KUMEKUWA na mjadala mzito juu ya ajenda ya Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania (CHADEMA) kuhusu ama kususa au kuzuia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025, huku viongozi wa chama, hasa mwenyekiti Tundu Lissu, wakidai kuwa watazuia uchaguzi kufanyika, kwa sababu hawapo tayari kushiriki uchaguzi utakaosababisha mauaji ya wananchi. Upande mwingine, baadhi ya wanachama na wachambuzi wanasema hiyo ni nadharia isiyotekelezeka, na kwamba hata jitihada za kuzuia uchaguzi zinaweza kuhatarisha maisha ya wananchi vile vile. Katika makala hii, mchambuzi mwingine, EDWARD KINABO, anasisitiza kuwa hofu ya Lissu haina mashiko kisiasa kwani umaarufu wake na ushawishi wake pekee ni nguvu ya kushinda uchaguzi iwapo atakuwa na uwezo wa kuing’amua na kuitumia vema. Endelea:
Kwa Mwenyekiti huyu, tunao mtaji wa kushinda uchaguzi kwa mazingira haya haya
Si kweli kwamba mbinu za kukabiliana na hujuma ndani ya uchaguzi zimekwisha. Si kweli. No Reforms, No Elections isifunge fikra zote za kimkakati, za kupambana na kushinda uchaguzi katika mazingira haya haya magumu, ya katiba mbaya na sheria mbaya.
Na mwenyekiti wetu huyu tuliyenaye, huyu aliyenadiwa kwa sifa za kijasiri, hakika tunapaswa kumtumia kama mtaji na kama fursa kuu ya kufanya maajabu katika uchaguzi huu.
Tunapaswa kuumiza kichwa badala ya kufikiri suluhisho pekee ni kudai reforms kabla ya uchaguzi au kuzuia uchaguzi.
Mikakati na mbinu za kupambana katika uchaguzi usio huru wala wa haki bado zipo, tena nyingi sana. Nidokeze tu kwa ufupi.
Kwanza, tutafute pesa, tena ziwe nyingi. Tone Tone ni ubunifu mzuri, iboreshwe (maoni na mapendekezo yangu ya kuboresha Tone Tone nimeshatoa).
Kwa vyovyote vile itakuwa ni hasara na kosa kubwa la kimkakati iwapo tutakusanya pesa nyingi kutoka kwenye Tone Tone halafu pesa zote hizo zikaishia kutumika nje ya uchaguzi. Tone Tone ikawe mtaji na nguvu ya kwenda kwenye uchaguzi huu. Tone Tone isiishie kuwa mvua inayonyeshea nyikani.
Tutafute pesa nyingi ili tuweze kusuka na kuimàrisha organaizesheni ya kushinda uchaguzi katika mazingira haya haya magumu ɓadala ya kutafuta fedha nyingi za kuzuia uchaguzi. Lengo letu kuu kama Chama cha siasa si kuzuia uchaguzi, bali ni kuingia madarakani.
Tunaweza kuleta hizo “reforms” tukishaingia madarakani. Ukweli ambao hausemwi kabisa ni kwamba “njaa na ufukara mkubwa wa fedha,” ni sehemu ya mambo ambayo yamekuwa yakitukwamisha sana katika kujenga organaizesheni imara ya nguvu ya umma katika chaguzi zilizopita.
Tukiweza kupata fedha nyingi safari hii na fedha hizo zikatumika vizuri kimkaķati, hakika tunaweza kupiga hatua kubwa sana katika kukabiliana na hujuma nyingi za uchaguzi usio huru wala wa haki.
Pili, tuandae mapema makundi makubwa ya nguvu za umma katika ngazi za vitongoji, vijiji na mitaa kuanzia sasa.
A. Makundi hayo ya nguvu ya umma ndiyo yaje yatumike vizuri kwenye uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa vishindo ambavyo havijawahi kutokea nchi nzima (wahofie mapema kutuengua).
B. Makundi hayo ya nguvu ya umma ndiyo yaje kutumika kusindikiza mawakala wetu kwenda kuapishwa na kuwapeleka vituoni kulinda kura mapema kabisa kabla vituo havijafunguliwa, na kwa nguvu hiyo, wasimamizi washindwe kuzuia mawakala wetu kuingia vituoni. Kituo ambacho wakala wetu ataanza kuzuiwa kuingia, nguvu ya umma ihakikishe hakuna upigaji kura utakaoendelea kwenye kituo hicho, mpaka wakala wetu aruhusiwe (No Our Agent, No Voting).
C. Makundi hayo makubwa ya nguvu ya umma, ndiyo yatumike vizuri kwenye kuanzisha maandamano ya kuonya, kupinga au kuzuia njama zozote za kutaka kuengua mgombea wetu wa udiwani au ubunge. Angalau ni rahisi kufanya maandamano makubwa ya kupinga uenguaji katika kata au jimbo kuliko kuwaza kuzuia uchaguzi wa nchi nzima (No candidate, No election in that ward or constituency)
Tatu, tubadilishe “narrative” yetu kwa umma kuanzia sasa. Badala ya kusema watu hawana imani ya kupiga kura, sisi tubadilishe ujumbe na kujenga hamasa mpya mapema ili umma si tu uhamasike kupiga kura, bali pia ukashiriki kuzilinda kura kwa kishindo ambacho hakijawahi kutokea. Tuseme wazi kwamba ikibidi tutafia kwenye uchaguzi huu, watu wakapige kura na tutazilinda kwa gharama ya roho zetu zote.
Tumtumie vizuri kisiasa mwenyekiti huyu ili kujenga imani na mwamko mpya kwa umma. Zile hoja zilizosemwa kwenye kampeni za uchaguzi wa ndani ya chama, ya kwamba bwana huyu ndiye kipenzi cha umma, ndiye jasiri sana asiyeogopa kitu, ni mwanasheria nguli, ni muujiza wa Mungu unaotembea, ndiye mtu aliyewahi kuchungulia ahera halafu akarudi duniani, tuzitumie simulizi zote hizo sasa kujenga hamasa na mwamko wa umma ukapige kura na kulinda kura.
Itakuwa ni hasara kubwa na kosa kubwa la kimkakati, iwapo chama chetu kitaogopa kuingia kwenye uchaguzi huu wakati kimepata mwenyekiti mpya, aliyenadiwa kwa hoja na sifa za kijasiri. Sifa nyingi na nzuri ambazo mwenyekiti wetu wa chama alinadiwa nazo, si sifa za kutufanya tukimbie au tuzuie uchaguzi, bali ni sifa za kupambana na kushinda uchaguzi huu katika mazingira haya haya magumu ya katiba mbaya na sheria mbaya.
Mwenyekiti wetu aliyesheheni sifa nyingi za kijasiri, sasa ageuzwe kuwa fursa na mtaji wa Chama kuingia kwenye uchaguzi kwa nguvu mpya, kwa kishindo kipya, kwa uthubutu na kwa jeuri ya hali ya juu.
Tutoke kwenye kauli mbiu ya “No Reforms, No Elections“, na badala yake twende kwenye kauli mbiu za kijasiri zaidi, kama “No Retreat, No Surrender“, “Tutarudi na roho zetu” “Come what may, we shall win“. Twendeni kwenye uchaguzi.
Nne, kwa nguvu ya umma na organaizesheni yote tutakayoijenga, tuingie kwenye uchaguzi kwa lengo la kudhibiti na kupambana na hujuma zote, moja baada ya nyingine, hatua kwa hatua.
Tuwe na mkakati wa kitaifa wa usimamizi wenye kuongozwa na makamanda wa chama waliopikwa kwa ubora wa kitaifa na kimataifa katika kuongoza nguvu ya umma, na makamanda hao wasambazwe kwa wingi nchi nzima, kwenye kata na majimbo yote kama walivyokuwa ZOCs na JOCs.
Tupunguze ule udhaifu wetu katika chaguzi zilizopita, ambapo karibu kila jimbo na kila kata ilihujumiwa, ilionewa na kudhulumiwa kivyake-vyake na bila kupata msaada wowote kutoka kwenye machineries za chama.
Tutengeneze mfumo imara na wenye uangalizi na udhibiti wa pamoja wa hujuma za uchaguzi ili tusiteketezwe kirahisi kama Kuku wanaokufa kwa kideri, kama walivyotufanyia katika chaguzi zilizopita. Wanaodhani tutaingia kwa unyonge na udhaifu ule ule wa siku zote, tuwashangaze. Kikawake, kikanuke, pakachimbike, haki ikashinde dhidi ya uonevu.
Tukahakikishe tunashinda uchaguzi wote na kushika dola au tukapate kura nyingi na viti vingi sana, na hapo hapo vuguvugu la kupinga matokeo haramu na kudai “reforms” likazuke kwa nguvu kubwa kwa kutokea kwenye uchaguzi wenyewe.
Tano, key point ni kwamba, uchaguzi usio huru na haki si kikwazo, bali ni fursa kuu ya kuushiriki kama ulivyo na kuanzisha mapambano ya kudai haki na mageuzi katika Taifa. Tusiwe wepesi kufikiri kwaba njia nzuri na ya pekee ni ya kudai reforms kabla ya uchaguzi au kuzuia uchaguzi. Matatizo hayakimbiwi wala hayakwepwi, bali matatizo hukabiliwa.