IMETHIBITISHWA kuwa Balozi Dk. Pius Ng’wandu sasa atazikwa kesho, Jumatano, nyumbani kwake Makabe, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Uamuzi huo umetokana na wosia alioacha Dk. Ng’wandu, kwamba akifariki dunia azikwe pembeni mwa kaburi la mkewe wa kwanza, Lucy, aliyefariki miaka sita iliyopita.
Kabla ya familia kutambua kuwepo kwa wosia huo, kulitokea mgogoro kati ya watoto wake na mjane wake, Mary, aliyefunga ndoa naye Oktoba mwaka huu, kuhusu mahali pa kumzima marehemu Ng’wandu.
Mjane alikuwa amependekeza mwili wa mumewe uzikwe Maswa, eneo alikozaliwa na kukulia, ambako pia alikuwa mbunge kwa vipindi vitatu. Watoto walitaka azikwe Makabe pembeni mwa mama yao, wakidai alisema hivyo.
Baada ya kafariki, Desemba 18, 2020 katika Hospitali ya Mkoa wa Simiyu, Somanda, iliyoko Bariadi, baadhi ya ndugu wa marehemu walikubaliana na mkewe kwamba ni vema apumzishwe nyumbani kwao, badala ya kusafirisha mwili hadi Dar es Salaam.
Hata hivyo, watoto wawili wa marehemu waliamua kwenda Maswa kumaliza mzozo huo kwa kuonyesha wosia wa baba yao, kwamba alipendekeza azikwe Makabe, pembeni ya kaburi la mkewe wa kwanza.
Ibada ya kuuaga mwili wa Balozi Dk. Ng’wandu huko Maswa ilifanyika nyumbani kwake Mtaa wa Uzunguni Wilayani Maswa, mkoa Simiyu. Ilihudhuriwa na idadi kubwa ya waombolezaji. Jana mchana walianza safari kuelekea Dar es Salaam.
SAUTI KUBWA imeelezwa kwamba baada ya mwili wa marehemu kuwasili Dar es Salaam, shughuli zote za msiba zitafanyika nyumbani kwake, Kawe, Dar es Salaam – jirani na uwanja gofu wa JWTZ, kabla ya kupelekwa mazikoni Makabe, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.