MWANDISHI mkongwe, Ndimara Tegambwage, amezua mjadala mzito mitandaoni kupitia makala yake fupi: “Tabasamu la Waandishi wa Habari: Ni la Moyo au Shuruti?” akichambua tabasamu linaloonekana usoni mwa waandishi wa habari wanaokabidhiwa kadi mpya za uandishi wa habari (digital press cards).
Kwa Tegambwage, tabasamu lina maana kubwa kuliko sura iliyojaa bashasha. Kwa kawaida, tabasamu ni taswira ya furaha ya kweli, inayotoka ndani ya moyo baada ya kuguswa na kitu chenye maana kwa mhusika.
Lakini yeye anahoji: “je, tabasamu la waandishi waliopokea vitambulisho hivyo ni la moyoni, au ni la kulazimishwa na mazingira?”
Tegambwage anatofautisha aina mbili za tabasamu: lile halisi linalotokana na mguso wa hisia chanya, na lile la maigizo, ambalo anaita “tabasamu-kazi” – linalotokana na shuruti au matarajio ya kijamii.

Kwa mantiki hii, anaongeza swali: “je, tabasamu la wale waliopokea vitambulisho ni la kweli au ni ishara ya kugandishwa na hofu ya mamlaka?”
Mfumo wa Kutoa Press Cards
Uchambuzi wa Tegambwage unagusa moja kwa moja mfumo uliopo Tanzania wa utoaji wa vitambulisho vya waandishi wa habari. Kijumla, nchi nyingi duniani kote zinafuata mifumo mbalimbali ya kutoa press cards.
Kuna mfumo wa vyama vya waandishi wa habari au mabaraza ya kitaaluma, unaotumika kwa wingi barani Ulaya, hususan nchi za Skandinavia, Ujerumani, Uholanzi, Uingereza na Ireland.
Kuna mfumo wa kiserikali, ambao Tanzania imeuchagua, ambapo mamlaka ya utoaji vitambulisho yapo mikononi mwa dola.
Kuna mfumo shirikishi, unaohusisha serikali, taasisi za kitaaluma na sekta ya habari, kama ilivyo Ufaransa, Italia, Ubelgiji na Austria.
Na upo mfumo wa kimataifa – kupitia International Press Card (IPC) ya Shirikisho la Vyama vya Waandishi wa Habari Duniani (IFJ), inayotolewa kwa wanachama wa vyama vya kitaifa vilivyo chini ya IFJ.
Mfumo huu wa Tanzania unashabikiwa na wale walio na imani na serikali katika kusimamia kila nyanja, ikiwemo tasnia ya habari.
Lakini kwa wanaoamini kwamba serikali nayo inapaswa kumulikwa na vyombo vya habari hivyo hivyo, mfumo huu ni hatari. Unaifanya Serikali kubaki kuwa mwamuzi, mwandishi na mshindani kwa wakati mmoja.

Mtazamo wa Kimataifa
Uzoefu wa kimataifa unaonesha kwamba pale ambapo serikali pekee hudhibiti utoaji wa press cards, mara nyingi vitambulisho hivyo hubadilika kutoka kuwa zana za kitaaluma hadi kuwa nyenzo za udhibiti wa habari.
Nchini Misri na Uturuki, kwa mfano, waandishi wa habari waliokosana na serikali walipokonywa vitambulisho vyao, jambo lililowaondolea hadhi ya kitaaluma na kuzuia shughuli zao.
Nchini Urusi, press card inayotolewa na mamlaka za serikali imekuwa kigezo cha kubagua waandishi wa habari wa vyombo visivyopendwa na watawala, na mara nyingine hutumika kama silaha ya kuzuia upatikanaji wa taarifa.
Kwa upande mwingine, katika nchii za Skandinavia na Ujerumani, ambapo vyama vya waandishi hutoa vitambulisho, waandishi hujihisi huru zaidi, kwa kuwa hadhi yao haitokani na ridhaa ya serikali bali hutokana na ithibati ya taaluma.
Mfumo shirikishi, unaohusisha serikali na wadau wa habari, umethibitika kutoa usawa zaidi kwa sababu unajenga uwajibikaji wa pande zote, huku ukizuia matumizi mabaya ya mamlaka.
Nafasi ya Wadau wa Habari
Kwa miaka mingi, wahariri na vyama vya waandishi wa habari nchini Tanzania wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba jukumu la kutoa ithibati kwa waandishi wa habari linapaswa kuwa mikononi mwao, si serikali.
Hii ndiyo hoja inayosukumwa pia na Tegambwage katika andiko lake. Ikumbukwe, Tegambwage ni miongoni mwa waasisi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA), na ni mwandishi wa kitabu “Uhuru wa Habari Kitanzini.”
Kwa Tegambwage, tatizo si press card zenyewe, bali mfumo unaozizalisha. Na tabasamu la waandishi wa habari wanaozipokea ni kioo cha taswira hiyo ya mfumo. Ama ni furaha ya kweli ya “kutambuliwa,” au ni tabasamu la “shuruti” la kuonesha utii.
Kwa hiyo, hoja hii ya Tegambwage ni mwaliko wa mjadala mpana juu ya mustakabali wa uhuru wa habari nchini Tanzania. Haipaswi kupuuzwa. Badala yake, inahitaji kujadiliwa kwa uwazi, bila hofu wala mzaha.
Kwanini? Kwa sababu, hatimaye, si tabasamu pekee linalohesabika, bali mfumo unaotengeneza tabasamu hilo.