NIMESIKIA mara nyingi baadhi ya wachambuzi wakitoa hoja kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anahujumiwa makusudi na watu walio karibu naye au wanaonufaika na zogo la kisiasa nchini.
Kwa haraka, hoja hii inaweza kuonekana kama nadharia ya njama, lakini matukio ya hivi karibuni yanaleta uzito mpya kwa hoja hii. Nitataja machache.
Wakati wa sherehe za Idd, mwezi uliopita, hotuba ya Rais Samia ilijaa shutuma dhidi ya viongozi wa dini. Alisema: “mchelea mwana kulia hulia yeye.”
Hotuba hiyo sasa inasambazwa mitandaoni, na baadhi ya watu wanaitumia katika muktadha wa shambulio dhidi ya Padre Charles Kitima lililofanyika jana Kurasini, Dar es Salaam. Fuatilia maelezo haya.
Fr. Kitima, katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), ameshambuliwa siku ambayo TEC ilikuwa na kikao na viongozi wa juu wa BAKWATA, TEC na CCT. Kikao hicho kilikuwa na mpango wa kumwona Rais Samia ili kuzungumzia hali ya nchi kuelekea uchaguzi mkuu.
Taarifa zinasema kuwa mmoja wa washiriki wa kikao hicho alisaliti wenzake, akatoa taarifa kwa afisa usalama mmoja (ambaye ametambuliwa kwa jina la Kayombo). Ndipo watu wakatumwa kufuatilia mambo haya huko TEC Kurasini, ambako Fr. Kitima alivamiwa.
Wakati kikao cha TEC kinaendelea, maafisa wawili wa usalama – (Kayombo na Mkude) – walitumwa na mkuu wao (ajulikanaye kama Fadhili) kukutana na Waziri innocent Bashungwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Baada ya kikao hicho, Bashungwa alitoa tamko akitaka polisi washughulikie “matishio” yote bila woga.
Fr. Kitima aliwekwa kwenye orodha ya watu wanaotajwa kuwa “hatari kwa amani ya nchi.”

Mwaka jana mwanzoni, afisa mmoja aliyedaiwa kutoka Ikulu, alimwendea mmoja wa wakuu wa TEC akamwambia kuwa Rais Samia amemtuma aiombe TEC imwondoe Fr Kitima kwenye nafasi yake ili maridhiano kati ya TEC na serikali yaweze kukamilika.
Mkuu huyo wa TEC alifikisha ujumbe kwa maaskofu. Walichukia sana na kuamua kumbakiza Fr. Kitima kwa kipindi kingine.
Baadaye, Rais Samia alipelekewa taarifa na watu wake kuwa waliokuwa wanamchonganisha na TEC ni Waziri Angelina Mabula na Makamu wa Rais Dk. Phillip Mpango.
Baada ya Mabula kuondolewa kwenye baraza la mawaziri, tetesi zilisema kuwa hayo yalikuwa matokeo ya ujumbe ambao wapambe walikuwa wamempelekea rais. Baadaye zikaanza kusikika habari kuwa makamu wa rais anatengwa kabisa kiasi cha rais kubadili baraza la mawaziri bila kumhusisha.
Zikasikika tetesi nyingine kuwa wapambe wa DP World walianza kutamba hadharani kuwa “TEC wamekuwa wanajifanya miungu watu, ila safari hii watakoma.” Taarifa zinasema kuwa hata pale Rais Samia aliposubirisha utekelezaji wa mkataba wa DP World, wafanyabiashara wenye maslahi walimshauri: “Ukiacha, TEC watajiona wanakuendesha.”
Miongoni mwa wapambe wa rais wamo ambao wamekuwa wakimwambia mara kwa mara kuwa, “Maaskofu hawana tatizo nawe, bali ni Fr. Kitima tu kwa sababu anatoka mkoa mmoja na Lissu.”
Kwa vyovyote vile, hii linaonekana kama jaribio la kuchafua uhusiano wa serikali na taasisi za dini. Jambo hili linamomonyoa imani ya waamini wa dini mbalimbali kwa Rais Samia
Lipo na hili la kesi ya Tundu Lissu. Katika mwaka huu wa uchaguzi, kiongozi wa upinzani amekamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini. Kwa maelezo ya kawaida, hizi ni juhudi za mgombea mmoja (Samia) kumwondoa mgombea mwingine mtarajiwa (ambaye hata hivyo, amesema chama chake hakitashiriki uchaguzi bali kitauzuia). Hii inamletea Samia taswira ya dikteta kuliko kiongozi mwanademokrasia.
Kwa sababu ya taswira hii, mitandaoni, baadhi ya watu, hata wanaCCM wenzake, wameanza kupendekeza CCM kitafute mgombea mwingine mwenye mvuto wa kisiasa (kuliko Samia) kabla ya muda kuisha.
Ukatili uliofanywa na vyombo vya dola siku ya kesi ya Lissu nao umemwongezea doa. Baadhi ya wafuasi wa CHADEMA walizuiwa kufika mahakamani, wakapigwa, wengine wakalawitiwa, na picha zao zikasambazwa. Wapo baadhi ya washauri wa rais waliomshauri akae kimya, naye akakubali.
Sasa baadhi ya wanachama wa chama chake na watumiaji wa mitandao ya kijamii wanasema kimya hicho ni ishara kuwa aliidhinisha mateso hayo.
Aidha, taarifa zinasema Bashungwa alisisitiza kuwa kesi ya Lissu isikilizwe kwa njia ya mtandao hata kabla ya uamuzi wa mahakama kutolewa rasmi. Tafsiri ya haraka ni kuwa uhuru wa mahakama katika kushughulikia wakosoaji wa serikali umeshaingiliwa.
Kwa mtazamo huu, mbele ya macho ya wengi, Rais Samia anaonekana ni dikteta anayepuuza sheria.
Hata katika hotuba yake kwa taifa, alichomekewa suala la kuunganisha mihimili ya dola. Hii ni kinyume cha katiba. Ni jaribio jingine la kuondoa uhuru wa Bunge na Mahakama.
Kitendo hiki kinamwingiza Rais Samia katika orodha ya viongozi wanaotamani mamlaka ya kifalme au kimalkia.
Lipo na hili na vitendo vya utekaji na mauaji vinavyoripotiwa nchini. Vinaelezwa kuwa vinatokana na baadhi ya watu kumshauri Rais Samia kwamba watu hao ni tishio kwake. Na zipo taarifa kuwa baada ya kuwaua, wasaidizi wake humweleza kwamba wahusika wanahojiwa au wameachiwa.
Hii inaweza kueleza, kwa mfano, sababu ya kimya cha rais katika kutekwa na kuuawa kwa wanaharakati na wanasiasa kadhaa, wakiwemo Deusdedit Soka na wenzake, na Ali Kibao.
Wengine wameenda mbali hata kudai wana ushahidi wa maagizo ya rais, na kwamba umetunzwa na watu walio karibu naye. Baadhi yao wameanzisha mchakato wa kuandika kitabu kuhusu maelekezo hayo kwa kushirikiana na mwandishi aliye uhamishoni.
Hata suala la mkataba wa DP World linatajwa, kwamba limesababisha sintofahamu. Inadaiwa kwamba baadhi ya viongozi, akiwemo makamu wa rais na waziri mkuu, walitengwa katika uamuzi na ushauri kwa Rais Samia.
Wanamtaja mtu anayehusishwa kuwa na ushawishi mkubwa kwa rais, ambaye ni mfanyabiashara maarufu, kwamba alihusika moja kwa moja kwenye mchakato huo, na kwamba ukaribu huo wa kipekee unaweza kumuumiza rais mwenyewe kisiasa.
Kwa ujumla, mwelekeo wa matukio haya unamuacha Rais Samia katika nafasi tata kisiasa. Iwapo kweli anahujumiwa, basi ni wazi kuwa baadhi ya watu ndani ya mfumo wake wanaendesha mikakati ya kumharibia taswira, kutisha wapinzani, kuingilia mihimili ya dola na kumwondolea uhalali wa kisiasa mbele ya wananchi. Wachambuzi wa kisiasa wanasema kuwa hali hii isiporekebishwa, itakuwa na athari mbaya kwake kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Swali: Je, haya yanatokea kwa kuwa anahujumiwa? Kama hahujumiwi, ina maana haya yanafanyika kwa idhini yake. Je, ndiyo maana hakuna hatua zinazochukuliwa? Kama ndivyo, wanaodai anajihujumu mwenyewe wamekosea?