA SERIKALI: Kingai kasema mlipofika kituoni mkawashusha akina mama mkarudi mitaani kumtafuta Moses Lijenje.
SHAHIDI: Ndivyo alivyoeleza.
WAKILI WA SERIKALI: Kingai akasema kuwa baadaye wakawarudisha kituoni baada ya kumkosa Moses Lijenje.
SHAHIDI: Ndivyo alivyoeleza.
WAKILI WA SERIKALI: Ni kweli kuwa Kingai hakuhojiwa kuwa alikuwa anadanganya isipokuwa mlipofika kituoni mkaenda kuteswa? Hili suala hakuhojiwa?
SHAHIDI: Sijakuelewa. Kuhojiwa na nani?
WAKILI WA SERIKALI: Wakati mnamuuliza Kingai maswali kama haya ya dodoso.
JAJI: Nafikiri kuna tatizo hapa. Na hali haijabadilika. Bado wakili unaweka explanations. Ndiyo maana kila wakati anarudi kusema rudia swali sijakuelewa.
Mahakama imetulia.
Jaji anavuna ukimya.
JAJI: Mkishindwa kueleza nitasema tuje Jumatatu.
WAKILI WA SERIKALI: Kwanini maswali mengi ninayokuuliza hutaki kujibu?
SHAHIDI: Mlolongo mreeeeefu na swali halijukikani lipo wapi.
WAKILI WA SERIKALI: Wakati Kingai anahojiwa hakuulizwa kuhusu wewe kuteswa.
SHAHIDI: Si kweli. Alihojiwa.
WAKILI WA SERIKALI: Umeleeza Kuwa walikutesa wakawa wanakuchoma na bisibisi matakoni na tumboni.
SHAHIDI: Kweli.
WAKILI WA SERIKALI: Kwa hiyo baada ya kuchomwa na bisibisi ulitokwa na damu nyingi sana.
SHAHIDI: Si kweli
WAKILI WA SERIKALI: Kwa kuwa hukutokwa na damu nyingi, majeraha yalikuwa madogo sana.
SHAHIDI: Sahihi.
WAKILI WA SERIKALI: Kama majeraha haya yalikuwa madogo, uliweza kuyavumilia.
SHAHIDI: Sahihi.
WAKILI WA SERIKALI: Utakubaliana na mimi kwamba majereha hayo madogo ambayo uliyavumilia hayakuwa kitu kikubwa.
SHAHIDI: Yalikuwa kitu kikubwa ndiyo maana nimeiambia Mahakama.
WAKILI WA SERIKALI: Mwanzo ulisema kitu kilichokufanya majeraha yalikuwa madogo. Sababu ya kuvumilia ilikuwa sababu hayakutoa damu au Kwa sababu ya mazingira?
MALLYA: Objection! Kum- harass shahidi kwa jambo ambalo shahidi ameshajibu ni kupoteza muda wa Mahakama.
WAKILI WA SERIKALI: Sawasawa Mheshimiwa.
WAKILI WA SERIKALI: Kwa sababu majeraha yale hayakutoa damu, hayakuweka vidonda kwenye matako yako.
SHAHIDI: Sahihi.
WAKILI WA SERIKALI: Ulichomwa sana bisibisi kwenye matako yako. Damu haikutoka na majeraha hayakutoka. Je, ni kweli au si kweli?
SHAHIDI: Kweli.
JAJI: Ndiyo.
WAKILI WA SERIKALI: Kwa ruhusa yako naomba tushauriane hapa.
JAJI: Sawa na ukirudi tumalize juu ya bisibisi za matako.
WAKILI WA SERIKALI: Nimeshamaliza Mheshimiwa Jaji.
Kimya kinatawala kidogo.
WAKILI WA SERIKALI: Wale waliokuwa wamekuzingira na kukufanyia uhalifu tarehe tano hakuna hata mmoja uliweza kumtambua?
SHAHIDI: Ni kweli. Kabla ya pale sikuwa namfahamu hata mtu mmoja pale.
WAKILI WA SERIKALI: Hukuwahi kuwaona kabla ya hapo?
SHAHIDI: Ni sahihi.
WAKILI WA SERIKALI: Kabla ya hapo hukiwahi kugombana, kurushiana maneno kwa namna yoyote ambayo inaweza kuleta chuki?
SHAHIDI: Sahihi.
WAKILI WA SERIKALI: Hukuwahi kuwa na kinyongo nao kabla ya wakati ule?
SHAHIDI: Sahihi kabisa.
WAKILI WA SERIKALI: Watu hawa licha ya kuwa huna kinyongo nao, walikuja kukufanyia ubaya?
SHAHIDI: Ndiyo.
WAKILI WA SERIKALI: Hakika hali hii ni ya kustaajabisha sana.
MALLYA: Objection! Maneno hayo anayotumia wakili anajaribu kumlisha shahidi maneno kabla ya swali.
JAJI: Nafikiri shahidi mwenyewe anaweza kujibu.
WAKILI WA SERIKALI: Ni hali ya kustaajabisha. Kweli au si kweli?
SHAHIDI: Ni kweli.
WAKILI WA SERIKALI: Watu waliokuvamia siku ile, ukiachia Ramadhani Kingai na Mahita, wengine wote huwakumbuki wala huwafahamu?
SHAHIDI: Si kweli.
WAKILI WA SERIKALI: Kwa hiyo wote unawakumbuka na kuwafahamu?
SHAHIDI: Si wote.
WAKILI WA SERIKALI: Ieleze Mahakama kuanzia siku ile wanakukamata Rau Madukani tarehe tano mwezi wa nane mpaka tarehe saba mwezi wa nane hukuwa unawafahamu majina yao, ndiyo maana umekuja kuwafahamu hapa akina Ramadhani Kingai kwa sababu hakukwambia majina yao.
SHAHIDI: Sahihi kabisa.
(Kimya kidogo kimetawala wakati upande wa Serikali wakishauriana. Kisha Jaji anavunja ukimya).
JAJI: Nafikiri inatosha kwa leo. Ni saa 10:30inakaribia sasa. Siku ya Jumatatu tunaweza kuendelea
JAJI: Upande wa utetezi mnasemaje?
KIBATALA: Tutakuwa na nafasi.
WAKILI WA SERIKALI: Tutakuwa na nafasi Mheshimiwa.
Jaji anaandika halafu anauliza, “tutakuwa na shahidi mwingine upande wa utetezi”?
MALLYA: Ni mshitakiwa.
JAJI: Naahirisha kesi mpaka Jumatatu kwa sababu ya muda umekuwa changamoto. Natarajia tutaanza saa tatu … Mpaka hiyo Jumatatu, nawashukuru mawakili wa pande zote pamoja na kuvutana. Nawashukuru wote wanaotumia muda wao kufuatilia shauri hili.
Jaji anaondoka mahakamani.