Katika usiri wa madini, Magufuli hana tofauti na Mkapa wala Kikwete

TUNDU Lissu, mbunge wa Singida Mashariki ambaye anaendelea na matibabu katika University Hospital Leuven, Ubelgiji, anasema kuwa licha ya mbwembwe za Rais John Magufuli kuhusu “mabadiliko” anayodai kufanya katika sekta ya madini, usiri unaoendekezwa sasa ni sawa na ule ule wa watangulizi wake, unaopaswa kutiliwa shaka. Endelea.

Nimemsikia Waziri wa Sheria na Katiba, Dr. Palamagamba Kabudi akiliambia Bunge kwamba Serikali ya Rais John Magufuli haitatoa hadharani, na kwa hiyo Bungeni, taarifa zinazohusu fedha tulizolipwa na makampuni ya kigeni ya madini. Serikali ya Magufuli inahofu kwamba fedha hizo zikitangazwa hadharani basi wadai wetu mbali mbali watatufungulia kesi nyingi za madai, kwa sababu watajua sasa tuna fedha. Aidha, fedha hizo hazitalipwa kama maduhuli ya Wizara ya Madini. Maana yake ni kwamba taarifa ya mapato na matumizi ya Wizara ya Madini inayotolewa Bungeni kila mwaka, haitaonyesha mapato yanayotokana na madini.

Kwenye suala hili na kwa kauli hii ya Waziri Kabudi, sasa ni wazi kwamba Serikali ya Magufuli haina tofauti yoyote ya kimsingi, na pengine ni ya hovyo zaidi ukilinganisha, na Serikali za watangulizi wake, Rais Jakaya Kikwete na Ben Mkapa. Nitafafanua.

1. Usiri ulitawala masuala yote ya leseni, mikataba na malipo serikalini yaliyotokana na uchimbaji madini wakati wote wa tawala za Kikwete na Mkapa. Bunge lilinyimwa kuangalia na kuchunguza mikataba ya madini kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kikatiba ya kuisimamia na kuishauri Serikali.

2. Usiri huu ulitengeneza mazingira yaliyozaa mikataba mibovu na ufisadi mkubwa katika sekta ya madini, ulioligharimu taifa letu mabilioni ya fedha za kigeni.

3. Kwa kauli ya Prof. Kabudi, usiri huu sio tu utaendelea, bali sasa utakuwa mkubwa zaidi kwa sababu leseni za uchimbaji madini zitatolewa na Baraza la Mawaziri, badala ya watendaji wa serikali. Kama inavyojulikana, majadiliano na maamuzi ya Baraza la Mawaziri ni siri kwa mujibu wa sheria zetu na Mawaziri wote hula kiapo cha kutunza siri hizo.

4. Usiri uliotangazwa na Prof. Kabudi unavunja wazi wazi Sheria za Rasilmali za Nchi zilizopitishwa kwa mbwembwe kubwa na majidai mengi Bungeni mwaka jana. Mpiga Mbwembwe Mkuu alikuwa Prof. Kabudi mwenyewe.

(a) Kifungu cha 12 cha Sheria ya Milki ya Kudumu ya Utajiri na Rasilmali za Asilia ya 2017 kinaruhusu Bunge kupitia mikataba yote inayohusu uchimbaji (extraction), utumiaji (exploitation) au upataji (acquisition) wa utajiri na rasilmali asilia kupitiwa na Bunge. Sasa, kwa kauli ya Prof. Kabudi, haitawezekana tena kwa Bunge kuipitia mikataba hiyo na hivyo kuiweka hadharani kwa wananchi.

(b) Wakati Prof. Kabudi amedai bungeni kwamba itakuwa ni marufuku kwa Serikali kuingia mikataba ya uendelezaji madini (Mineral Development Agreements – MDAs) kwa sababu mikataba hiyo imetuletea matatizo mengi sana, vifungu vyote muhimu vya Sheria ya Milki ya Kudumu ya Utajiri na Rasilmali Asilia vinahusu utaratibu wa ‘mikataba’ ya utajiri na rasilmali asilia, ikiwemo madini. Angalia tafsiri ya maneno ‘arrangements or agreement’ katika kifungu cha 3. Vifungu vingine husika vinavyohusika na mikataba ni 5(4), 6, 7, 8, 9, 10(1), 11(3) na 12.

(c) Ni sahihi, kwa hiyo, kusema kwamba Sheria ya Milki ya Kudumu ya Utajiri na Rasilmali Asilia imeweka utaratibu mpya wa ‘mikataba’, wakati Prof. Kabudi na wanafunzi wake wa sheria – Naibu Spika Tulia na Mwanasheria Mkuu Kilangi – wanadai bungeni kwamba kuanzia sasa ni marufuku kuingia mikataba ya uendelezaji madini. Heri wale ambao hawakufundishwa na wabobezi hawa wa sheria!!!

(d) Kifungu cha 5(2) cha Sheria hii kinasema kwamba “utajiri na rasilmali asilia zitashikiliwa na Rais kama dhamana kwa niaba ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano.” Haya pia ni masharti ya kifungu kipya cha 5(1) cha Sheria ya Madini kama ilivyorekebishwa mwaka jana.

(e) Ukiachia Sheria ya Ardhi ya 1999, hii ni mara ya kwanza kwa Rais wa Tanzania kujitwalia kisheria umiliki wa utajiri na rasilmali asilia zote za nchi yetu, ikiwemo madini. Ukijumlisha na kauli kwamba sasa leseni zote za madini na, by extension, utajiri na rasilmali asilia nyingine zote zitatolewa na Baraza la Mawaziri, sasa madili yote ya kifisadi yatahamia Ikulu ya Magufuli na hatutayajua, kwa sababu tukiyajua wadai wetu watatushtaki mahakamani!!!

(f) Utaratibu huu wa kifisadi kwenye masuala ya rasilmali asilia za nchi yetu haukuwepo kabisa wakati wa Kikwete na Mkapa, ambao ndio wanaowajibika kwa kiasi kikubwa na hali aliyoikuta Magufuli alipoingia madarakani.

5. Msimamo wa sasa wa Serikali ya Magufuli unakinzana moja kwa moja na matakwa ya Sheria ya Kupitiwa na Kujadiliwa Upya kwa Masharti Yasiyofaa ya Mikataba ya Utajiri na Rasilmali Asilia ya 2017 (The Natural Wealth and Resources Contracts (Review na Re-Negotiation of Unconscionable Terms) Act, 2017).

(a) Wakati Prof. Kabudi amesema bungeni kwamba itakuwa ni marufuku kwa Serikali kuingia mikataba ya uendelezaji madini, Sheria hii yote inahusu kupitiwa na kujadiliwa upya kwa mikataba iliyopo sasa.

(b) Wakati Prof. Kabudi na Serikali ya Magufuli haitaki mikataba hii na fedha zinazopatikana kwa mujibu wake zijulikane kwa wananchi kupitia kwa wabunge wao, kifungu cha 4(1) cha Sheria hiyo kinasema: “Kwa ajili ya utekelezaji kwa ufanisi wa kazi zake za usimamizi na ushauri zilizotajwa chini ya ibara ya 63(2) ya Katiba, Bunge linaweza kupitia taratibu zozote au makubaliano yaliyoingiwa na Serikali kuhusiana na utajiri na rasilmali asilia.”

(c) Kifungu cha 5(1) kinaitaka Serikali kupeleka Bungeni mikataba yote ya utajiri na rasilmali asilia iliyoingiwa na Serikali ndani ya siku sita za Mkutano wa Bunge unaofuata kuingiwa kwa mikataba hiyo.

(d) Kwa vile Prof. Kabudi amekiri kwamba Serikali imekwishaingia makubaliano ya msingi na Barrick Gold kuhusu makinikia ya Bulyanhulu na Buzwagi; na pia na Tanzanite One kuhusiana na tanzanite ya Mererani, Serikali inawajibika kisheria, na wabunge wanatakiwa kudai, kuwasilishwa mikataba hiyo Bungeni katika Mkutano huu wa Bunge, ili Bunge liweze kuipitia na, ikihitajika, kuishauri Serikali kuanzisha majadiliano mapya kuhusu mikataba hiyo, kama inavyotakiwa na vifungu vya 5(2) na (3) vya Sheria hiyo.

Kutofanya hivyo ni kuendeleza ufisadi na usanii ule ule wa miaka ya Kikwete na Mkapa ambao Magufuli anajidai kuwa anapambana nao.

6. Prof. Kabudi amesema bungeni kwamba kuanzia sasa leseni zote za uchimbaji madini zitatolewa na Baraza la Mawaziri. Kama kawaida yake, Waziri huyu msomi anapotosha wabunge au anafanya maandalizi ya kukiuka sheria alizoziwasilisha bungeni yeye mwenyewe na mbwembwe nyingi na madaha makubwa.

(a) Baraza la Mawaziri halijatajwa mahali popote katika Sheria ya Madini kama ilivyorekebishwa mwaka jana. Badala yake, wajibu wa kutoa leseni zote za uchimbaji madini umekabidhiwa kwa Tume ya Madini, kwa usimamizi wa Waziri wa Madini. Angalia kifungu kipya cha 19(f) cha Sheria ya Madini.

(b)Tume ya Madini ndiyo uwezo wa kusimamisha au kufuta kabisa leseni yoyote ya madini. Angalia kifungu kipya cha 24(m) cha Sheria ya Madini. Itakuwa maajabu ya Tanzania kwa Tume iliyoteuliwa na Rais kufuta leseni iliyotolewa na Baraza la Mawaziri linaloongozwa na Rais.

Haya ndiyo ya Magufuli na watu wake wanaojifanya kwa wananchi kuwa ndio watetezi wa madini na rasilmali asilia za nchi yetu.

Ni usanii mtupu. Ni ukiukaji mtupu wa sheria walizozipitisha wenyewe na wanazozipigia debe kila kukicha. Ni maandalizi ya ufisadi mkubwa zaidi; au mwendelezo wa ufisadi wa miaka ya Kikwete na Mkapa. Waheshimiwa wabunge na Watanzania wanatakiwa kuyaelewa haya na kuyachukulia hatua.

Like
1
1 Comment
  1. Mtanzania 6 years ago
    Reply

    Prof .Kabuli siyo mtu wakuaminika. Huwa anajaribu kugeuza sheria kwa faida ya rais. Huwa anageuka kufutana na upepo. Analinda maslahi tu, siyo msema ukweli.

    1

    0

Leave a Comment

Your email address will not be published.