Chadema yaingia Mara kwa kishindo

– Mbowe aibuka na ‘Dira ya Maendeleo Vijijini’
– Lissu akemea mauaji, ukandamizaji raia jirani na hifadhi

BAADA ya mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga na Simiyu, leo Oparesheni +255 ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeingia mkoa wa Mara, kwa kuanzia Bunda Mjini, ambapo viongozi wakuu wa Chama hicho, Mwenyekiti Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu, wamepata mapokezi makubwa.

Wakihutubia umati wa wananchi wa Bunda mjini, Mbowe alizungumzia zaidi umaskini na ukiukwaji wa haki wanaofanyiwa wananchi wa vijijini, huku Lissu akizungumzia zaidi mauaji wanayofanyiwa Watanzania wote washio jirani na maeneo ya hifadhi, ikiwemo hifadhi ya Serengeti.

Mbali na kupokewa kwa nderemo nyingi, viongozi hao wakuu wa Chadema, wamezawadiwa ng’ombe na mbuzi kutoka kwa wazee wa Nyatwali na Bunda mjini.

Lissu akimpokea Mbowe alipowasili kwenye mkutano wa hadhara Bunda Mjini

Akinadi ‘Dira ya Maendeleo Vijijini‘ chini ya Serikali itakayoongozwa na Chadema, Mbowe, akiwa maeneo ya Shigala, Dutwa, Sapiwi, Hunyari na baadaye Bunda Mjini, amesema kwenye mikoa yote nane waliyopita mpaka sasa, Chama hicho kimethibitisha kukithiri kwa umaskini vijijini na ukandamizaji mkubwa wa haki za wananchi, huku serika ikivitelekeza vijiji kwenye miradi ya maendeleo.

Kwamba, pamoja na kuwa umaskini upo nchini kote, lakini hali inatisha zaidi vijijini, wanakoishi asilimia 70 ya Watanzania.

“Mijini angalau kuna barabara za lami, lakini vijijini kwenye watu wengi, wanakolima chakula kinacholisha nchi, barabara ni mbovu.

“Wakati angalau baadhi ya maeneo ya mijini yana mtandao wa maji safi ya bomba, zaidi ya 60% ya vijijini vya mikoa yote tuliyopita, wana shida ya kutisha ya maji.

“Mkoa wa Simiyu, kwa mfano, wananchi wanachimba maji kwenye mchanga uliopo kwenye mito iliyokauka.

“Watashia kupata maji machafu yenye rangi ya maziwa. Na wanalazimika kunywa maji hayo pamoja na mifugo yao. Hiyo ndiyo hali halisi ya Tanzania yenye ziwa Victoria, ziwa la pili kwa ukubwa duniani kwa kuwa na maji baridi yanayofaa kunywa. Hiyo ndiyo Tanzania yenye madini, gesi asilia, mbuga za wanyama na raslimali nyingi, chini ya miaka 62 ya uhuru na utawala wa CCM. Hali hii haikubaliki. Ni lazima tufanye mabadiliko ili tuwakomboe Watanzania wote hasa wa vijijini,” alisema Mbowe.

Mbowe akihutubia wa Bunda

Alieleza kuwa kwasababu ya sera mbaya za CCM, Watanzania wa vijijini wameishia kutumika tu kama wazalishaji wa mazao ya chakula na biashara pamoja na mifugo na uvuvi, huku wakinyima haki ya kufaidi bajeti ya Taifa, kwani zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya nchi, imekuwa ikielekezwa mijini zaidi.

Kwamba, mbali na uzalishaji wa mazao, watu wa vijijini wamekuwa wakinyonywa kwa kutozwa kodi na ushuru mwingi, huku wakilazimishwa kuuza mazao yao kama Pamba na Kahawa kwenye soko la ndani kwa bei ndogo na hivyo kunyimwa kabisa fursa ya kujikwamua na umaskini.

Katika mikoa ya Geita, Shinyanga, Mwanza na Simiyu, inayolima pamba, wakulima wanakatwa takribani shilingi 1,000 katika kila kilo moja ya pamba, hali inayosababisha wapate shilingi 1,060 kwa kilo badala ya 2,040.

Makato hayo ni zaidi ya 50% ya pesa yote wanayopaswa kulipwa kwa kila kilo moja ya pamba.

Makato hayo yanazidi makato ya 18% ya kodi la Ongezeko la Thamani (VAT).

Mbowe aliendelea kuchambua hali ya umaskini vijijini, akisema kuwa kanda ya ziwa imejaliwa kuwa na madini mengi hususan dhahabu, lakini sera mbaya za CCM, zimewatenga na kuwabagua Watanzania wasinufaike na madini yao.

Migodi yote, mikubwa na midogo, imelalamikiwa kugawiwa kwa wageni.

“Nimekwenda kijiji kinaitwa Mwakitolyo, jimbo la Solwa. Mungu aliamua kuwapa Mwakitolyo ardhi yenye dhahabu ili iwakomboe. Kulikuwa na wachimbaji wadogo waliokuwa wanachimba dhahabu na kujipatia riziki. Sasa nimefika kule nimekuta vilio, nimekuta msiba.Wananchi wanalia kwasababu serikali imeamua kuwaondoa na kuwapa Wachina migodi ile wawe wachimbaji wadogo wadogo. Ujinga gani huu…leo Mtanzania ukienda China huwezi hata kuruhusiwa kuuza “Big G” (Bazoka), lakini hapa CCM inawapa dili la kuwa wachimbaji wadogo,” alisema Mbowe.

Wananchi wa  Kata ya Dutwa wakimsikiliza Mbowe

Aidha, leo asubuhi akiwa Kata ya Dutwa, Bariadi Vijijini, Mbowe alielezwa kuwa shida kubwa kuliko zote ni vijana wa Kitanzania waliokuwa wachimbaji wadogo wa madini, kuondolewa kwenye migodi kwa madai kuwa maeneo yote waliokuwa walichimba yana leseni ya kuchimbwa na Wachina.

“Mheshimiwa Mwenyekiti,  huko nyuma mji huu wa Dutwa ulikuwa umechangamka sana, kwasababu ya wachimbaji wadogo wa madini, lakini sasa umepooza kwasababu maeneo yote wamepewa wachina,” alisema Maendeleo Makoye aliyekuwa mgombea ubunge wa Chadema, Jimbo la Bariadi Vijijini katika uchaguzi mkuu wa 2020.

Makoye aliungwa mkono pia na maelfu ya wananchi wa Dutwa waliohudhuria mkutano huo.

Wakati serikali ya CCM ikilalamikiwa kuwatenga wachimbaji wadogo wa Kitanzania na kugawa migodi yote kwa wageni, Sera ya Chadema ya Madini, pamoja na mambo mengine, imeahidi kuwalinda na kuwapati wachimbaji wadogo wadogo. Kitanzania, kwa kuwapatia mikopo ya kuwawezesha kununua mashine na zana bora za uchimbaji zinazotumia teknolojia ya kisasa ili wapate madini mengi na kubadilisha maisha yao.

Vile vile, Sera ya Madini ya Chadema, imeahidi kujenga uwezo wa kitaasisi na kitaalam kwa wachimbaji wadogo wa Kitanzania na kuhakikisha kunakuwa na ubia baina ya wenyeji na makampuni ya kigeni ili wanufaike moja kwa moja na madini..

Akihitimisha Ajenda hiyo ya Maendeleo Vijijini, Mbowe alisema kuanzia sasa Chadema imeamua kwa makusudi kuongeza kasi ya asi ya kuwasemea shida zao wananchi wa Jijini, huku akiahidi kuwa Chadema itafanya mageuzi makubwa ya kuboresha uchumi na hali za maisha ya watu wa vijijini kwa kuelekeza sehemu kubwa ya bajeti ya nchi pamoja na usimamizi wake kwenye katika kugharamia maendeleo vijijini.

Kwa upande wake, Lissu alilaani vikali wimbi la wananchi wanaoishi jirani na hifadhi za wanyamapori kuhamishwa kwenye maeneo yao ili kupisha wawekezaji huku wengine wakiuawa wao na mifugo yao, wakidaiwa kuingilia maeneo ya hifadhi.

Akitoa mfano, Lissu alisema wananchi wa eneo la Nyatwila, Bunda, ambako kuna ziwa lililo jirani na hifadhi ya mbuga ya Serengeti, wamekuwa wakipelekewa huduma za kiserikali ikiwemo umeme, lakini sasa wametakiwa waondoke kwenye eneo hilo kwa madai kuwa ni sehemu ya hifadhi.

Lissu alisema kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha hifadhi ya Serengeti, mipaka ya Serengeti haifiki kwenye ziwa hilo, lakini serikali imeamua kuwaondoa wananchi 13,500, kwa makusudi, ili iweke wawekezaji watakaojenga hoteli za watalii.

“Wananchi maelfu kwa maelfu wanaondolewa katika maeneo yao isivyo halali ili serikali ipanue mipaka ya Serengeti. Ili wapewe wawekezaji wajenge hoteli za kitalii, ili watalii waweze kuona wanyama wakiwa katika ufukwe wa ziwa. Halafu fidia waliyoambiwa watalipwa ni shilingi milioni 2 kwa ekari moja. Na tayari nyumba zao zimechorwa ‘X’. Mipaka halisi ya mbuga ya Serengeti haifiki ziwani. Jambo hili halikubaliki,” alisema Lissu na kuongeza:

“Ukanda wote wa kuanzia Meatu, Kisesa, Itilima, Maswa, Bariadi, Bunda na Tarime, umekuwa ni uwanja vita baina ya wananchi na askari wa hifadhi. Watu wanafukuzwa kutoka kwenye maeneo yao waliyorithi kutoka kwa wazazi wao walioishi enzi na enzi, ili tu maeneo hayo wagawiwe wageni. Watu wanauawa siyo na wanyamapori tu bali pia na askari wa hifadhi. Wanauwawa wao na mifugo yao wakidaiwa kuvamia hifadhi.

“Kule kata ya Nkololo wameuwawa watu tisa kwasababu tu wamekutwa wanachunga ng’ombe. Mwatongo wameuwawa watu watano. Ni kinyume cha sheria kuuwa watu. Nchi hii ina makosa mawili tu yanayoruhusu mtu kuuwawa, na mpaka makosa hayo yathibitishwe na mahakama: ni kosa la mauaji ya kukusudia na uhaini. Sasa huku watu wanauwawa bila hatia. Hii ndiyo Tanzania ya Samia.”

Catherine RugeWaKanzaniMkuu wa BAWACHA, akisalimia wananchi Sapiwi, Bariadi Vijijini i

Lissu amewataka Watanzania wote kujiunga kwa wingi Chadema ili kuing’oa CCM na kukiiwezesha Chama hicho kuunda serikali itakayokomesha madhila yote wanayofanyiwa Watanzania wanaoishi kwenye maeneo ya hifadhi.

Like