Katika hili la kiwanda cha maziwa, Magufuli atakabwa na mgogoro wa maslahi. Apewa ng’ombe, bado “mke wa Kinyarwanda.”

President John Magufuli - File photo

WIKI hii Rais John Pombe Magufuli (JPM) yuko Mkoani Kagera. Alianzia Bukoba na sasa yuko mapumzikoni “nyumbani” kwake kwingine, Karagwe.

Ziara hii imeibua mengi na itaendelea kuibua mengine, hata kama umma hauwezi kuyajua yote kwa sababu ya kitanzi ambacho serikali imeviwekea cha vyombo vya habari, na kutokana na hofu iliyotanda kila sekta. Watu hawasemi wazi lakini wapo wanaojua ukweli wa mambo.

Jumapili iliyopita, akiwa njiani kwenda Bukoba, Magufuli “alimtumbua” Kigogo mmoja wa wizara ya ardhi – Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Matumizi ya Ardhi, Dk Steven Nindi. Sababu hazikutajwa, lakini baadhi ya maofisa wake walio katika msafara wanadai alifanya kosa la kusita kutekeleza amri za rais zinazokiuka sheria na taratibu. Alikuwa amemuagiza abadili umiliki wa ardhi ya Ihungo sekondari kutoka Kanisa Katoliki kwenda serikalini.

Tangu shule ilipotaifishwa miaka ya 1970, hati miliki ilibaki kanisani na imekuwa inalipiwa na kanisa kila mwaka. Marais wanne waliotangulia waliheshimu hilo. Nindi alikuwa tayari kutekeleza amri ya rais lakini alitaka kufuata njia halali ya kubadili umiliki huu. Alitaka kufuata kanuni, akatumbuliwa.

Rais Magufuli hakutaka kuzindua shule ikiwa katika umiliki wa Kanisa Katoliki. Mmoja wa wateule wake katika wizara ya ardhi amehoji: Mbona aliidhinisha fedha za ukarabati bila kubadili hati?”

Baada ya uzinduzi wa shule JPM alielekea Karagwe. Huko aliweka jiwe la msingi la kiwanda cha maziwa cha mwekezaji wa ndani aitwaye Joswam Ntangeki. Kiwanda kinadaiwa kugharimu tsh 4.5 bilioni zinazodaiwa kutolewa kama mkopo kutoka Benki ya Kilimo.

Katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi, JPM alifanya mambo kadhaa yaliyoibua hisia za mgongano wa maslahi.

Kumekuwa na uvumi mwingi hapo Kijijini Kihanga kuwa kiwanda hicho ni mali ya JPM. Mara kadhaa tangu maandalizi ya ujenzi wa kiwanda hicho yaanze, JPM na wasaidizi wake wamekuwa wakifika hapo “saiti” kukagua maendeleo ya mradi.

Hata baadhi ya walalamikaji waliochukuliwa ardhi zao, walitishwa kwa maelezo kuwa “wanapambana na rais”. Wengi wao walinywea baada ya kuambiwa hilo. Baada ya uvumi juu ya rais kuzidi, ndipo Josam Ntangeki alipojitokeza kwa jina la Kampuni ya Kahama Fresh Milk.

Taarifa zisizo rasmi kutoka Benki ya Kilimo zinadai kuwa mkopo kwa Ntangeki ulikuwa unashughulikiwa na kusukumwa na maofisa wa Ikulu wakiongozwa na mmoja aliyehamishiwa Mtwara siku za karibuni. Jana wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi, Mtendaji Mkuu wa Benki ya Kilimo alikuwepo.

Josam Ntangeki, siku za nyuma, alikuwa mkandarasi wa barabara Mkoani Kagera na Geita na kazi hiyo ndiyo ilimuweka karibu na JPM. Ili kuficha umma usijue wanavyofahamiana, Ntangeki alimpa JPM zawadi ya ng’ombe wanne, na JPM amewapokea Jumatano asubuhi. JPM yuko kwenye shamba lake la mifugo (ranch) akiendelea na mapumziko huko huko Karagwe.

Jambo jingine lililojitokeza lilihusu umoja wa wafugaji kutoka Kahama na Karagwe. JPM aliwatetea kwa nguvu zote akisema kwanza wote ni wana CCM na kwamba wameonewa sana na serikali zilizopita.

Kwa kuwa JPM naye amekuwa mfugaji sasa na ameamua kuwa na makazi Karagwe, alitumia fursa hii kutamka rasmi kuwa yeye ni mfugaji na anaishi Karagwe. Akatoa maagizo rasmi kwa NARCO na wizara ya mifugo kuchukua hatua zitakazowanufaisha wafugaji, akiwamo yeye. Akamwagiza Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa, awashirikishe wabunge wengine kutetea wafugaji hao.

Waliohudhuria hafla hiyo walishangaa kuona wafugaji waliosimama wengi wao ni raia wa Rwanda.

Siku za karibuni tangu JPM aanze kufugia Karagwe, raia hawa wa Rwanda wamekuwa wakichanga mifugo na kuipeleka zizini kwake. Jumanne usiku maafisa kadhaa walio katika msafara wa JPM walikutana na wafugaji hao katika hotel moja iliyo mjini Kayanga na kuwahakikishia ulinzi wao na mifugo yao.

Mwenyekiti wao, ambaye ni kada maarufu wa CCM, amewaambia wenzake leo Jumatano mchana wakiwa katika benki ya CRDB walipokutana na Kigogo mmoja wa polisi aliye kwenye msafara kuwa mipango imeiva ya kumpatia JPM “mke wa Kinyarwanda.” Huu waweza kuwa utani lakini unabeba ujumbe mzito.

Wakati wa awamu ya tatu, Rais Benjamin Mkapa alimfukuza kazi aliyekuwa DC wa Karagwe Kapteni Nditi baada ya kupewa mke wa Kinyarwanda na ng’ombe wengi ili asiwabughudhi. Baadaye alikuja DC Ole Saningo Telele ambaye naye alipewa ng’ombe wengi na kuishia kuongozwa na Wanyarwanda.

DC wa sasa amekwepa mtego wa wanawake wa Kinyarwanda lakini anamiliki mamia ya ng’ombe huko Misenyi. Serikali ya JPM imevunja rekodi kwa kuwateua raia wa Kinyarwanda katika ngazi za juu tangu tupate Uhuru.

Wiki iliyopita ng’ombe kadhaa wa JPM waliibiwa toka ranchi yake na baadhi yake wanasemekana kuelekea Misenyi. Msako mkali unaendelea kuwatafuta lakini vyombo vya dola wilayani vimedai wahusika wanajulikana.

Rais JPM ameonekana asubuhi jumatano akiwa anakamua maziwa zizini kwake Karagwe wakati magari ya maafisa wake yanarandaranda kikao kona.

Katika mkutano hadhara, JPM alimchimba mkwara Mhandisi Mkazi wa Mkoa kuhusu ujenzi wa darasa la kuunganisha Karagwe na Misenyi. Baadaye JPM alijikuta akitoboa siri alipotamka kuwa naye anatokea Chato na ni jirani yake. Baadaye walikutana usiku nyumbani kwake na JPM akamtuliza kuwa ulikuwa mkwara.

Anayoyafanya JPM Wilayani Karagwe hayana tofauti na aliyoyafanya hayati Mkapa kule Kiwira, Kilombero na benki ya AMBEN ambayo yalimtia msukosuko baada ya kustaafu.

Mmoja wa mawaziri wake walio kwenye msafara amewaona wawekezaji kivuli hao wawe makini maana JPM hataishi Ikulu milele.

“Hata kama amezuia taarifa za mali za Viongozi kuwa wazi na kutoziweka mtandaoni, lakini ujue hawa hawa wanaotumwa na kujituma ndio watakaogeuka na kujipendekeza kwa Rais ajaye kwa kumpa siri zote”, alisema waziri huyo aliyeondoka na kurejea Bukoba baada ya tukio.

Like
6