JUZIJUZI niliandika ninavyoona tabasamu kwenye nyuso za waandishi wa habari wanaokabidhiwa Press Card kidijiti.
Tabasamu? Sura iliyojaa furaha, bashasha na uchangamfu. Ni kung`ara na kuwaka uso kwa furaha bila kucheka kwa sauti. Ni kumetameta. Aliye mbele yako aweza kuona hali uliyomo na hata kuuliza: Mbona kama unaongea peke yako na tabasamu pana?
Tabasamu huonwa haraka. Ni kwakuwa hupatikana kwenye uso. Miongoni mwa viungo muhimu vioneshavyo tabasamu haraka ni pamoja na macho, mdomo na pua. Kadri sehemu mbalimbali za ubongo zinavyoamuru mishipa ya usoni, ndivyo viungo hivi hufinyanga ujumbe – kwako na kwa anayekuangalia – na kutoa tafsiri ya hisia zako za kimyakimya.
Utashangaa. Ukimlazimisha mtu kuwa na tabasamu; basi badala ya kutabasamu, atagegema. Kugegema ni kuleta uso (sura) yenye mchanganyiko wa furaha iliyominywa; huzuni, mshangao, shaka, woga na hata majuto.
Katika mazingira haya basi, Kitambulisho – ile press card kidijiti – inatabasamisha waandishi wa habari; yenyewe inatabasamika na waandishi wanaitabasamia. Kawaida msukumo wa kutabasamu huja wenyewe – kwa mtu, kitu, tendo fulani au mategemeo/matarajio.
Jongea kwa hesabu hii: Ili kuwepo tabasamu halisi, sharti kuwepo kitabasamika ambacho ni kitabasamishi na kina watu wa kukitabasamia. Hapa unapata tabasamu halisi.
Tabasamu halisi huja kwa ridhaa ya MGUSO. Umeguswa wapi. Umeguswa vipi. Umeguswa kiasi gani na kile unachoona na kusikia wakati huo; unachotamani, ulichotarajia; ulichoahidiwa, unachofikiria au unachopewa. Unakuta tabasamu linasambaa uso mzima, hata ukiwa peke yako.
Tabasamu ni zao la hisia chanya. Halizuiliki. Huishi katika ngome ya MGUSO ambako huwezeshwa na sehemu mbalimbali za ubongo kwa kutoa amri kwa mishipa ya uso kupwa na kujaa – kufuatana na unachoona, unachosikia au unachotarajia; na kulingana na unavyoguswa.
Lakini kuna Tabasamu-kazi. Tabasamu lisilohalisi wala asili. Tabasamu la kuchonga. Tabasamu la kukidhi haja kwa mazingira yaliyopo na bila kelele. Tabasamu la kufinyanga kwa shabaha ya maigizo. Sababu za kulifinyanga zikiisha – na mara nyingi hunyauka haraka – unakuwa mwisho wa tukio na tabasamu lenyewe.
Je, katika mazingira ya waandishi wa habari Tanzania, ambao wanapokea press card kidijiti kwa tabasamu; na mwakilishi wa Ithibati anayewakabidhi vitambulisho – lile tabasamu tunaloona – ni halisi na linatoka kwenye ngome ya MGUSO?
Tunaweza kujibia waandishi kwamba hisia zao zimeganda kwenye kukabidhiwa kitambulisho na “kutambuliwa” na “kuthibitishwa.” Je, tabasamu la mkabidhi kitambulisho linatokana na nini? Kwamba biashara imejibu au “wajinga ndio waliwao?”
Tunaweza kujadiliana. TUSEMEZANE.