Trump aaga Tanzania kwa “bakora la viza.” Azuia vigogo kusafiri Marekani kwa tuhuma za kuvuruga uchaguzi na uvunjaji haki za binadamu

TANZANIA imekuwa nchi ya mwisho kuonja makali ya Rais Donald Trump ambaye anaondoka madarakani rasmi kesho Januari 20. Siku moja kabla hajaondoka amewekea viongozi waaandamizi wa Tanzania vikwazo vya kuingia nchini humo.

Trump anaondoka Ikulu ya Marekani baada ya kushindwa uchaguzi na Joe Biden anayeapishwa kesho hiyo hiyo.

Taarifa ya Marekani iliyotolewa leo kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje, Michael Pompeo, inaeleza kuwa vikwazo hivyo vimewekwa kwa baadhi ya viongozi wa Tanzania baada ya kuthibitika kuwa walihusika kuvuruga mchakato wa uchaguzi. Wanatuhumiwa pia kukiuka haki za binadamu.

Katika taarifa hiyo, Pompeo anaeleza kuwa taarifa za waangalizi wa uchaguzi na taasisi za haki za binadamu zinaeleza kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu za haki wakati wa kampeni, kupiga kura na baada ya uchaguzi huo.

Uchaguzi wa Tanzania ulifanyika tarehe 28 Oktoba 2020 katika mazingira yaliyodhihirisha ukosefu wa uhuru na haki. Tume ya Uchaguzi (NEC) ilimtangaza Dk. Magufuli akifuatiwa kwa mbali na Tundu Lissu wa Chadema aliyekuwa akipewa nafasi ya kushinda.

Taarifa inaendelea kutanabaisha kuwa wakati wa mchakato huo na baada ya uchaguzi, viongozi wa vyama vya upinzani, wanaharakati wa haki za binadamu, waandishi wa habari na wananchi wengi waliendelea kuonewa, kuteswa na kutishwa na vyombo vya ulinzi na usalama vya serikali ya Tanzania.

Pia taarifa imegusia kuminywa na hatimaye kufungwa kwa intaneti, kuminywa kwa haki ya mawasiliano kwa umma ambayo inatambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN). Mitandao ya kijamii – Facebook, Twitter na Instagram ilifungwa wakati na baada ya uchaguzi.

Pamoja na kutotaja majina ya watu wanaowekewa vikwazo kwa sasa, SAUTI KUBWA ina taarifa kuwa walengwa wakuu ni Rais Magufuli mwenyewe na baadhi ya wasaidizi wake, viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi, Idara Usalama wa Taifa, na Tume ya Uchaguzi.

Marekani imesema inaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya Tanzania kuhusu namna viongozi wake na  vyombo vya ulinzi vinavyozingatia na kulinda haki za raia.

Hii ni mara ya pili kwa Marekani kuweka vikwazo kwa Baadhi ya viongozi wa Tanzania, wakati wa uongozi wa Rais Magufuli. Mara ya kwanza ilikuwa Januari Mosi, 2020 ambapo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliwekewa katazo la “kukanyaga” Marekani.

Katika taarifa yake, Marekani iliseka inaweka katazo hilo kwa Makonda kwa kuwa mshirika mkuu katika matendo ya kukomesha uhai wa baadhi ya wananchi, hasa wakosoaji wa serikali ya Rais Magufuli.

Marekani ilisema iliamua kuchukua hatua hiyo baada ya matokeo ya uchunguzi mpana na wa kimfumo ambao ulifanywa na Wizara ya Usalama wa Ndani pamoja na ushirikiano na mashirika mengine ya serikali.

Marekani ilisema uamuzi huo ulitokana na Tanzania kutotaka au kushindwa kuheshimu usimamizi wa haki za binadamu. Ilielezwa pia kuwa Makonda alikuwa akituhumiwa “kuumiza” haki za wengine, wakiwamo mashoga, kuukandamiza upinzani pamoja na uhuru wa kujieleza.

Like
1