Tume ya ya Taifa ya Uchaguzi yadaiwa kuongeza wapiga kura hewa

WATANZANIA wengi wamesikia malalamiko ya mgombea urais Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, akidai kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imeongeza majina ya wapigakura hewa 117,000 ili kusaidia ushindi kwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Mwinyi.

Pamoja na ukimya wa ZEC kuhusu tuhuma hizo, wananchi visiwani humo wanaamini ukweli katika hilo. Tume hiyo imekuwa ikikwepa kuzungumzia suala hilo na haionekani kuchukua hatua kufafanua jambo hilo mbele ya umma.

Upande wa Tanzania Bara, tuhuma kama hizo zimesikika kutoka kwa Mgombea Ubunge wa Arusha Mjini kupitia Chadema, Godbess Lema.

Akiwasilisha malalamiko yake kwa mkurugenzi msaidizi wa uchaguzi Arusha, Dk. John Pima, Lema amesema amegundua uwepo  wa idadi kubwa ya wapigakura hewa, ikiwa ni mpango wa kusaidia CCM kushinda jimbo hilo.

Akizungumza kwa hisia kali, Lema amesema daftari la kudumu katika Jimbo la Arusha Mjini lina wapigaura 240,000, lakini yeye na chama chake, jana walishtushwa kuona wapigakura 370,110 ikiwa ni ongezeko la wapigakura hewa zaidi ya 100,000.

Mgombea huyo amesema baada ya kumuuliza msimamizi  wa uchaguzi kuhusu ongezeko hilo, ambalo linatia shaka, msimamizi ameshindwa kutoa ufafanuzi. Badala yake amewataka viongozi wa Chadema kufika ofisini kwake kesho.

Tayari Lema ameandika barua jioni ya leo kwa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Dk. Wilson Mahera kulalamikia hali hiyo.

Mrisho Gambo, mgombea ubunge kutoka CCM Jimbo la Arusha, pamoja na timu yake, wanadaiwa kushirikiana na NEC na taasisi za usalama kuhujumu uchauzi huo kwa kuhakikisha Gambo anashinda.

Lema amedai kwamba aliingia ofisini kwa mkurugenzi huyo na kumkuta Mkuu wa Wilaya ya Arusha (DC), Kenan Kihongosi na Mkuu wa Usalama wa Taifa wa Wilaya (DSO), wakichambua fomu za mawakala.

Kanuni na sheria za uchaguzi hazimtaji popote mkuu wa wilaya  kuwa mmoja wa wasimamizi wa uchaguzi na hausiki na hatua zozote za mchakato wa uchaguzi. Hii inaelezwa na Lema kuwa uenda ulikuwa na nia ovu dhidi ya uchauguzi huo wa Arusha.

Dk. Pima amekataa kueleza lolote kuhusu tuhuma hizi, baada ya kupigiwa simu akieleza kwamba hana habari kama kulikuwa na mkutano wa kuhujumu uchaguzi huo unaofanyika Oktoba 28, 2020.

Kinachosemwa Arusha kimeripotiwa pia katika majimbo mengine nchini. Juzi, Katibu wa Chadema Misungwi, Mwanza, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa yeye na chama chake wamegundua idadi kubwa ya majina mapya katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Mbali na wapiga kura hewa tayari wananchi wameanza kugundua vituo vya kupigia kura hewa, kama video hii inavyoonyesha.

Like
3