Daini Tanganyika yenu, achaneni na Zanzibar yetu – Mwalimu

WAKATI wanasiasa na wanaharakati wakihoji kwanini serikali imeziacha bandari za Zanzibari na kuziingiza bandari za Tanganyika pekee kwenye Mkataba wa Ushirikiano na Serikali ya Dubai, huku waliohusika kusaini mkataba huo, Rais Samia Suluhu Hassan na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Makame Mbarawa, wakionekana kutiliwa shaka kwasababu ya kuwa ni Watanzania wanaotokea upande wa Zanzibar;

Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar) wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Salum Mwalimu, ambaye ni Mzanzibari, ameibuka kujibu mapigo, na kuitetea Zanzibar, kuhusiana na sakata hilo

Karibu katika mikutano yote ya Oparesheni +255 ya Chadema, inayoendelea kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, Mwalimu amesikika akiitetea zaidi Zanzibar katikati ya mjadala wa bandari unaoendelea nchini.

Salum Mwalimu

Katika hotuba yake aliyoitoa jana Bunda mjini, Mwalimu, pamoja na mambo mengine, alisisitiza hoja na haja ya kupata Katiba Mpya ili kukomesha kabisa kile alichokiita chokochoko za Muungano baina ya upande wa Tanganyika na Zanzibar.

“Tunahitaji tupate Katiba Mpya ambayo si tu ipunguze madaraka makubwa ya rais, lakini pia itupatie muundo wa Muungano wa serikali tatu, ambao utaondoa malalamiko kutoka pande zote za Muungano,” alisema Mwalimu.

Mbali na jana, Mwalimu akizungumzia hoja yake hiyo, akiwa Bukoba Mjini , mkoani Kagera, na mjini Kahama, mkoani Shinyanga, ndani ya wiki chache zilizopita, Kiongozi huyo wa Chadema Zanzibar alisema tatizo si uzanzibari, bali ni muundo wa Muungano wa serikali mbili.

Kwamba, malalamiko yanayoibuka hivi sasa dhidi ya viongozi wa Jamhuri ya Muungano wanao tokea Zanzibar, yanayolenga viongozi wa serikali ya Muungano wanaotokea Zanzibar, kuhusishwa kufanya jambo lisilowapendeza Watanganyika, ni sawa tu na malalamiko ya muda mrefu ya Wazanzibar kuhusu Tanganyika kuvaa koti la Muungano.

“Hata hiyo nafasi ya Urais wa Muungano, ilisubiri mpaka kutokee msiba, ndipo Mzanzibari aweze kuongoza nchi. Wakati Watanganyika wanadhani nchi yao imemezwa na Muungano, sisi Wanzanzibari kwa muda mrefu tumekuwa tukipinga Tanganyika kuvaa koti la Muungano. Sisi tunaiona hii Tanganyika yenu kuwa Tanzania yenyewe. Sasa nyie jambo moja tu, kelele kibao. Sisi tumevumilia mambo mangapi?” alisema Mwalimu

Alisema ajenda kuu ya Wazanzibar ni kuipata Zanzibar yenye mamlaka kamili chini ya muundo wa Muungano wa serikali tatu, ili kila upande uwe na serikali yake na kuwe na serikali ya Muungano ambayo Mtanzania wa upande wowote wa Muungano atakuwa na uhuru wa kuongoza nchi bila kutiliwa shaka wala kuonekana anaingilia mambo ya nchi nyingine kama ilivyojitokeza sasa.

“Sisi tumedai Zanzibar yetu kwa muda mrefu, ninyi ndugu zetu Watanganyika kwa muda mrefu mlibaki mmelala. Mlipaswa mdai Tanganyika yenu na sisi tudai Zanzibar yetu halafu tukutane katikati kwa kila upande kuwa na serikali yake na mamlaka yake lakini wakati huo huo tupate serikali ya pamoja ya Muungano inayotuunganisha wote.

“Ninawashauri sasa ndugu zetu Watanganyika mdai Tanganyika yenu, lakini tafadhali “tusikanyagane.” Tatizo si uzanzibari bali muundo wa Muungano,” alisisitiza Mwalimu.

Rais Samia Suluhu Hassan

Mwanasiasa huyo aliyekuwa pia mgombea mwenza wa urais wa Chadema katika uchaguzi mkuu wa 2020, alisema yeye atakuwa mtu wa mwisho kutaka Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uvunjike, akitoa msimamo kuwa Muungano huo unapaswa kulindwa kama mboni ya jicho na kwamba kinqchohitajika ni kuboresha tu muundo wake.

“Kwa undugu wetu wa damu na malengo mazuri ya waasisi wetu, mimi Salum Mwalimu nitakuwa mtu wa mwisho kutaka Muungano uvunjike. Haupaswi kuvunjika bali kuboreshwa tu.

“Ni kwasababu ya Muungano huu mzuri, miye Mzanzibari niliweza kusoma shule ya sekondari hapa Shycom hapa Shinyanga. Nikaishi vizuri na ndugu zangu Wasukuma, japo mmekuwa wachoyo, miye Muislamu hamjanipa mke wa pili wa kisukuma mpaka leo,” alisema Mwalimu akiwa Kahama na kuibua vicheko kutoka kwa wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Chadema inaendelea na mikutano yake ya Operesheni +255 inayolenga kuzisemea shida za wananchi, kunadi sera za kisekta za chama hicho, kuvutia watia nia wa uchaguzi na kuimarisha mtandao wa wanachama na safu za uongozi wa Chama hicho kuanzia chini kabisa kwenye ngazi ya vitongoji mpaka Taifa.

Baada ya kumaliza mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga na Simiyu, Oparesheni hiyo sasa imeingia mkoa wa Mara.

Like