KUONDOKA NCHIMBI KWAFUNGUA MASWALI MAGUMU ZAIDI

Matukio ya kujiuzulu na kufukuzwa kwa Dk Emmanuel Nchimbi yameacha gumzo kubwa kitaifa, na yameongeza sura katika kitabu cha uongozi wa nchi, hasa wanapojadiliwa makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania tangu Abeid Karume hadi Deo Ndejembi.

Lakini historia haitamkumbuka Nchimbi kwa sababu tu alikuwa Makamu wa Rais aliyejiuzulu. Itamkumbuka zaidi kwa mazingira ya kuondoka kwake.

Alitangaza kujiuzulu Agosti 25, 2026, akisema angeondoka rasmi Septemba 4. Rais Samia Suluhu Hassan akakubali. Siku iliyofuata, kabla hata tarehe hiyo haijafika, CCM ikamfukuza uanachama kwa madai ya kukiuka Katiba, kanuni, maadili na nidhamu ya chama. Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kufukuzwa huko kulimwondolea sifa ya kikatiba ya kuendelea kuwa Makamu wa Rais. Hivyo, safari iliyotarajiwa kumalizika Septemba 4 ikakatishwa Agosti 26.

Hapo ndipo kujiuzulu kukageuka kuwa jambo kubwa kuliko kujiuzulu. Kwa sababu swali halikuwa tena: Kwa nini Nchimbi amejiuzulu? Likawa: Nini hasa kimetokea?

Barua yake ilisema mengi 

Katika barua yake, Nchimbi hakumtuhumu Rais. Hakusema amefukuzwa serikalini. Hakusema amelazimishwa kujiuzulu.

Badala yake, alikumbusha ahadi aliyosema alimpa Rais Samia kabla ya uchaguzi wa 2025: kwamba angemsaidia kwa uaminifu, lakini siku Rais akihitaji Makamu mwingine, yeye angekuwa tayari kuondoka.

Kisha akaandika maneno ambayo ndiyo yamebeba uzito wa barua nzima: “Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa Mheshimiwa Rais anatamani mabadiliko.”

Akaondoka. Hapo ndipo lugha ya kisiasa inapotakiwa kusomwa zaidi ya maneno yenyewe. Nchimbi hakusema Rais alimwambia aondoke. Alisema yeye amejiridhisha kwamba Rais anataka mabadiliko. Hakusema mabadiliko hayo ni yapi. Hakusema amejiridhisha kwa ushahidi gani.

Kwa hiyo, badala ya barua kujibu maswali, ikazalisha mengine. Kama huu ulikuwa uamuzi wa kawaida wa kustaafu, kwa nini CCM ilihitaji kumfukuza mtu ambaye tayari alikuwa ametangaza kuacha siasa?

Kama kosa lake lilikuwa kubwa kiasi cha kustahili kufukuzwa CCM, kosa hilo ni lipi? Na kama alikuwa amekiuka kwa kiwango hicho maadili na Katiba ya chama, ukiukaji huo ulianza lini?

Haya ndiyo maswali yanayofanya suala la Nchimbi lisimalizwe kwa taarifa ya kujiuzulu.

CCM inamjua Nchimbi

Nchimbi hakuwa mgeni ndani ya CCM. Amekulia humo kisiasa. Amekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, mbunge, naibu waziri, waziri, balozi, katibu mkuu wa CCM na hatimaye makamu wa rais.

Huyu si mtu aliyekuja ghafla na chama kikashindwa kujua tabia yake, historia yake, marafiki zake, mitandao yake na fikra zake. Zaidi, Nchimbi ana historia ya kuwa na msimamo katika nyakati ambazo si rahisi kuwa nao.

Mwaka 2015 alikuwa miongoni mwa viongozi wa CCM waliopinga namna jina la Edward Lowassa lilivyoondolewa katika mchakato wa kupata mgombea urais wa chama. Alipitia misukosuko yake, lakini hakutoweka. Miaka baadaye akarudi katika safu za juu, akawa katibu mkuu wa CCM.

Kisha akateuliwa kuwa mgombea mwenza wa Samia mwaka 2025. Hapo ndipo jambo linakuwa zito zaidi.

Kwa kumteua kuwa mgombea mwenza, CCM haikuwa inampa tu Nchimbi cheo. Ilikuwa inamweka katika nafasi ambayo, katika mazingira yanayotajwa na Katiba, inaweza kumfikisha kwenye urais.

Tanzania tayari imeona hilo likitokea. Samia mwenyewe alikuwa makamu wa rais hadi Machi 2021, kifo cha Rais John Magufuli kilipomfikisha katika urais.

Kwa hiyo, chama kinapokuchagua kuwa mgombea mwenza, kwa maana nyingine kinakuwa kimesema: tumekuchunguza, tunakujua na tunakuamini kiasi cha kuwa tayari kukukabidhi nchi endapo mazingira yatahitaji.

Ndiyo maana tukio la Nchimbi linahitaji maelezo zaidi. Mtu ambaye miezi michache iliyopita alifaa kuwa hatua moja kutoka urais, alikuwaje ghafla hafai hata kuwa mwanachama wa CCM?

Labda tatizo ni nyendo zake

Katika wiki zilizotangulia kuondoka kwake, Nchimbi alikuwa tayari amezua mjadala ndani na nje ya CCM kutokana na kauli zake kuhusu Katiba Mpya.

Julai 2026, akizungumza katika mkutano wa watetezi wa haki za binadamu, aliwataka Watanzania kuendelea kupigania Katiba Mpya; Katiba yenye muafaka wa kitaifa, inayoheshimu utu na haki za wananchi. Kauli hiyo ilivuta mjadala mkubwa kwa sababu hoja ya Katiba Mpya tayari ilikuwa sehemu ya ahadi za serikali na CCM.

Lakini jambo muhimu zaidi halikuwa tu kile alichosema. Lilikuwa nani aliyesema hayo. Makamu wa Rais si mwanaharakati. Si kiongozi wa upinzani. Ni mtu wa pili katika uongozi wa nchi.

Anapowaambia wananchi “pambaneni” kupata jambo ambalo serikali yake yenyewe ina mamlaka makubwa ya kulitekeleza, sentensi hiyo inapata maana pana zaidi.

Watu wakaanza kuhoji: Pambaneni na nani? Hata Askofu Benson Bagonza aliuliza swali hilo wakati huo. Kama rais anataka katiba mpya, kwa nini wananchi waambiwe waipambanie?

Siwezi kusema kwa ushahidi kwamba kauli hiyo ndiyo iliyomwondoa Nchimbi. Lakini tunaweza kusema kwa uhakika kwamba ilizua mjadala na ukosoaji ndani ya chama. Vyombo vya habari vimeripoti kwamba baadhi ya watu ndani ya CCM waliziona kauli zake kuwa hazikuwa za lazima. Hapo ndipo 2030 inapoingia.

Kivuli cha 2030

Tayari Nchimbi amekuwa anatajwa katika mijadala ya kisiasa kuwa anataka baada ya Samia. Kutajwa si kugombea. Kutamani si kutangaza nia. Na mpaka sasa hakuna ushahidi wa wazi kwamba Nchimbi alikuwa ameanzisha kampeni rasmi ya urais wa 2030.

Lakini siasa hazisubiri kampeni rasmi. Wakati mwingine tatizo la mwanasiasa si kile alichotangaza. Ni kile ambacho watu wenye mamlaka wanaamini anaweza kuwa anakifikiria.

Hapa ndipo nafasi ya .akamu wa rais inakuwa ya ajabu. Makamu anatakiwa kuwa mkubwa, lakini asiwe mkubwa sana. Anatakiwa kuonekana, lakini asionekane sana.

Anatakiwa kuwa na ushawishi wa kutosha kumsaidia rais, lakini ushawishi huo ukianza kuonekana kama mtandao wake binafsi, unaweza kuwa tatizo. Anatakiwa kuwa tayari kuwa rais ikibidi, lakini asionekane kama anasubiri kuwa rais. Hilo ndilo fumbo la umakamu wa rais.

Nchimbi mwenyewe alionekana kulifahamu. Alipokubali kuwa mgombea mwenza, alisisitiza hadharani kwamba angekuwa msaidizi, si mshindani wa Samia.

Kauli hiyo leo inavutia zaidi sasa kuliko ilivyokuwa wakati ilipotolewa.Kwa nini mtu ambaye hakutuhumiwa hadharani kumshindania rais aone umuhimu wa kusema yeye si mshindani? 

Huenda ilikuwa lugha ya kawaida ya utii. Lakini huenda pia alikuwa anajua kwamba katika nafasi hiyo, hata uwezo wako tu unaweza kutafsiriwa kuwa tishio au ushindani.

Kufukuzwa kulibadili simulizi

Kama Nchimbi angeishia kujiuzulu na kwenda nyumbani, mjadala huu ungeweza kufa taratibu. Lakini CCM ikafanya jambo jingine. Ikamfukuza.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro, alisema vikao vya chama vilibaini ukiukaji wa Katiba, kanuni na maadili na kwamba uamuzi wa kumfukuza ulifikiwa kwa kauli moja. Lakini maelezo ya kina ya makosa yaliyosababisha adhabu hiyo hayajawekwa hadharani.

Kimsingi, CCM ndiyo ilifanya kesi ya Nchimbi kuwa kubwa zaidi. Kwa sababu sasa si suala la mtu kuamua kustaafu. Ni suala la chama kumwadhibu mtu ambaye jana yake alikuwa mtu wa pili kwa ukuu nchini.

Na adhabu hiyo ilikuwa na athari ya moja kwa moja ya kikatiba. Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema baada ya kupoteza uanachama wa chama kilichomdhamini, Nchimbi alipoteza pia sifa ya kuendelea kuwa Makamu wa Rais.

Kwa hiyo kufukuzwa hakukuwa ishara tu. Kulimaliza mamlaka yake.

Kwa hatua hiyo, Rais Samia sasa ana makamu mwingine: Deo Ndejembi. Kisiasa, hiyo inarudisha utulivu wa taasisi. Serikali inaendelea. Nafasi imejazwa. Mfumo unasonga mbele.

Lakini uteuzi wa Ndejembi haujibu maswali yaliyoachwa na Nchimbi. Badala yake, unafungua mengine.

Ndejembi ameingia katika ofisi ambayo mtangulizi wake ameondoka katika mazingira ya kutatanisha. Atalazimika kujifunza mipaka yake mapema: kiasi gani cha kuonekana, kiasi gani cha kusema, kiasi gani cha kujenga ushawishi na, muhimu zaidi, jinsi ya kuwa mrithi wa kikatiba bila kuonekana kuwa mrithi wa kisiasa.

Hilo si tatizo la Ndejembi peke yake. Ni tatizo la mfumo. Kwa sababu kama makamu wa rais mwenye ushawishi anaweza kutafsiriwa kuwa tishio, basi mfumo unaweza kujikuta ukipendelea manaibu wasio na nguvu. Na makamu dhaifu anaweza kuwa salama kisiasa, lakini si lazima awe bora kwa nchi.

Nchimbi wa nje anaweza kuwa mkubwa kuliko wa ndani?

Kuna uwezekano Nchimbi anamaanisha kabisa alichosema, kwamba amestaafu. Anaweza kwenda nyumbani na kukaa kimya.

Lakini mazingira yamembadilisha. Jana alikuwa mwanasiasa wa CCM aliyesema anastaafu. Leo ni .akamu wa rais wa zamani aliyefukuzwa CCM. Hadi sasa hana chama.

Hayo ni mazingira mawili tofauti. Akiwa serikalini, alikuwa amefungwa na uwajibikaji wa pamoja. Akiwa CCM, alikuwa amefungwa na nidhamu ya chama.

Sasa minyororo yote miwili haipo. Hilo halimaanishi ataanza kuzungumza. Lakini maana yake ni kwamba anaweza kuzungumza. Na akizungumza, atasikilizwa. Akinyamaza, ukimya wake nao utatafsiriwa.

Atakayetembelea nyumbani kwake ataangaliwa. Atakayemtetea ataangaliwa. Wanasiasa waliokuwa karibu naye wataangaliwa. Na iwapo hatua za kinidhamu zitaanza kuwafuata watu wanaodhaniwa kuwa katika mtandao wake, tutajua kwamba jambo hili halikuwa kuhusu mtu mmoja, bali Lilihusu kitu kikubwa zaidi.

2030 imeanza mapema

Hapa ndipo kuna kejeli ya mwisho. Kama sehemu ya wasiwasi dhidi ya Nchimbi ilitokana na hofu kwamba alikuwa akijiandaa kwa 2030, basi kumwondoa kwake kumefanya jambo lilelile ambalo huenda lilikuwa linaogopwa.

Kumeanzisha mjadala wa 2030 mapema. Sasa kila anayepanda kisiasa atapimwa kwa kipimo hicho.  Maswali yataibuka. Samia anataka nani baada yake? CCM inamwandaa nani? Ndejembi ni .akamu wa rais tu au anaweza kuwa zaidi? Nchimbi amestaafu kweli, au mazingira yanaweza kumrudisha?

Na kubwa zaidi: CCM itasimamiaje mpito wa madaraka baada ya Samia bila kugeuza kila mwanasiasa mwenye nguvu kuwa mshukiwa? Na katika mazingira ambayo CCM inazomewa kila kona, haitajiki walau mwanasiasa mmoja wa aina ya Nchimbi ambaye angesaidia chama kukubalika kwa umma na kushindana kwa hoja?

Haya ni baadhi ya maswali ambayo kuondoka kwa Nchimbi kumeacha mezani. Ndiyo maana simulizi hii haiwezi kufungwa kwa sentensi kwamba Emmanuel Nchimbi amejiuzulu umakamu wa rais au amefukuzwa uanachama. Hayo tunayajua.

Tusichokijua ndicho muhimu zaidi ni hiki: alifanya nini hasa, au mfumo uliamini alikuwa anakuwa nani, kiasi kwamba ndani ya muda mfupi mtu aliyekuwa anafaa kuwa hatua moja kutoka urais akaonekana hafai hata kubaki mwanachama wa chama kilichomfikisha huko?

Mpaka Nchimbi aamue kusema, au CCM iamue kueleza kwa undani zaidi, kuondoka kwake kutakuwa kumemaliza umakamu wake. Lakini hakutakuwa kumemaliza simulizi yake. Huenda ndiyo kwanza kumeianza.

………………………………………………………………………………………

Uchambuzi huu niliuandika na ukachapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la mtandaoni PAMBAZUKO toleo namba 180 tarehe Agosti 31 – 6 Septemba 2026.

 

Like