Tanzania yapoteza bilioni 690 za kodi inayofichwa


TANZANIA inapoteza karibu shilingi bilioni 690 (dola 300 milioni) za kodi kila mwaka kutokana na kampuni kubwa na watu biafsi kulipa kodi kidogo au kukwepa kabisa.

Hasara ambayo serikali inapata kwa sababu hii, ingetosha kulipa mishahara ya wauguzi 135,577 kila mwaka.

Imebainika kuwa hasara ya kodi hii ni zaidi ya asilimia 38 ya bajeti nzima ya afya na utabibu kwa mwaka.

Juni 2020, Bunge lilidhinisha bajeti ya Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Ustawi wa Jamii ya shilingi bilioni 900 kwa mwaka 2020/21. Serikali imepanga kukusanya Shilingi bilioni 467.8, na kati ya hizo bilioni 155 zilitajwa kutoka vyanzo vya ndani.

Ripoti ya kila mwaka inayotolewa na Mtandao wa Haki Zinazohusiana na Kodi (TJN) inaeleza kuhusu kuimarika kwa ulipaji kodi duniani na juhudi za serikali kukabiliana na tatizo la kukwepa haki hiyo na kubainisha kuwepo kwa kiwango kinachoongezeka kwa matajiri kukwepa kulipa kodi.

Ripoti hiyo inaeleza juu ya utafiti wa kwanza wa kupima kiasi gani kila nchi inapoteza kodi kupitia kodi za kampuni na zile zinazolipwa na watu binafsi.

Tanzania inapoteza kiasi kikubwa cha kodi ambayo ni sawa na asillimia 14.13 bajeti ya elimu kwa mwaka. Bunge la Tanzania liliidhinisha bajeti ya shilingi trilioni 1.3 kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021.

Kulingana na uchunguzi wetu, imegundulika kwamba vitendo vya ulaghai katika masuala ya kulipa kodi vimeenea zaidi katika mfumo wa kuingiza bidhaa nchini. Kitengo Kitengo cha Mipango, Sera na Utafiti katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kimekiri kuwepo kwa “ujanja-ujanja” katika eneo hili, ingawa kimeeleza kuwa hali “sasa imedhibitiwa.”

Upo ulaghai mkubwa nchini kwa wafanyabiashara wakubwa kutoa taarifa potofu kuhusu kiasi cha bidhaa zilizoingizwa nchini na pia kuficha bidhaa hizo na shehena za makontena kwa lengo la kukwepa kodi.

Kampuni kubwa, pamoja na wawekezaji wa kigeni, wakishirikiana na wataalam wa kodi wa ndani na baadhi maafisa wa TRA wasiokuwa waaminifu, wamejipanga kutapeli fedha kwa kutumia ankara za mashine za kielektroniki kudai Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kutoa taarifa za mauzo ya uwongo.

Uchunguzi wetu umebaini kuwepo kwa mashirika ya kimataifa yanayolipa mabilioni kidogo ya shilingi ya kodi pungufu ya kiwango kinachopaswa kulipwa. Kampuni hizo hufanya hivyo kwa kuhamisha kutoka nchi faida ya matrilioni ya shilingi yaliyopatikana nchini na kuyapeleka nchi ambako viwango vya kodi viko chini sana au kodi hizi hazipo.

Walipa kodi binafsi, hasa viongozi wakubwa serikalini na matajiri, wamebainika kuweka fedha nyingi nje ya nchi katika nchi ambazo hazina kodi na haziulizi fedha hizo zimepatikana kwa njia gani; iwe haramu ama halali kwao ni sawa tu.

Wakati nchi zenye kipato kikubwa hupoteza kodi zaidi kutokana na ukiukaji wa kodi unaofanywa na kampuni za kimataifa, ripoti ya “Hali ya Haki Zinazohusiana na Kodi” ya 2020 inaonyesha kuwa hasara hizo za kodi zina athari kubwa zaidi katika nchi za kipato cha chini.

Nchi za kipato cha juu kabisa hupoteza zaidi ya dola 382 bilioni kila mwaka wakati nchi zenye kipato cha chini hupoteza Dola 45 bilioni.

Lakini, hasara za kodi katika nchi za kipato cha chini ni karibu sawa na asilimia 52 ya bajeti zao za sekta ya afya, wakati upotezaji wa kodi katika nchi za kipato cha juu ni sawa na asilimia nane ya bajeti zao za sekta ya afya. Vivyo hivyo, nchi za kipato cha chini hupoteza sawa na asilimia 5.8 ya mapato yote ya kodi ambayo kawaida hukusanya kwa mwaka mzima wakati nchi zenye kipato cha juu kwa wastani hupoteza asilimia 2.5.

Kutathmini ni nchi zipi zinahusika zaidi na ukiukaji wa kodi duniani ripoti ya “Hali ya Haki Zinazohusiana na Kodi” la 2020 linatoa ushahidi kwamba wawezeshaji wakubwa wa kukwepa kodi ni nchi tajiri zinazotawala uchumi dunia na “wategemezi wao.”

Lakini, nchi ambazo, kwa sababu za kisiasa, huonekana kwenye orodha ya Umoja wa Ulaya (EU) kama nchi zilizokubuhu kwa kukwepa kodi na visiwa vidogo vinavyoaminika kuwa vitovu vya ukwepaji wa kodi, havihusiki.

Dk. Lenny Kasoga, mchumi na mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania anasema kuwa, “mara nyingi, viongozi wa nchi maskini, hasa barani Afrika, wanaficha nje ya nchi pesa nyingi zilizopatikana kiharamu kwa faida zao binafsi. Na jambo la kuhuzunisha zaidi ni kwamba viongozi hawa wanashirikiana na matajiri kuwaibia watu wao masikini, na jambo hili ni upuuzi.”

Dk. Kasoga, alisema mifumo ya kodi iliyoshindwa kwa makusudi katika nchi nyingi ipo kulinda wale walio madarakani na washirika wao, pamoja na vyama vya siasa ambavyo ni kitovu cha ufisadi mkubwa wa nchi nyingi za Afrika.

Dt. Dereje Alemayehu, Mratibu Mtendaji wa Umoja wa Taasisi ya Haki Zinazohusiana na Kodi, anasema; “ripoti yetu ya 2020 inaonyesha ukubwa wa hasara inayopata nchi kwa kampuni na baadhi ya watu wake kukwepa kodi.

Imebainika kuwa nchi za kipato cha chini hupoteza zaidi ya nusu ya kile kinachokusanywa kwa ajili ya matumizi ya sekta ya sekta ya afya kila mwaka kutokana na udanganyifu na kuficha mapato halali ya serikali. Kodi hiyo inayopotea inagetosha kulipia mishahara ya kila mwaka ya wauguzi karibu milioni 18 duniani kila mwaka.

Anasema ni wakati muafaka sasa dunia kufanya mkutano wa wadau wote ili kuleta mageuzi katika mfumo wa kodi duniani. Kuwa na mfumo ambao unaendana kwa nchi zote na kuzuia kupokea kila fdha zinazotoka nje, hasa kwa wakwepa kodi, kunaweza kuikoa dunia na janga la nchi masikini kuendlea kuibiwa fedha zao.

Umoja wa Mataifa (UN) lazima usimamie hili ili kuwepo kwa mfumo wa kodi wa kimataifa kuwa wa haki na usawa, na unaheshimu haki zinazohusiana na kodi katika nchi zinazoendelea.” “

Mtandao wa Haki Zinazohusiana na Kodi umekosoa sana utaratibu wa Nchi za Umoja wa Ulaya (EU) kutengeneza orodha ya nchi zilizotengwa na umoja huo kwa sababu ya tuhuma za ukiukwaji wa kodi, ambapo orodha hiyo haujumuishi  nchi ambazo ni maficho makubwa zaidi ya kodi inayokwapuliwa kutoka nchi masikini, hasa za Afrika.

Imebainika kuwa EU imeorodhesha nchi za Palau na Trinidad na Tobago na kuamua kuziekea vikwazo kadhaa kwa kuwa zimeonekana kupokea na kuhifadhi fedha “haramu” lakini umoja huo umeacha nchi zenye idadi kubwa ya kampuni na watu biafsi wanaoficha fedha zao huko.

Hatua tatu ambazo lazima zichukuliwe na serikali

Mtandao wa Kimataifa wa Haki Zinazohusiana Kodi pamoja na mashirika, azaki,wanaharakati na wataalam anuai wa kodi na haki za binadamu duniani wanaungana Pamoja kushinikiza nchi kuchukua hatua zifuatazo ili kunusuru nchi masikini kuwa masikini Zaidi kwa kuibwa kodi zake. Njia hizo ni Pamoja na hizi zifiatazo;

Mosi, serikali zianzishe kodi ya ziada kwenye faida zinazotengenezwa na mashirika ya kimataifa yanayopata faida ya ziada, kama vile kampuni za simu na zile zinazohusika na mifumo ya kidigitali, kupunguza matumizi ya faida na kuziba mianya ya kutorosha fedha kutoka kampuni au watu binafsi.

Hatua nyingine inayopaswa kuchukuliwa na serikali ni kuanzisha kodi ambao itaratibiwa vyema na kutunzwa ili kutumika wakati wa majanga na milipuko ya ghafla ya magonjwa au hali ya hewa. Hali hii itapunguza fedha za maendeleo kutumika kudhibiti majanga hayo yanapotokea.

Pia, serikali zinapaswa kuitisha mikutano ya kodi  na nchi tajiri kujadili namna ya kudhibiti mifumo hafifu ya kodi inayotoa mwanya kwa kukwepa kodi na kuficha fedha katika nchi zisizotoza kodi kwa mapato haramu, hasa kutoka nchi masikini.

Like