MKUU wa Wilaya ya Arusha, Kenani Kihongosi, ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM Iringa, ameonekana katika video moja akicharaza viboko watu wazima kwa tuhuma ambazo hazijathibitishwa. Kitendo hicho cha kikatili kimezusha mjadala katika jamii kuhusu ukatili unaofanywa na viongozi wa serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli. Mmoja wa wachambuzi ambao wamekubali tuchapishe maoni yao ni Livino Ngalimitumba, ambaye anasisitiza kwamba mkuu wa wilaya amevunja sheria kwa kudhalilisha raia hawa. Endelea.
Adhabu ya viboko (corporal punishment) ni moja ya adhabu zilizowekwa na Sheria za Jinai za Tanzania hususani Kanuno ya Adhabu, Sura ya 16, kifungu cha 25.
Adhabu ya viboko imewekewa utaratibu wa utekelezwaji kwa mtuhumiwa; chini ya sheria yake mahsusi inayoitwa “The Corporal Punishment Act,” baada ya kukutwa na hatia na mahakama yenye mamlaka kwa mujibu wa Ibara ya 13 (6) (a & b) ikisomwa sambamba na Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania (1977).
Adhabu zilioorodheshwa katika sheria hiyo ni pamoja na adhabu ya kifo kwa kunyongwa, kifungo jela, kulipa faini, na kadhalika.
Kitendo alichofanya DC wa Arusha kuwachapa viboko watuhumiwa wa wizi; ni kuwahukumu na kutekeleza adhabu ya viboko bila kushtakiwa na kusikiliza katika mahakama yenye mamlaka na bila kwanza kutiwa hatiani.
Je, DC akibaini au akimtuhumu muuaji katika eneo lake la utawala; atamnyonga kwa mkono wake? Amejichukulia sheria mkononi. Ni kosa!
Baada ya tukio hili, DC atapata ujasiri wa kukemea tabia ya wananchi kujichukulia sheria mkononi dhidi ya washukiwa na watuhumiwa?
DC amekuwa ni mlalamikaji mwenyewe, kisha akawa mshitaki mwenyewe, halafu akajivika mamlaka ya mahakama kuwahukumu adhabu ya viboko; mwishoni akawa ni afisa wa polisi yeye mwenyewe akatekeleza adhabu aliyowahukumu watu hao. Amekiuka misingi ya utoaji haki.
Amekiuka misingi ya mgawanyo wa madaraka miongoni mwa mihimili ya dola. DC ameingilia kazi ya mahakama, kutoa haki na kuhukumu baada ya kusikiliza kesi kwa ukamilifu wake. DC wa Arusha amekosea.