ITHIBATI NA PRESS CARD: PACHA AU PACHANGA?

Ndimara Tegambwage

TUSEMEZANE. Kitambulisho au Press Card anayobeba mwandishi wa habari, haina uwezo wa kumpa au kumwongezea elimu, maarifa wala stadi.

Tuseme hivi: Hiki ni kitambulisho tu. Hakina hata uwezo wa kukamilisha, kuongeza au hata kupunguza sifa za mwandishi wa habari. Ni kwa ajili ya kutambulishwa na kutambulika.

Bali mara hii, hupewi Press Card mpaka uwe walau na diploma ya/katika Uandishi wa Habari. Nadhani wahusika watataka na wataweza kuthibitisha ni kutoka chuo gani; na iwapo chuo hicho – ndani au nje ya nchi – kimesajiliwa rasmi na kina hadhi ya kutoa elimu ya uandishi wa habari.

Tuje kwenye Ithibati. Anayethibitisha kuwa unastahili kupewa Press Card, ndiye anatoa ITHIBATI – uthibitisho na ruhusa. Hii basi ndiyo maana unasikia Press Card na Ithibati vimekuwa pacha; au muzikidansa – pachanga.

Sasa kuna mpagao. Waliokuwa wakiripoti, wakifukua na kuanika taarifa, wakihariri, wakichambua, wakichora katuni, wakitangaza, wakisimamia programu mbalimbali katika redio na televisheni; waweza kupoteza ajira.

Waliokuwa wakiandika na kuhariri, huku wakilea, kuelekeza na kufunza wenye vyeti, diploma na digrii ambao walijiunga nao; waweza kupoteza sifa kwa kuwa hawana vitambulisho vyenye Ithibati. Na wao hawana Ithibati. Ni kwa kuwa hawana diploma.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Ithibati (JAB), Patrick Kipangula, amekaririwa na DW – Deutsche Welle akisema (sijaona akikanusha), “…tunawashauri kama mtu hana sifa, basi ajitahidi azipate hizo sifa zilizoainishwa kisheria kisha arudi kwenye kazi yake.”

Kwa mpangilio wa maneno, Kipangula ameeleweka: Kwamba anatoa ushauri. Lakini pia, anatoa tangazo la kufukuza kazi wale wasiokuwa na diploma. Kwa kifuatacho baada ya kauli yake, ni kiza tupu.

Katika mazingira ya “chapuchapu.” Yale ya “mwendokasi.” Yale ya “nipe-nikupe.” Ya kukidhi haja. Ya kurudi haraka kuchukua nafasi yako; ninaona diploma inaweza kupatikana; lakini isiyo ya elimu ya “kiwango cha diploma” katika uandishi wa habari.

Ni kiza kwa sababu Kipangula anayesema waende kusaka Diploma kisha kila mmoja “arudi kwenye kazi yake,” hana uwezo wa kulinda ajira za anaowaanua katika mamia ya vyombo vya mawasiliano. Wakati mwingine wanaviita vyombo vya habari, hata kama havifanyi kazi ya habari.

Miongoni mwa wanaoanuliwa kama nafaka wakati wingu likitishia kulia, wamekuwa kazini kwa miaka mitano, kumi, hata ishirini au zaidi. Si kwamba wamekuwa ving`ang`anizi tu. Si kwamba waliwekwa kwa maonesho. Hapana. Wamiliki wa vyombo vyao wanajua, wanathamini uwezo na mtaji wao.

Hao wanaoanuliwa, pamoja na kufanya kazi za uandishi wa habari, wamekuwa wakilea, wakielekeza na kufundisha wanaojiunga na vyombo vyao ambao wanakuja, ama na diploma, digrii au sifa nyingine kitaaluma.

Ni kwa hili, na ndio maana, wamiliki wa vyombo vya mawasiliano, hawajaona umuhimu wa kuwaachia. Utatupaje dhahabu chooni?

Chukua mfano huu. Wewe ni mmiliki wa chombo cha mawasiliano. Unamwacha vipi mwandishi wa habari anayeandika habari na makala zinazopigiwa mfano kwa ubora hata katika vyombo vingine; anayelea, kuelekeza na kufundisha wenzake na “wapya” wanaoingia na wenye sifa za juu za vyuoni hata kuliko yeye? Anayeweka chombo chako sokoni kwa uchambuzi, mahojiano na masimulizi?

Na huyu asingefanya yote haya kama hajifunzi. Maarifa anayowagawia wenzake hayaji kwa sala. Kutakuwepo mito na vijito anamochota ya kwake na yale anayowagawia wengine.

Mfano mwingine. Nani awezaye kuachana na mchora katuni wa kimataifa kwa misingi kuwa hana diploma? Wahaya wanasema, “kanage nkalonde.” Tafsiri ya haraka: “Katupe nikaokote” – huku mdomo ukibinukia pembeni, jicho likilala kwa kengeza la dharau na pua ikituna utadhani inataka kushindana na Sambu – vyote vikitoa msonyo mrefu wa kusuta – mhvyyy!

Kila mmoja anakahitaji. Kila mmoja anajua hata kakikaa nyumbani, katavuna kutoka kokote duniani. Lakini kangekuwa katika chombo cha wasomaji, watazamaji na wasikilizaji; ubunifu wake – mbali na kuchora – ungerutubisha waandishi wengine, wachoraji, chombo kwa jumla, mazingira na wananchi wanaokitumia. Hukaachii hata kwa shuruti.

Kama ilivyo katika mfano wa kwanza hapo juu, wengi wa wanaoanuliwa ni watafutaji, wasakaji, wachimbaji elimu na maarifa; na ndiyo maana wana hazina ya kushiriki na wengine kutoa elimu, maarifa na hekima za wengine; vitabu/mitandao na mazingira.

Tukifika hapa, ndipo tunajiuliza: hivi katika kupata elimu na maarifa kwa walioko kazini, kuna njia moja tu, aina moja tu, mahali pamoja tu na kitu kimoja tu cha kusoma?

Kama wasiokuwa na diploma wameweza kujiendeleza na kufundisha wengine; sasa wao hawawezi kusomea hapo hapo kazini kwao na kufikia viwango vinavyohitajika?

Kuna kitu kinaitwa “life-long learning” – usakaji elimu wa maisha yote. Udugu usioisha kati ya maisha ya mtu na elimu, na maarifa; au taaluma fulani. Elimu inayoendelea au usakaji elimu usiokoma. Hawa wa “miaka mingi” kazini, na waajiri wao bado wanawahitaji; waliishaanza zamani kutekeleza mradi huu binafsi.

Hawa, wala hawapingani na Kipangula. Wanataka mjadala. Je, hawawezi kusomea hapo hapo walipo – huku wanasoma na huku wanafanya kazi? Ni lazima watoke nje ya ajira zao ambazo Kipangula hana uwezo wa kuzilinda/kuzitunza mpaka warejee?

Kwa wanaoandika, ni lazima waache kuandika; kana kwamba wanafanya adhabu kwa kosa walilotenda? Ni kosa lipi? Au wawe wanaandika taarifa na habari na kubandika majina bandia; na lipyoto afanye kazi yake – hatimaye taarifa zivuje kuwa huu ni mradi wa JAB?

Kwenda shule ni muhimu, hata kwa wenye umri mkubwa. Viwango ni muhimu pia. Je, katika hili, wataalamu wa Ithibati waliwahi kufanya, au kufikiria kufanya, tathmini ya elimu, maarifa na stadi; kati ya pande hizi mbili: walimu/wataalamu wasiokuwa na diploma; na wanafunzi wao wenye vyeti, diploma na digrii? Kuna upungufu gani, wapi na kuna kitu gani cha kujifunza? Hii ilipaswa kuwa kabla ya amri za Toka! Toka!

Nani atalea, ataelekeza na kufundisha wanaoingia? Nani atalinda/atatunza nafasi za watakaokwenda “kusaka diploma” mpaka watakaporudi? Nani atakuwa anafanya kazi za wajuzi – kulinda haki na hadhi ya chombo ili serikali nyemelezi ikae mbali? Nani ataondolewa pale wasakadiploma watakaporejea; au watakuta chombo kimeyeyuka?

Je, kuna uchunguzi wowote uliothibitisha kuwa hawa wanaoanuliwa, hawana elimu au wana elimu ndogo iliyoleta madhara kwa chombo; au hata kuvunja sheria? Nani atabisha iwapo hili litaitwa ubabe na akili ya viziavizia?

Hii miaka mitano ya kupata diploma iliwekwa kwa utafiti gani ulioonesha kuwa kila mmoja atakuwa na uwezo au atawezeshwa na mwajiri wake, kwenda nje ya eneo la ajira kusaka diploma?

Hivi nani ajuaye kilichosibu waajiri na wataalamu wao katika vyumba vya habari, kutofikia lengo la kuwa na diploma katika miaka mitano kama sheria ya 2016 inavyotaka? Hakuna anayetaka kujua? Hakuna anayetaka kutaarifu? Hakuna anayetaka kusikiliza? Ni kasome…kasome!

Kuna ukweli huu. Kazi zote katika vyumba vya habari, hupita mikononi mwa maripota wa muda mrefu; maripota wakuu, wahariri wa habari; wasanifu; kaimu wahariri na wahariri wakuu. Vibarua hawa hulalamikiwa, husutwa na kulaaniwa kwa kila kosa gazetini, redioni, kwenye skrini ya TV – kila siku, kila wiki, kila mwezi, kila mwaka na siku zote.

Nina ushahidi wa wahariri wakuu, wenye digrii, ambao hawakuwa na vyeti wala diploma za uandishi wa habari. Wasikilize. Bado wanakumbuka ripota mwelekezaji, tena asiye na diploma, alivyokuwa mkali; akidai “uthibitisho” wa ulichoandika, maelezo ya anayetuhumiwa; na kukutolea jicho kali kwa kutoweka alama za uafikishaji katika andiko lako.

Wengine wanakumbuka walivyofunzwa jinsi ya kuandaa uchunguzi wa habari yoyote; kuanzia kutafuta wazo la kuandikia habari kwa chombo chochote; muundo wa hojaji, orodha za watoa taarifa, jinsi ya kukusanya data kwa ajili ya kazi yako; jinsi ya kuandika makala mbalimbali na kuwasilisha.

“Mzee Ndimara, wewe ndio uliniambia kuwa nilionekana kuwa na background nzuri. Nikueleze basi; nilipita mikononi mwa hao ambao hawana diploma lakini ni wakali wa kazi…” ameeleza binti mmoja shahidi wa kazi bora za waelekezaji katika chombo alikoanzia kazi – yeye akiwa na diploma.

Uliza baadhi ya wahariri. Watakwambia. Walifanya hivi: Walitundika diploma na digrii zao kutani. Wakaingia vyumba vya habari. Wakakaa chini ya wasio na vyeti. Wakalelewa. Wakaelekezwa. Wakafundishwa, Wakajua. Wakakua. Wakakwea madaraja. Wakawa wahariri. Wakameremeta!

Acha tunong`onezane: Baadhi ya wahariri, wanakiri kuwa hadi kustaafu, hawajawahi kufikia viwango vya baadhi ya walezi, waelekezji na walimu wao ambao hawakuwa na diploma. Wanawaenzi. Kwa nyakati zile na nyakati za sasa za kidijiti.

Kusoma ni muhimu. Nikiwa Mhariri wa Jamii kwa miaka mitano, Mwananchi Communications Limited, nilikuwa ninaongea na waandishi wa habari na kuwauliza: Lini uliajiriwa hapa? Ulikuwa unatoka wapi? Tangu umalize chuo umesoma vitabu vingapi? Msako wa elimu.

Kijana mmoja aliniambia kuwa tangu amalize masomo ya chuo kikuu na kuajiriwa – miaka mitano iliyopita – hakuwa amesoma hata kitabu kimoja. “Ni kuja kazini tu…”

Mwingine aliniambia kuwa kwa miaka mitano amekuwa akisoma kitabu kimoja ambacho hajamaliza; na chenyewe hivi sasa hajui kilipo. Niliumia sana; ingawa niliona wengine wakijisomea vitabu mitandaoni na wengine wakiwa na nakala za vitabu mikononi.

Nikashawishika kaandika makala kwa lengo la kuchochea usomaji; sasa nikipanua eneo hadi kwa wasomaji wa The Citizen – chini ya MCL. Msanifu Mkuu aliipa kichwa: If you don’t read, how do you write? (tafsiri nyembamba: kama husomi, unaandikaje/vipi/nini?). Jisomee hapa.

Lakini kuna wanaosoma. Wanaojisomea vitabu mbalimbali juu ya uandishi wa habari; misingi ya uandishi kwa wanafunzi; fikra mpya juu ya uandishi katika maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano; aina za uandishi; ufukuaji taarifa, uandishi habari za usuluhishi, uandishi katika mazingira magumu, uchambuzi, uandishi wa habari za siasa… Wanapekua. Wanataka kujua. Wanajielimisha.

Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo

Turudi kwenye swali letu la awali: Kwani kusoma kuna njia moja tu, aina moja tu, mahali pamoja tu na kitu kimoja tu cha kusoma?

Mapinduzi ya kiteknolojia katika eneo hili, kwa sasa, yanatosha kuanika wenye uwezo na kuanua waliopitwa na wakati. Ni ujio huu ambao utaondoa malalamiko ya kizembe kuwa “tasnia ya habari imevamiwa.” Haijavamiwa.

Mambo ya kuvamiwa ni kilio cha walioshindwa kujifua na kujipambanua kitaaluma; wanaolialia kuwa kila mmoja mwenye simu ya smati “anajifanya” mwandishi wa habari na mpigapicha.

Ukweli ni kwamba, hao kwa mamilioni, hawafanyi uandishi wa habari. Hao wanaolalamikiwa, wala siyo waandishi wa habari. Ni WAANDIKAJI wanaofurahia kujua kusoma na kuandika; na wanaofurahia uhuru wao wa kujieleza katika mazingira tuliyopigania toka mikaka ya 1980 kwamba, “We Want A Talking Nation; A Talking People!” Tunataka kuwa na Taifa linaloongea. Watu wanaoongea!

Kwahiyo, badala ya kulialia kuwa “taaluma imevamiwa,” waandishi wa kweli wajitahidi kujipambanua, kujitofautisha na waandikaji kwa kujihusisha na mambo mazito na ya maana.

Kwa mfano, habari za uchunguzi, utawala wa kisheria, haki za binadamu, uwajibikaji kwa walioko madarakani na maeneo mengine – utawala, haki, demokrasia – maeneo yanayohitaji ufukuaji na yenye mguso kwa jamii.

Sasa maripota, wasanifu, wahariri wengi walio katika vyombo hivi vya mawasiliano kwa muda mrefu; wakiwa bila diploma lakini wakilea, kuelekeza na kufundisha wenye diploma na digrii, hawastahili kile ambacho serikali inapanga au inatekeleza. Hapana!

Wengi wao wana upeo mpana na maarifa makuu ya kuwamegea wenzao; na siyo kuacha kazi, kwenda kusaka diploma ambayo, huenda wameishaivuka kama kungekuwepo tathmini ya kazi na uwezo wao.

Hapa kuna pendekezo. Siyo langu. Langu nitalitoa mwishoni mwa andiko langu juu ya kusemezana na waandishi wa habari, watawala na wananchi/wadau. Hili ni pendekezo la baadhi tu ya wadau wa habari ambao wamesoma baadhi ya makala zangu. Hili hapa:

“Kwakuwa serikali imetunga sheria – Sheria ya Huduma za Habari 2016 – inayotaka waandishi wa habari kuwa na diploma; basi hiyo iwahusu wanaoingia kazini kwa mara ya kwanza; na wale ambao, kwa tathmini maalum, watakutwa chini ya viwango kitaaluma.

“Kwa mfano, wenye miaka minne na zaidi kazini, ambao wamekuwa walezi, waelekezaji na walimu kwa miaka mingi (minne na kuendelea); wapate mafunzo maalumu, yanayohusisha mazoezi kikazi; kwa angalau miezi mitatu (kwa mfumo wa saa mbili kwa siku tatu kwa wiki) inayofuatiliwa kwa usimamizi wa wajuzi – ya kuongeza uwezo wao na thamani ya kazi zao; huku wakiendelea na kazi zao; badala ya kutelekeza vyombo ambavyo, ama walishiriki kuunda, kulea au kuimarisha.”

Sheria hii, Sheria ya Huduma za Habari 2016, ni chafu kuliko ile Newspaper ACT ya 1976 iliyofutwa. Hii inastahili kufanyiwa marekebisho makubwa au kufutwa kabisa. Tuijadili katika andiko lijalo.

 

Like
1