ACT yanusa ufisadi katika uchapishaji noti mpya

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimetoa taarifa fupi kwa umma inayoonyesha kuwa kinatilia shaka uadilifu wa wakubwa katika mchakato wa kuchapisha noti mpya unaoendelea, ambao SAUTI KUBWA imewahi kuandika habari zake wiki chache zilizopita. Ifuatayo ni taarifa ya chama hicho iliyotolewa leo na Ado Shaib, Katibu Mwenezi wa ACT:

Leo nilifanya mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia Ripoti ya Mwaka ya Ufanisi Katika Sekta ya Elimu (AESPR) ambayo pamoja na mambo mengine inatoa picha ya kuporomoka kwa elimu ya msingi kwa vigezo vya kupima uwezo wa kusoma, Kuandika na kuhesabu (KKK) kwa wanafunzi wa darasa la pili.

Katika mkutano huo, waandishi walitaka pia nigusie rai ya hivi karibuni ya Kiongozi wa Chama Ndugu Zitto Kabwe kwa Gavana wa Benki Kuu (BOT) kutoa kauli kuhusu mchakato wa uchapishaji tena wa noti (reprint).

Nimewaeleza waandishi wa habari kuwa chama cha siasa ni taasisi yenye wajibu wa kimapambano, kiusimamizi na kidira. Katika kutekeleza wajibu wetu wa kiusimamizi, tunaimulika Benki kuu na Serikali kwa ujumla ili kuhakikisha kwamba kila jambo linakwenda kwa kufuata utaratibu. Wajibu huu tunautekeleza na tutaendelea kuutekeleza bila hofu.

Hivyo basi, kuhusu uchapaji tena noti kutokana na uelewa na utafiti wetu yapo mambo tunayoyafahamu, yapo tunayoendelea kuyachunguza/kuyafuatilia na yapo ambayo hadi sasa hatujayafahamu.

*Kwa muhtasari* :

1. Tunafahamu kwamba ni kawaida kwa BOT kuchapa tena noti (reprint) kufidia noti zilizoharibika, kupotea au kutokana na kupanuka kwa uchumi. Noti chakavu na zizizofaa kwa matumizi huteketezwa na BOT kwa mujibu wa sheria;

2. Tunafahamu ndani ya BOT mchakato huo hufanyika kila baada ya miaka mitatu na mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2014.

3. Tunafahamu upo mchakato unaendelea ndani ya BOT wa kuyapata makampuni ya kuchapisha noti katika utaratibu huo.

4. Tunafahamu kwamba mbali na kigezo cha bei, kutokana na unyeti wake, mchakato wa kupata kampuni ya kuchapa fedha huzingatia hoja mbalimbali ikiwemo uwezo wa kampuni husika kutengeneza noti zenye kudumu, alama za kiusalama (security feuatures) na sifa za kimaadili za kampuni husika

5. Tunafahamu kwamba kwa kuzingatia sifa hizo na baada ya kupitia mchakato wa tenda, kampuni mbili za Crane Currency na De La Rue (ambao ndio wametengeneza noti zinazotumika sasa) zilichaguliwa tena kuchapisha noti (reprint).

5. Tunafahamu pia, kampuni moja ya kifaransa (Oberthur Fiduciare SAS) ililalamika kwa kuiandikia BOT kwamba ndio yenye bei ndogo na hivyo basi BOT kubatilisha maamuzi yake ya awali. Tunafahamu kwamba baadhi ya wakubwa BOT wanaipigia chapuo kampuni hii.

6. Kwa uchunguzi wetu, tunafahamu kuwa rekodi ya kampuni hiyo kwenye nchi nyingi ni ya kutilia shaka na kwenye nchi kadhaa kampuni hiyo imeingia kwenye kashfa ya ifisadi. Kwenye baadhi ya nchi kampuni hiyo imefungiwa kabisa kufanya kazi. Pia, kwa sababu ya vitendo vya kifisadi, kampuni hiyo haimo kwenye Taasisi ya Kimataifa ya Uadilifu wa Wachapisha Fedha (BnIE)

7. Jambo ambalo hatuna hakika nalo na tunaendelea kulichunguza ni wakubwa wanaoipigia chapuo kampuni hiyo ndani ya BOT wana maslahi gani? Wamelipwa? Kwa nini Serikali inayojinasibu kupambana na rushwa na ufisadi inaipigia chapuo kampuni yenye rekodi ya dhahiri ya rushwa na ufisadi?

8. Tunaendelea kufuatilia kwa karibu juu ya mchakato huu na tuna imani kwamba watanzania wenye nia njema wataendelea kutupatia taarifa muhimu ili tuendelee kulitetea na kulipigania taifa.

9. Tuna imani kuwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa italichunguza suala hili ili kuhakikisha mchakato huo ambao ni nyeti kwa usalama wa taifa na uimara wa uchumi wetu unazingatia uwezo na uadilifu wa makumpuni ya uchapaji wa fedha yanayoteuliwa.

Ado Shaib
Mwenezi ACT
0653619906

Like

Leave a Comment

Your email address will not be published.