KURA YAKO INA THAMANI

KURA yako ina nguvu. Ina thamani. Usipoitumia, basi nguvu yake na thamani yake vinakufa ukingali hai. Njia pekee ya kulinda kura yako, na kwa “wivu mkubwa,” ni kuitumia kufanya uchaguzi; na hapo ndipo huongezeka thamani. Mshindi hapatikani bila kura ya aliyemshindisha au aliyempinga. Umuhimu wa tarakimu!

Hata kama uliyechagua hakushinda, utaratibu na matokeo vanakupa data juu ya nafasi yako; kustuka na, au hata kushangaa. Inakuelekeza katika hatua nyingine: nifanye nini, nifanye vipi, nifanye wapi, nishirikiane na nani.

Utaratibu wa kupiga kura, umebaki kwa sasa kuwa njia pekee na salama ya kupata viongozi na watawala. Wanaochimba mikwara, mashimo na maandaki katika njia hii – kwa kuendesha utawala wa vitisho na ufujaji mali ya umma – ndio wanatafuta kuangamiza nguvu na thamani ya kura na katika mazingira ya sasa ya kistaarabu duniani.

Kinachokosekana, kwa mfano katika mazingira kama ya Tanzania, ni kuwezesha kila raia mwenye umri wa kupiga kura, kujua umuhimu na nguvu ya kura yake; na haki yake binafsi ya kutumia kura hiyo kuamua: ninataka hiki, sitaki kile. Ninataka huyu, sitaki yule. Ninataka huku, sitaki kule!

Kwingine ambako wengi wana ufahamu mpana; wametambua nguvu na thamani ya kura yao, kuna kujiamini. Kuna ujasiri. Hawayumbishwi na hongo za “nipe-nikupe” au zozote zile; wala hawawi chawa. Wakipata taarifa sahihi, wakakutana, kujadiliana na kukubaliana – chini ya vyama vyao au mifumo mingine – waweza kufanya wingi wa kura zao kuwa chimbuko la nguvu na utawaa wao.

Kwanza, nguvu ya kura ni usiri wake – nani ajuaye ya moyoni? Nguvu ya pili ni maarifa juu ya umuhimu wake. Nguvu ya tatu ni utambuzi wa kile ambacho mtu binafsi na jamii wanataka na sharti kipatikane kwa mwafaka wa wengi na kwa manufaa ya wote (uamuzi na mamlaka). Nguvu ya nne ni kushikilia – bila kuachia – msingi wa nguvu zao katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1975), inayosisitiza umuhimu wa uwakilishi wa wananchi na uwajibikaji wa viongozi/watawala.

Aidha, Ibara 124 ya Katiba inatamka kuwa mamlaka ya dola inatoka kwa raia ambao, kwa nguvu ya kura, ndio wanachagua watawala wao. Nguvu hii ya kura huweza kuweka, kubadili, kugeuza, kuondoa au kurejesha kile ambacho kura ya awali ilirasimisha.

Juhudi za kutoa, kusambaza, kukuza elimu na maarifa juu ya nguvu hizi za kura miongoni mwa raia, katika jamii zote; ndizo zinahitajika zaidi. Hii ni kwa njia yoyote ile – matangazo, nyimbo, mashairi, mijadala, hotuba, barua, simu, maongezi ya ana kwa ana, taarifa za vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Bila kukoma.

Hatimaye raia wataelewa na kuthamini nguvu yao na thamani ya kura yao. Linda kura yako – nguvu yako ya utawala – kwa kupiga kura. Tukumbushane: Kura siyo karatasi. Kura ni utashi binafsi unaotafsirika kwa tarakimu: mtu mmoja kura moja. Usijiweke gerezani.

Ndimara Tegambwage ni mwandishi wa habari Tanzania kwa zaidi ya miaka 40; mhariri na mmiliki wa gazeti la RADI,(lilifungwa na serikali), na mwandisi wa zaidi ya vitabu 20 vikiwemo  Uhuru wa Habari kitanzini, Uhuru gerezani na Who Tells the truth in Tanzania? Ni mlezi wa waandishi wa habari na mpigania Uhuru wa Vyombo vya Habari. Ndimara ni mshindi wa Tuzo ijulikanayo kama Lifetime Achievement in Journalism Award (LAJA) mwaka 2022 ya Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Like
2