Askofu Bagonza: Tusitese wengine kwa dhana ya kukomboa wanyonge

Katika ibada ya Ijumaa Kuu iliyoadhimishwa kitaifa katika Dayosisi ya Karagwe (KKKT), mkoani Kagera leo Aprili 19, 2019, Askofu Benson Bagonza, katika mahubiri mafupi na mazito, ametoa tafakuri juu ya mateso, uhuru, na utumwa – katika muktadha wa hali halisi tunayopitia kama taifa na kanisa. Kwa msaada wa teknolojia na watu wengine, nimechukua dondoo 11 kutoka katika tafakuri hiyo. Hizi hapa:
1. Sisi binadamu hatupendi kuteswa kama alivyoteswa Yesu. Lakini wewe binadamu usimtese mtu eti Bwana Yesu aliteswa.
2. Utesaji ni kama bangi ukiishamuingia mtu anapenda kila mara kutesatesa wengine.
3. Yesu aliteswa kwa ajili yetu. Huu ni upendo wa ajabu. Sisi binadamu tunapenda kupewapewa tu badala ya kuteswa. Haya ni mapendo ya kweli kwa binadamu. Ndani ya Kristu kulikuwemo na Umungu. Alibeba dhambi zetu ili sisi tuchukue utakatifu.
4. Kwa yote hayo hakuna lolote binadamu alichangia. Kwa alichotufanyia Kristu, tuchukie dhambi. Tujitolee kwa ajili ya wengine, ingawa hali ilivyo kwenye kanisa letu na taifa letu kujitolea imekuwa ni jambo la nadra.
5. Inatubidi tuonyeshe kuwa sisi ni watumwa waliokombolewa, na hivyo tusitese walio utumwani. Watumwa waliokombolewa hawafurahii utumwa; lakini (bahati mbaya) tabia ya watumwa ni kupenda kumiliki watumwa na kuwatesa.
6. Tunu ya Watanzania tuliyoirithi kwa Baba wa Taifa ni kuwa hatuwezi kuwa huru mpaka Afrika yote iwe huru. Uhuru wetu hauko kamili kama jirani yetu bado anateseka.
7. Tukikataa ukombozi wa Yesu tunajikomoa wenyewe.
8. Damu ya mwenye haki haimwagiki bure. Ikishamwagika, isipokomboa, itaangamiza. Kukumbatia umwagikaji damu ni kujiletea maangamizi. Maangamizi yake yanakwenda hadi vizazi vinne – ndivyo Biblia inavyosema.
9. Wanahitajika watu wateseke ili kukomboa wenzao. Wachache wakubali kuteseka ili kukomesha dhambi, na kuondoa kanisa na taifa katika mateso haya.
10. Unyonge wetu si mtaji wa wasaka tonge. Wanaojitolea wasitumie fursa hiyo kujinufaisha. Wanaopiga kelele kutetea wanyonge wasitufanye wanyonge na kujinufaisha kiitikadi na kiimani.
11. Tunalia sana dhidi ya ufisadi na rushwa, na kadhalika. Lakini umaskini wetu si mtaji kwa wasaka tonge kutesa watu wengine. Bwana Yesu hakujivunia unyonge na umaskini wetu.
Baada ya ibada ya Ijumaa Kuu Askofu Bagonza alitoa salaam za Pasaka kwa Watanzania, wakiwakilishwa na mkuu wa mkoa wa Kagera, ambaye alishiriki ibada hiyo. Hizi ni nukuu chache kutoka katika salaam hizo:
1. Mheshimiwa mkuu wa mkoa kwa kuwa huko hapa, nitumie fursa hii kukuomba ufikishe shukrani zetu kwa serikali na pongezi kwa kazi mnayoifanya. Kila siku  tunawaombea. Ninyi ni sehemu ya liturjia yetu na tunaamini Mungu anasikia maombezi yetu kwa ajili yenu.
2. Sisi huku Karagwe, tunaona jitihada zenu katika kutatua kero mbalimbali za kijamii. Kipekee sana tunapongeza jitihada za ujenzi wa hospitali ya Wilaya. Ni jambo jema na Mungu awabariki. Kwa kuwa sisi tumekuwa katika uendeshaji wa hospitali hapa wilayani kwa miaka 107; tunashauri msikimbie ushauri wetu. Sisi tunajua hospitali si majengo, na kwa hiyo, tuko tayari kutoa ushauri na uzoefu wetu.
3. Baba wa Taifa letu alipoulizwa wakati anastaafu kuwa angependa akumbukwe kwa jambo gani? Alijibu kuwa akumbukwe kuwa ALIJARIBU! Matatizo ya taifa letu ni mengi, taifa letu ni kubwa, na kwa hiyo, pale tusipoweza kutatua – TUJARIBU.
4. Wanyambo wa Karagwe wana msemo mmoja unaoonekana wazi katika tabia na makuzi yao. Msemo huo unatafsrika kwa Kiswahili kuwa “UKIMSIFIA MNYAMBO AKIWA KAZINI, ANAACHA NA KUDHANI AMEMALIZA”. Na msemo mwingine unaofanana na huo unasema “ANAYEDAI AMEFANYA KAZI NI YULE ALIYEMALIZA KAZI”. Kwa hiyo, usije ukashangaa ukiwa upande huu wa mkoa wako, utakapoona pongezi pongezi zinapungua, si kwamba watu hawaoni kazi nzuri unayoifanya. Wanasita wasije wakakusifia, halafu ukaacha kufanya kazi. Mungu akubariki kuitenda kazi yako bila kujali kama unashukuriwa. Na tayari nimeona na kusikia bidii yako na unyenyekevu wako. Napenda kukuhakikishia sala zangu na ushirikiano wangu. Ukisubiri shukrani, utasubiri sana. Mungu akubariki na aendelee kuibariki serikali yetu.
4. Dayosisi ya Karagwe kama mdau wa maendeleo na ustawi wa jamii hapa mkoani, tutaendelea kutoa mchango wetu ili kumfanya mwanadamu awe kamili kimwili, kiroho na kiakili. Hatuna uzoefu wa kumkatakata mwanadamu vipande vipande vya kiroho, kimwili, na kiakili. Tumeendelea kufundisha kila tunapopata nafasi kuwa:
– Mwanadamu mwenye roho tu bila mwili ni pepo
– Mwanadamu mwenye mwili tu bila roho ni maiti
– Mwanadamu asiye na akili ni hayawani.
Tumefanya hivi wakati wote kwa miaka 109 ya uwepo wetu kama kanisa hapa mkoani. Hatuna Uzoefu wa kubagua watu katika utoaji wa huduma tunazotoa. Ni kwa ajili hiyo, na kwa unyenyekevu, tutaendelea kukataa kuitwa SEKTA BINAFSI. Tunasita kukubali sifa hiyo kwa sababu Kanisa halimilikiwi na mtu yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu.
5. Zinazoitwa mali za Kanisa na huduma zake, ni mali za jamii na hutoa huduma kwa wote. Hata zile huduma zinazodaiwa kutengeneza faida, hiyo faida haiendi katika mfuko wa mtu binafsi, bali hurudi kwa jamii hiyo hiyo. Tunaomba likikosekana jina sahihi la kutuita, basi hata tuiteni taasisi zisizo za kiserikali lakini si sekta binafsi! Sisi ni wadau wa maendeleo kabla ya uhuru, na tutaendelea kufanya hivyo kwa sababu huduma hizo ni sehemu ya sisi kuitwa Kanisa la Kristo wa Nazareth. Hatuwezi kuacha kutoa huduma hizo kasha tukaendelea kuitwa Kanisa la Kristo.
6. Tutaendelea kufanya hivyo hata pale serikali itakapokuwa na uwezo wa kumpelekea huduma kila mtanzania nyumbani kwake. Tutawahudumia hata wale kwa sababu zao hawalipendi kanisa. Tunafanya hivyo kwa sabau hata Bwana Yesu alikula na  kushirikiana na wasaliti wake.
7. Mkoa wetu wa Kagera una baraka moja kubwa na hiyo hiyo inageuka na kuwa balaa la mkoa huu. Tuna mazao ya kudumu ya biashara na chakula (kahawa na migomba). Ni baraka kwa sababu hatulazimiki kulima na kupanda kila mwaka. Ni balaa kwa sababu hata wavivu wana uhakika wa kula. Kitu kinachodumu muda mrefu huua ubunifu na kujiaminisha kupita kiasi.
Mazao haya mawili ndio uhai wa mkoa huu na ustawi wa wakazi wake. Kukitokea changamoto yoyote katika mazao haya, furaha katika familia inapungua. Kanisa tunaamini, ustawi wa taifa lolote huanzia nyumbani. Kwa niaba ya wana Karagwe, tunaishukuru serikali kwa jitihada zinazofanyika kuboresha mazao haya mawili na kutafuta mengine mbadala. Serikali inayotaka kukaa mioyoni mwa wana Kagera, daima itafute kuboresha mazao haya. Na serikali inayotaka kukaa midomoni mwa wana Kagera, iwe ile isiyoshughulikia mazao haya mawili.  Na wana Karagwe wanajua faida na hasara za kukaa moyoni na mdomoni. Tiba ya magonjwa ya mazao haya, masoko mazuri na ya uhakika, na bei nzuri ni baadhi ya matatizo sugu yanayokabili mazao haya. Na ushauri wangu kwa serikali ni kujitahidi kurejesha nguvu ya maamuzi ya bei mikononi mwa wakulima wenyewe.
8. Ndugu zangu watanzania na watu wote wenye mapenzi mema, taifa letu ni moja na haligawanyiki. Lakini pia umoja wa kitaifa ni kama mmea. Unahitaji kutunzwa, kuwekewa mbolea, kunyweshwa maji, kupaliliwa, na kuukinga na wadudu wahalibifu.
Bila jitihada hizo, umoja waweza kunyauka au kunyongonyea. Sala yetu ni kuwa Mungu adumishe Uhuru na Umoja wetu. Wake kwa waume na watoto, Mungu aendelee kuibariki Tanzania yetu. Pale ambapo changamoto za umoja na mshikamano zimejitokeza na kwa kweli tumeziona; dawa yake ni kukaa pamoja.
9. Wale wanaodhaniwa kuwa hawakubaliki, wasikilizwe. Na wale wanaodhaniwa kuwa wanakubalika, waheshimiwe.
10. Kazi ya uongozi daima iwe ni ile ya kuleta watu pamoja kama alivyofanya Bwana wetu Yesu Kristo. Alipokabiliwa na upinzani wa Mafarisayo, Waandishi, Masadukayo na wapinzani wengine, aliwasikiliza, akawapa changamoto kwa njia ya hoja na iliposhindikana akasema, yaacheni magugu na ngano yakue pamoja, ukweli utajulikana wakati wa mavuno!
11. Furaha ya familia na hata taifa ni pale tunapokaa pamoja kama ndugu. Hata yule mchoyo huwa anaonywa wakati wa chakula, si kwa kunyimwa chakula.
12. Tanzania yenye amani na umoja ni tunda la dini zote, itikadi zote, makabila yote na jinsia zote. Tutaendelea kuombea Amani ya nchi. Tutaombea hekima kwa watawala na viongozi wetu. Tutaendelea kuombea mihimili yote ifanye kazi yake kwa uzalendo. Tutaendelea kuombea utawala sharia, haki na ustahimilivu. Tutaendelea kutoa ushauri wetu wa wazi na wa siri. Tutaendelea kutoa sauti yetu ya kinabii kama tulivyoapa kufanya. Daima tutakuwa tayari kuitumia kalama ya upatanisho aliyoiweka ndani yetu, Bwana wetu Yesu Kristo. Tutaendelea kujivunia kuwa watanzania.
Like
5

Leave a Comment

Your email address will not be published.