NCHINI Tanzania kuna kitu kinaitwa: Sheria ya Huduma za Habari. Ilitungwa mwaka 2016.
Sheria hii ndiyo mzazi wa ITHIBATI; ule uhakikisho wa serikali kuwa umekubaliwa (au umetambuliwa, umethibitishwa, umeidhinishwa, umeruhusiwa) kuwa mwandishi wa habari.
Baada ya hapo, unapewa kitambulisho – maarufu PRESS CARD – kuonesha kuwa wewe ni mwandishi wa habari aliyeidhinishwa na serikali.
Hii, maana yake ni kwamba, sheria imeipa serikali; au serikali imejipa mamlaka – kupitia sheria yake – kuamua nani awe mwandishi wa habari Tanzania.
Kwahiyo, hamu yako, utashi wako, malengo yako, matarajio yako, ndoto zako; vyote hivi havina maana kama hujaorodheshwa, ukasajiliwa na kutamkwa na serikali kuwa umehakikishwa; na hivyo unaruhusiwa kupata ITHIBATI ya kuwa mwandishi wa habari.
Bila shaka, hii ndiyo sababu, fasili ya “mwandishi wa habari” – journalist – katika sheria hii, inatanguliza uhakikisho wa serikali kwamba inaridhia “mwombaji” afanye kazi ya uandishi wa habari.
Huko kwingine duniani, fasili ya mwandishi wa habari huwa moja kwa moja, kwamba ni mtu mwenye kazi/taaluma ya habari. Baada ya hapo, huhorodheshwa kazi anazofanya.
Chaguo la serikali
Huku kwetu Tanzania, sheria iliyochongwa mwaka 2016 (imefanyiwa marekebisho kadhaa mwaka 2023), inatoa fasili ya mwandishi wa habari kwa kuanza kueleza kuwa: ni mtu (accredited) aliyekubaliwa rasmi na serikali; na kusajiliwa kufanya kazi ya uandishi wa habari. Huu ni msiba.
Sheria hii haitangulizi ufafanuzi wa mwandishi wa habari na kazi zake. Inatanguliza kibano. Kufuli. Pingu. Inatanguliza kile inachotaka kupata. Kumiliki mwandishi wa habari.
Aidha, ikiwa inalenga Huduma za Habari, sheria hii haina fasili ya “habari.” Kama imesahaulika au imetupwa makusudi katika “Kapu la Bibi” – MAUDHUI (content) wakijifariji kuwa kila mmoja atajua ni nini (!?).
Yawezekana pia, kwa serikali, kuwa “habari” siyo muhimu. Wanahitaji neno hilo kutumika kama ngazi tu ya kuwafikisha kule waendako: Kumiliki mwandishi wa habari.
Tungo tano shubiri
Hebu sasa tuone tungo tano za shanga zenye vimulimuli, tulizoletewa mwaka 2016; tukichumbiwa kuzivaa kwa hiari zetu wenyewe; kwa tabasamu na hata mpasuko wa kicheko:
(i) Ni marufuku kufanya kazi ya uandishi wa habari kama huna Ithibati (anayefanya kazi ya uandishi wa habari bila kusajiliwa, atakuwa ametenda kosa chini ya sheria hii (ya Serikali).
(ii) Mwandishi wa habari aliyesajiliwa kwa mujibu wa sheria hii atapewa Press Card na Bodi ya Usajili ya Waandishi wa Habari – Journalists Accreditation Board – JAB (ya Serikali).
(iii) Kitambulisho (Press Card) cha serikali ndicho kitakuwa ushahidi kwamba mwenyenacho ndiye anatambuliwa kuwa mwandishi wa habari; tena aliyesajiliwa (na Serikali).
(iv) Kila mwandishi wa habari aliyesajiliwa, moja kwa moja atakuwa mwanachama wa Baraza (Huru) la Habari (la Serikali).
(v) Yeyote ambaye, bila sababu kisheria, atashindwa au atakataa kufuata maagizo ya Bodi (ile Bodi ya thibitiko – itoayo Ithibati), atakuwa ametenda kosa chini ya sheria hii (ya Serikali).
Kila kitu cha serikali
Jipe muda kusoma tena, tungo hizo tano hapo juu. Utagundua kuwa hakuna kilicho cha mwandishi wa habari. Kila kitu ni cha serikali; tena kwa lengo la kuwa kitanzi kwa mwandishi wa habari.
Sheria hii – tuiite “mzazi wa Ithibati” – ni tishio kwa yeyote aliye katika kazi/ajira na taaluma ya habari; na hata mwenye shauku ya kuwa mwandishi wa habari.
Inafanya kazi ya uandishi wa habari kuwa kitu cha kuruhusiwa; cha kuomba na kupewa au kunyimwa na serikali. Kitu cha kusubiri majibu. Kitu cha kusajiliwa na kufutwa wakati wowote. Huu ni msiba.
Ni kama kukaa kwa tako moja, kwenye ncha ya mtumbwi wenye matobo katika bahari iliyochafuka kwa mawimbi mazito! Na bado unachumbiwa kutabasamu.
Tungo hizo tano hapo juu, zinaonesha kuwa sasa kuna njia moja tu iliyosalia kwa Mtanzania kuwa mwandishi wa habari: ni kwa kuidhinishwa, kusajiliwa, kupewa Press Card na serikali.
Baada ya hapa, hautakuwa utani kukuita “mwandishi wa serikali.” Hata neno “habari” halina mahali pa kukaa.
Tumetoka Press Card kuwa kitambulisho tu – kuwa wewe ni nani; tumeingia uhalalisho kuwa mwenye nacho ndiye pekee mwandishi wa habari. Kama tumetoka mbali, basi tumefika mbali.
Hoja basi ni iwapo tunajua tunakokwenda au tunakopelekwa: kwenye unyakuzi wa haki ya uhuru wa kujieleza. Kwenye maziko ya haki ya uhuru wa kupata, kutafuta na kusambaza taarifa: Nawe bado unatabasamu. Tusemezane.
Sheria tatu mwendokasi
Sheria ya Huduma za Habari ni miongoni mwa sheria tatu za udhibiti wa vyombo vya mawasiliano na waandishi wa habari, zilizotungwa kwa kasi kati ya mwaka 2016 na 2020.
Hizi hapa: Sheria ya Huduma za Habari, 2016; Sheria ya Upatikanaji Taarifa, 2016; na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni) Mawasiliano, 2020. Zitafute. Zisome.
Kumbuka haya yalifanywa katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Rais John Pombe Magufuli. Aliingia madarakani akihema, akilaani kwa kupata kura kidogo kuliko mtangulizi wake yeyote. Ni kweli.
Aliyekuwa mkiani hadi Magufuli anaingia alikuwa Jakaya Kikwete (CCM). Alikuwa àmepata kura 5,276,827 (62.83%}.
Mwaka 2015, Magufuli alipata kura 8,882,935 (58.46%}. Idadi hii ilimtibua. Mwaka 2020 alipata kura 12,516,252 (84.40%}. Alikuwa anajiandaa kwa 99% mwaka 2025. Hakufika.
Magufuli aliingia madarakani akijiapiza “ataangamiza upinzani.”
Alianza kwa kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama hivyo kwa madai kuwa baada ya uchaguzi, washindi waachwe kutekeleza ahadi zao kwa wapigakura; bila usumbufu. Kufuli likabanwa kwenye kazi za wazi za kisiasa za vyama vya upinzani.
Hoja na viroja vya Magufuli
Tangu mapema baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, Magufuli alitua kwenye kila hoja na kiroja; kwa nguvu na hamasa.
Atakamata wezi; atatuhumu wahujumu uchumi, ataona wasio wazalendo; “atatumbua” alioita wazembe na “wasiofaa” kuwa viongozi; atalialia kuwa yeye ni “msema kweli,” atajirudiarudia kuwa yeye ni “mpenzi wa Mungu.” Atamalizia kwa kusema, “…naomba mniombee.”
Magufuli alibeba waandishi wa habari kama mashahidi wa “mabomu” yake aliyolipua hapa na pale; nao wakawa maripota watiifu wa kunukuu na kusambaza alichosema – bila nyongeza, bila uchunguzi, bila upungufu wa vikolezo vyake, bila neno kwa kasoro zilizoonekana waziwazi; na mara nyingi, bila ufuatiliaji kabisa.
Mmoja wa maripota vijana walioripoti mikutano yake mingi amenisimulia – pamoja na mambo mengine – “Tulikwenda naye hivyohivyo. Akikiwasha tunakiwasha. Akikizima tunakizima. Hakutupenda. Alitutisha. Hatukumpenda. Tulimwogopa. Lakini kazi tulifanya.”
Ni katikati ya uhusiano wa aina hii, ndani ya miaka minne, zilitungwa sheria zilizoandaa unyakuzi wa haki ya uhuru wa waandishi wa habari; uhuru wa habari na uhuru wa mwananchi wa kutafuta, kupewa taarifa; na kusemezana na wenzake.
Nao waandishi wa habari hawakuhisi. Hawakuona. Hawakusikia la mtu. Walimbeba rais hadi Uchaguzi Serikali za Mitaa (2019) na Uchaguzi Mkuu, 2020 – chaguzi zilizokomba vyungu na kulamba mwiko wa upinzani.
Hata baadhi ya waliotangazwa kushinda, ndani ya chama chake, bado mpaka leo wanashangaa kilichotokea – ngazi zote: mitaa, udiwani na ubunge.

Mikono kichwani, kilio
Ni hapa Uchaguzi Mkuu wa 2020 ulipoitwa “Uchafuzi Mkuu.” Chama kikuu cha upinzani wakati huo Chadema, kilirudi na mbunge mmoja – mikono kichwani, kikibwaga kilio “…hapana, hapana! Wametuibia.” Waliibwa pia.
Lakini ni katika kipindi hicho cha kwanza cha urais wake, Magufuli alianza kutamka kuwa kazi anayofanya inaweza kufanywa tu na “mtu aliyejitoa Muhanga;” na kwamba yeye amejitoa muhanga kupambana na mafisadi.
Alifikia hatua ya kusema, hajui kama “atakuja kupatikana” kiongozi mwingine wa aina na uwezo kama wake, kuendeleza kazi na miradi aliyoanzisha kutoka pale atakapokuwa ameachia – kumaliza ngwe yake (2025).
Kauli hiyo, tena ya mara kwa mara, na nyingine za aina hiyo, ziliibua maoni mbalimbali. Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi alikuwa wa kwanza kusema hadharani kuwa ingekuwa vema kama Katiba ingekuwa inaruhusu Magufuli “atawale maisha.” Wabunge watatu wa Chama Cha Mapinduzi nao wakajiunga kwenye mnyororo wa kutaka Magufuli atawale milele.
Kitendawili kisichoteguka
Nani ajuaye – bila tuhuma za uwongo wala visingizio rejareja – kuwa sheria hii na nyingine za kibabe – za kunyakua uhuru wa waandishi wa habari, uhuru wa habari na haki ya uhuru wa kupata taarifa na kutoa maoni – hazikuwa nyuma ya mradi wa kuzima watakaopinga muda wa nyongeza kwa rais? Nani ajuaye? Atuwekee hapa.
Kwa kuangalia vema mfumo na hoja hii ya Ithibati, hebu tusemezane juu ya mfano huu wa jumla:
Serikali nyingi duniani zimekuwa zikituhumiwa utovu wa utawala wa sheria, kutozingatia haki za binadamu, kulea na kushiriki ufisadi; ufujaji mali ya umma na kutowajibika.
Sasa katika mazingira ya aina hii, iko wapi serikali ya kumpa mwandishi wa habari aliyejipambanua kuwa wa uandishi wa kina – wa kuchunguza, kufukua, kuchakata, kuchambua na kuanika; na anayefahamika hivyo – “leseni” ya uandishi wa habari? Iko wapi?
Ndimara Tegambwage ni mwandishi wa habari Tanzania kwa zaidi ya miaka 40; mhariri na mmiliki wa gazeti la RADI,(lilifungwa na serikali), na mwandishi wa zaidi ya vitabu 20 vikiwemo Uhuru wa Habari kitanzini, Uhuru gerezani na Who Tells the truth in Tanzania? Ni mlezi wa waandishi wa habari na mpigania Uhuru wa Vyombo vya Habari. Ndimara ni mshindi wa Tuzo ijulikanayo kama Lifetime Achievement in Journalism Award (LAJA) mwaka 2022 ya Baraza la Habari Tanzania (MCT).







