Katika Misa ya Pasaka iliyoadhimishwa kitaifa leo kwenye Jimbo Katoliki la Kayanga, mkoani Kagera, Askofu Almachius Rweyongeza amezungumzia masuala muhimu kijamii na kitaifa. Hizi ni dondoo kuu za mahubiri ya Askofu Rweyongeza:
1. “Amani ni kazi ya haki wala si matokeo ya vita. Amani si kutokuwa na vita. Amani ni matokeo ya haki.
Serikali inabidi ijihusishe katika kulinda amani.”
2. Mti hauli matunda yake wenyewe bali huliwa na wengine. Basi na sisi tujitoe katika kutoa matunda au karama zetu kuwanufaisha wengine. Hizi karama tumepewa bure.
3. Maendeleo bila dhamira (conscience) safi huaribiwa na kubomoka kwa muda mfupi sana.
Maendeleo ya watu hayajengwi kutokana na pesa wala vitu na teknolojia bali kwa dhamira njema ya kuwatumikia watu.
4. Ukitaka kuangamiza taifa lolote huhitaji kutumia nguvu za nuklia bali toa elimu duni. Kuchezea elimu ni kuangamiza taifa. “Watu wangu wameangamia kwa kukosa maarifa” (Kitabu cha Hosea).
Je, mfumo wetu ni kama biashara? Kubadilishwabadilishwa kwa sera na mfumo wa elimu nini mwelekeo wetu? Kila mara mitaala inabadilishwabadilishwa bila kuwepo umakini. Msemo wa kilatini wa
“Non scholae sed vitae discimus,” ni wa maana sana.
Mfumo wetu wa elimu hautayarishi vijana wetu kuwa raslimali imara kimaisha bali wa kuliangamizi taifa letu.
5. Kulegeza vigezo vya ufaulu kinyume cha viwango vya kimaitaifa hakuleti tija. Ubora wa elimu si kulegeza ufaulu ili kuongeza idadi ya wafaulu. Wanaopata viwango vya chini vya ufaulu ndio wanapelekwa katika vyuo vya walimu. Matokeo yake ni kuzalisha wezi, watu wasiokuwa na dira nk, na hatimaye kuchangia kujaza Magereza.
Kama mwalimu ni mbabaishaija akaanza kuchekwa na wanafunzi wenye akili ya kuzaliwa, ataamua kuwachapa viboko.
6. “Dunia itaharibiwa si na watenda mabaya bali kwa ukimya wa watu wema.” Einstein
7. Somo la dini shuleni liende sambamba na masomo dunia mengine ili watoto wetu waendane na tabia njema maishani mwao.
8. Mafisadi, wabaguzi, wategeaji na watoro kazini, wauwaji, wezi nk wanatokana na elimu isiyokwenda sambamba na maadili.
Wanaoapa eti “Mungu nisaidie,” na huku matendo yao ni kinyume cha hayo ndio matokeo ya uonevu, ubadhirifu nk.
9. Mtu aliyeshindwa na somo la dini asiajiriwe, na kabla ya kuajiriwa adhaminiwe na kiongozi wake wa dini; vinginevyo serikali itaendelea kuwaajiri wahalifu.
10. Kutokariri darasa kunazaa watoto wasiokuwa na maarifa. Vijana wanatahiniwa kwa kufanya mitihani ya multiple choice ambayo ni ya kubahatisha. Haiwajengei tu kutojua lugha ya kujieleza bali pia kutokuwa na uwezo wa kuchambua mambo.
Kwa nini serikali inazuia shule ambazo haizigharimikii kutokaririsha wanafunzi ili wakomae kielimu?
11. Unahitajika mjadala wa kitaifa kuhusu elimu ya vijana. Hili ni jambo lisiloepukika na kwa haraka sana.
Hii hapa ni video ya sehemu ya ibada hiyo.