TUMEISHINDWA KARIAKOO?

KATIKA soko maarufu la Kariakoo jijini Dar es Salaam, hali ya sintofahamu imegubika biashara huku wafanyabiashara wazawa wakilalama kuzidiwa na wageni, hususan Wachina, wanaodaiwa kutawala kila hatua ya mnyororo wa biashara.

Hili si suala la Tanzania pekee, bali linajitokeza kwa namna mbalimbali katika nchi nyingine barani Afrika kama Zambia, Nigeria, Uganda na Kenya, ambako biashara za Wachina zimezua mjadala mkali kuhusu ushindani usio wa haki.

Takwimu zinazotia shaka

Ripoti ya Kamati Maalum ya Bunge iliyochunguza biashara za wageni Kariakoo kuanzia Februari mwaka huu, ilifichua mambo mazito. Mojawapo ya mambo yaliyogunduliwa ni kuwa kati ya kampuni 9,380 zilizosajiliwa BRELA, ni asilimia 9.2 pekee ndizo zilizosajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Hii inaashiria uwepo wa mianya inayoruhusu wageni kusajili kampuni kwa njia ambazo huenda zinakwepa miongozo ya uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni.

Vile vile, kamati hiyo iligundua pia kuwa:

– Wageni wanauza bidhaa kwa bei ya chini ya soko, jambo linalowamaliza wafanyabiashara wazawa.

– Wanaondoa wazawa katika maeneo ya biashara kwa kulipa kodi kubwa na “kilemba”, malipo ya ziada yanayowanyima wazawa nafasi ya kuendelea.

– Wanamiliki mnyororo mzima wa thamani, kutoka kuagiza bidhaa, kutoa bandarini hadi kuzipeleka kwa mlaji, yote kupitia kampuni zao.

– Watanzania wanatumika kama “madummy owners” huku wageni wakitawala biashara nyuma ya pazia.

“Hili ni bomu linalosubiri kulipuka,” alisema mfanyabiashara mmoja wa mitumba aliyekataa kutajwa jina lake kwa kuhofia usalama wake. “Hatuwezi kuhimili ushindani huu, wanachukua kila kitu.”

Malalamiko sawa Afrika nzima

Hali kama hii imeripotiwa Zambia ambapo serikali ya Rais Hakainde Hichilema ililazimika kuchukua hatua dhidi ya maduka ya Wachina yanayofanya biashara za rejareja. Kenya nayo ilikumbwa na malalamiko makubwa mwaka 2022 baada ya Wachina kuanza kuuza bidhaa sokoni moja kwa moja kwa walaji, jambo lililosababisha maandamano ya wafanyabiashara wazawa.

Uganda nayo imeshuhudia makundi ya wafanyabiashara wakiandamana kupinga “biashara ya rejareja kwa wageni.” Na Nigeria, serikali imeanzisha kampeni ya kuwachuja wageni wanaofanya biashara ndogondogo kinyume cha sheria.

Wachina washika hatamu

Hadi sasa, Wachina wanatajwa kuwa wamechukua “pande kubwa zaidi” la biashara Kariakoo. Wamiliki wengi wa maduka makubwa, maghala, na hata mitandao ya uagizaji bidhaa ni raia wa China.

Mmoja wa wafanyabiashara wazawa alisema, “Siku hizi hata ukitaka kuuza vitenge Kariakoo, lazima ununue kwa Wachina, wao ndio wanaagiza kwa bei ya chini na wanapanga bei sokoni.”

Mianya na udhaifu wa udhibiti

Kamati hiyo pia imebaini kuwa:

– NIDA za Watanzania zinatumiwa kufungua kampuni huku wenyewe wakiwa wafanyakazi au vibarua wa kampuni hizo.

– Maduka 8 kati ya 10 hayakutoa risiti, moja ilitoa ya kughushi.

– 29 ya maduka ya mtandaoni hayakusajiliwa wala kupata leseni, 12 kati ya majukwaa 14 ya kibiashara mtandaoni hayakuwa na leseni.

– Wageni 148 kati ya 152 waliokutwa wameajiriwa Kariakoo walikuwa wauzaji wa bidhaa za rejareja, jambo lililo kinyume cha sheria za ajira na uwekezaji.

Je, seeikali tachukua hatua?

Katika hali ya kushangaza, ripoti hiyo pia imedai kuwa baadhi ya maafisa walipokea simu za kuwataka wasitishe uchunguzi, jambo linaloashiria uwepo wa ushawishi mkubwa nyuma ya pazia.

“Huu si uwekezaji, huu ni uvamizi wa kiuchumi,” alieleza kijana mmoja anayefanya biashara ya vifaa vya simu. “Tunataka serikali iangalie upya sheria hizi za biashara kwa wageni. Wanatubana na kutumaliza.”

Wakati uwepo wa wawekezaji wa kigeni unaweza kusaidia kukuza uchumi, ushahidi unaoibuka kutoka Kariakoo unaonyesha kuwa kuna hatari ya kugeuka “ukoloni wa kiuchumi mpya.” Bila mifumo imara ya udhibiti na utekelezaji wa sheria, biashara za ndani zinaweza kudidimia kabisa, na mapambano ya uchumi wa chini yakageuka kuwa vita vya kuishi.

Je, serikali ya Tanzania itaingilia kati kwa haraka kama ilivyofanya Zambia na Kenya? Au Kariakoo itabaki kuwa uwanja wa biashara wa wachache wenye nguvu za mtaji kutoka mbali?

Like