Askofu Bagonza atoa neno kukoleza “ufunuo” ulioletwa na Antony Diallo

Askofu Benson Bagonza

 KATIKA ukurasa wake wa Facebook, Askofu Benson Bagonza wa KKKT Dayosisi ya Karagwe ameandika chapisho akalipa kichwa “INAFIKIRISHA! INASUTA! TUSUTIKE!” Linatoa uchambuzi mfupi na maono yake baada ya kumsikiliza Mwenyekiti wa CCM Mkoa Mwanza, Dk. Antony Diallo, akizungumza katika kipindi cha AJENDA kupitia Star TV jana usiku, juu ya kile alichoita “rais mwenye kichaa” tuliyekuwa naye huko nyuma. Askofu Bagonza anasema hivi: 

Nilipochaguliwa kuwa Askofu baada ya wanaofaa kukosekana, marafiki zangu waliandaa tafrija ya kuniaga huko Chicago, Marekani. Mmoja wa watani wangu akatoa hotuba na kusema “Benson, wewe sasa ni Askofu. Tangu sasa una uhakika wa mambo matatu:

1. Daima utakula chakula kizuri

2. Daima utavaa vizuri

3. Daima hutaambiwa ukweli.

Ni miaka 19 tangu niambiwe na yote nimeyaona. Ufafanuzi wa niliyoyaona nitaufanya siku nyingine. Kimsingi Viongozi katika jamii tunaishi kwa kujidanganya,  kudanganya na kudanganywa.  

Leo Nina hili:

Comrade Anthony Diallo amesema maneno mazito. Ametimiza ahadi ya mwana TANU/CCM isemayo “Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko”. Ukweli uliochelewa ni bora kuliko uwongo uliowahi.  

Nitoe ushauri ufuatao:

1. Viongozi na watawala wetu kama hawawezi kuzuia kusifiwasifiwa basi angalau wanune wakisifiwa.

2. Waliokwishamaliza muda wa uongozi wasijengewe masanamu au kutangazwa ni watakatifu mpaka muda maalum upite.

3. Ikithibitika kuwa kiongozi wa umma ngazi yeyote amewahi kuwa na tatizo la afya akili, maamuzi yake yote yatenguliwe.

4. Walioathirika au kunufaika na maamuzi ya kiongozi mwenye tatizo la afya ya akili wajulikane na kusaidiwa.

5. Itungwe sheria maalum kujinaisha vitendo vya kusifia viongozi wa umma hadharani au kupendekeza ukiukwaji wa Katiba. Anayetaka kumsifia kiongozi amwandikie barua binafsi. Kusifia hadharani ni rushwa.

6. Iwe marufuku wananchi kuwapigia makofi viongozi au kuwachezea ngoma, badala yake Viongozi wawapigie makofi wananchi na kuwachezea ngoma. Waliomba kutumwa, makofi ni ya nini?

Haya yote yanasisitiza msimamo wangu wa TUSISUBIRI KUPONGEZA WALA KULAUMU.

BONYEZA HAPA KUSIKILIZA KIPINDI KIZIMA NA KAULI YA DIALLO

Like
8